Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  amewataka Watanzania kuchangamkia fursa zitakazotokana na  Mradi wa Ujenzi wa  Bomba  la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga Tanzania.

Rais Magufuli aliyasema hayo tarehe 8 Novemba, 2017, wakati alipofanya ziara katika Kiwanda cha Kagera Sugar kilichopo wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera.

Aliongeza kuwa, tayari Serikali imeweka mazingira ya kuwezesha mradi husika kupita nchini na kuhakikisha kwamba unatekelezwa, hivyo, jukumu la kutumia fursa za mradi husika ni la wananchi wenyewe.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizugumza wakati wa ziara ya Rais Magufuli alipotembelea kiwanda cha Sukari.

” Tayari Serikali imefanya sehemu yake. Sasa ni zamu ya watanzania kuona fursa zinazotokana na mradi huu na kuzifanyia kazi. Mradi utatekelezwa na kesho nitasafiri kwenda nchini Uganda kwa ajili ya Uwekaji Jiwe la Msingi kwa upande wa Uganda,”alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia kuhusu uzalishaji wa Sukari nchini alikitaka Kiwanda hicho kuongeza uzalishaji wa sukari kutokana na upungufu wa bidhaa hiyo nchini. Rais Magufuli alisema kuwa  hivi sasa nchi ina upungufu wa Tani  130,000 za sukari na kueleza kuwa, endapo viwanda vya ndani vitakuwa na uwezo wa kuzalisha kiasi kinachotosheleza mahitaji  cha Tani 450,000, atazuia uingizaji  wa bidhaa hiyo nchini, lengo likiwa ni kukuza ajira na kuwezesha mapinduzi ya viwanda.

Aidha, Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kipindi chote ambacho kimekuwa kikifanya shughuli za uzalishaji sukari tangu mwaka 2001.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati akizungumza katika ziara hiyo, alieleza mipango ya Serikali kuhusu miradi ya umeme nchini na kuutaja mradi wa  Ujenzi wa Miundombinu ya Kusafirisha Umeme wa Geita Nyakanazi wa Msongo wa kV 220  na kueleza kuwa, mradi husika unatarajiwa kuanza mwaka 2018.

Pia, Dkt. Kalemani alizungumzia kuhusu mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia  Maji wa Kakono wa Megawati 87 na kueleza kuwa, tayari fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi husika zimekwishapatikana.

Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, aliwataka viongozi wa Serikali za Mitaa katika maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha kwamba, wakati wa utekelezaji wa mradi huo, maeneo yanayotoa huduma za kijamii ikiwemo shule na zahanati kuhakikisha kwamba yanapewa kipaumbele.

Akizungumzia hali ya umeme kwa Mkoa wa Kagera alieleza kuwa, ni ya wastani na kwamba jula ya kiasi kinachozalishwa katika mkoa huo ni megawati 18.2, na umeme unaozalishwa na kiwanda hicho wa kiwango cha megawati 5.8 umeingizwa katika Gridi ya Taifa.

Akizungumzia mipango ya kiwanda hicho kuzalisha umeme alisea kuwa, kiwanda hicho kimepenga kuongeza ualishaji umeme kutoka megawati 5 mpaka 6  na baadaye kimepanga kufikisha megawati 30.

Viongozi wengine wa Wizara walioshiriki katika ziara hiyo ni Katibu Mkuu wa Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua na Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli Mhandisi Innocent Luoga.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. Hamis Mwinyimvua ( wa kwanza kushoto), Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli Mhandisi Innocent Luoga (wa pili kushoto) na Viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania Mkoa wa Kagera wakiteta jambo wakati wa ziara ya Rais Magufuli Kiwanda cha Kagera Sugar.

Rais Magufuli na ujumbe wake wanatarajia kusafiri tarehe 9 Novemba, 2017, kuelekea nchini Uganda kwa ajili ya kuhudhuria Sherehe za Uwekaji Jiwe la Msingi la Mradi huo kwa upande wa Uganda zitakazofanyika tarehe 11 Novemba, 2017.

Tayari sherehe kama hizo kwa upande wa Tanzania zilifanyika tarehe 5 Agosti, 2017 katika eneo la Chongoleani jijini Tanga mahali ambapo kutajengwa gati ya kushusha mafuta kwa ajili ya kusafirishwa nje.

Na Asteria Muhozya, Bukoba