Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati, wametia saini makubaliano ya msaada kutoka Shirika hilo utakaowezesha Mpango wa Mafunzo kwa watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) hususan katika usimamizi wa miundombinu ya usambazaji na usafirishaji wa umeme.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Novemba 17, 2017 Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, kati ya Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga, akiwakilisha Serikali na Mkurugenzi kutoka JICA, anayeshughulikia masuala ya nishati, Hiroto Kamiishi.

Akielezea kuhusu mafunzo husika, Kamishna Luoga amesema kuwa, yanalenga kuwaongezea uwezo wahandisi na mafundi mchundo na kwamba yatatolewa kwa njia ya vitendo, hivyo mbali ya kutoa elimu, pia miundombinu husika katika nchi nzima itakarabatiwa.

Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) na Mkurugenzi kutoka JICA, anayeshughulikia masuala ya nishati, Hiroto Kamiishi (kulia) wakipeana mikono baada ya kutia saini makubaliano ya msaada kutoka JICA kuwezesha sekta ya nishati nchini.

“Mradi huu umelenga zaidi kusaidia kuondoa tatizo la upotevu wa umeme wa kiufundi (technical losses) na hivyo kusaidia TANESCO kuongeza mapato,” amefafanua.

Akifafanua zaidi, Kamishna Luoga ameeleza kuwa, hii ni Awamu ya Pili ya Mradi husika ambayo ni ya kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2018 hadi 2021. “Katika mwaka wa kwanza, Mradi utatekelezwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na miaka miwili utatekelezwa katika Mikoa mingine yote nchini.”

Aidha, Kamishna Luoga (kwa niaba ya Serikali) amewashukuru JICA kwa misaada na mikopo wanayotoa katika kuwezesha miradi mbalimbali ya sekta ya nishati nchini ikiwa ni pamoja na Mradi mkubwa wa Backbone, Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida Tanzania hadi Isinya Kenya, pamoja na Mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa megawati 300 ulioko Mtwara.

“Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO, inaahidi kutoa ushirikiano katika kutekeleza Mradi huu na mingine yote, amesisitiza.”

Awamu ya kwanza ya Mradi huu, ambayo pia ilifadhiliwa na JICA ilitekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.

Na Veronica Simba – Dodoma