Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na Naibu Waziri Subira Mgalu kwa pamoja wamekutana na Wadau mbalimbali kutoka Sekta Binafsi na kujadiliana namna bora ya Kuongeza na Kuboresha hali ya upatikaji wa Nishati ya Umeme nchini wakilenga kuipeleka Tanzania katika uchumi wa Viwanda.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wadau mbalimbali kutoka Sekta za Umma na Binafsi katika mkutano maalum wa majadiliano ya jinsi ya kufanya ushirikiano wa kibiashara baina ya Serikali na sekta binafsi, kikao hichi kilifanyika katika ukumbi Hazina.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Nishati Makao Makuu Dodoma, Dkt. Kalemani aliwapongeza wadau wa sekta binafsi kwa uwasilishaji wa Mpango unaonyesha jinsi Sekta binafsi zinavyoweza kuongeza uzalishaji wa Nishati ya umeme nchini kufikia megawati 10,000 ifikapo 2025.

Baada ya kupokea Mpango huo, Dkt. Kalemani alieleza kuwa Serikali kupitia wizara ya Nishati imejikita katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme kwa kuhakikisha kuwa  inaweka mazingira rafiki  kuanzia  katika utungaji wa Sera, Sheria, Uzalishaji, Uunganishaji  mpaka  Usambazaji na kuongeza kuwa, Mazingira hayo yanatoa fursa kwa sekta binafsi kuweza  kushirikiana na Serikali kuboresha sekta husika.

Akielezea zaidi kuhusu miradi ya kuzalisha umeme nchini, Dkt. Kalemani alisema kuwa, Serikali ipo tayari  kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika  kutekeleza miradi mbalimbali akitolea mifano miradi ya uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia  na kuutaja mradi wa Somangafunga wa megawati 240, Kinyerezi Awamu ya tatu  wenye megawati 300 na mradi wa Kinyerezi Awamu ya  Nne  wa megawati 300.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (aliyekaa katikati) na Naibu waziri Subira Mgalu kushoto pamoja na Makam Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini (TPSF), Salum Shamte wakiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi zinazoshughulika na uzalishaji wa umeme.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Subira Mgalu alisisitiza kuwa serikali inatambua mchango wa sekta binafsi na itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wa maendeleo kwa lengo la kuleta maendeleo ya kiuchumi yanayounganisha Sekta ya viwanda.

Kikao hicho kilichofanyika tarehe 18/1/2018 na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANZANIA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF) Kampuni ya Winds East Afrika Ltd, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha na Mipango.