Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu amewataka Madiwani kupitia Mabaraza yao kujadili masuala yanayohusu Sekta ya Nishati  ikiwemo kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania  (TANESCO).

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu, akisisitiza jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri Wilayani humo.

Amesema endapo masuala ya Nishati yatajadiliwa katika mabaraza hayo yatasaidia kuwepo msukumo kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo katika maeneo yao na hivyo kuongeza kasi ya utekelezaji wake kwa kuzingatia umuhimu wa nishati hiyo.

Naibu Waziri Mgalu aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA Wilayani Kahama ambapo alitembelea Kata na vijiji mbalimbali  wilayani humo.

Aidha, aliwataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi husika kuhakikisha kwamba wanatoa taarifa za utekelezaji wa majukumu yao katika Ofisi za Wilaya na vijiji katika maeneo wanayotekeleza miradi hiyo.

Akifafanua zaidi kuhusu utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Tatu alisema kuwa, Serikali imelenga kuhakikisha kuwa vijiji vyote vilivyosalia katika utekelezaji wa REA awamu ya I na ya II vinafikiwa na nishati hiyo  na kuongeza kuwa, “fedha za umeme zipo lakini lazima serikali ijiridhishe kuhusu namna mradi unavyotekelezwa”.

“Viongozi wote wakuu wamekwishasema vijiji vyote kunakopita miundombinu ya umeme haviwezi kukosa umeme. Kwetu sisi kuwaletea wananchi umeme ni agizo, lazima tulitekeleze,”alisisitiza Mgalu.

Naibu Waziri aliwataka wananchi waendelee kuunga  mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ya REA na kuongeza kuwa,  ina manufaa makubwa kwa taifa katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Akiwa katika Kata ya Zongomela, Naibu Waziri alitembelea eneo kunakofanyika shughuli za uchimbaji madini ambako aliwataka TANESCO ifikapo tarehe 2 Machi, 2018 kufanya tathmini ya mahitaji ya umeme kwa ajili ya shughuli za uchimbaji. Awali, wachimbao walimweleza Naibu Waziri kuwa, wanatumia majenereta kwa ajili ya shughuli zao.

Mmoja wa wananchi akieleza jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya wa Kahama Fadhili Nkurlu alitoa onyo kwa wote wenye lengo la kufanya udanganyifu wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na kueleza kuwa, watakaobainika watashughulikiwa.

Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi wa REA Hussein Shemdasi aliwataka wananchi kutunza miundombinu ikiwemo kuachana na tabia ya wizi wa mafuta ya transfoma kwa kuwa serikali inatumia gharama kubwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Baadhi ya Kata alizotembelea wakati wa ziara hiyo ni pamoja na Kata ya Iboje, Nzogomela,  Kisuke na Isaka Jana

Na Asteria Muhozya, Kahama