Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuanzia Julai 1, 2018, Serikali inatarajia kusitisha rasmi uagizaji wa mita za umeme kutoka nje ya nchi ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani kuuza mita zinazozalishwa nchini.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa kiwanda cha kuzalisha mita cha Baobab Energy Systems, Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mara baada ya kuzindua kiwanda hicho jijini Dar es Salaam

Dkt. Kalemani aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizindua kiwanda cha kutengenezea mita za Luku cha Baobab Energy Systems kilichopo Mbezi jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wataanza kununua mita hizo za LUKU na ikifika mwezi Julai mwaka huu, kama  mita hizo zitaonesha ubora na viwanda  vya ndani kuzalisha mita zinazotosheleza mahitaji,  Serikali itasitisha uagizwaji wa mita kutoka nje ya nchi.

“Miezi miwili iliyopita nilikuja hapa na Wataalam wangu kukagua, tulitaka kujiridhisha kama kweli kiwanda hiki kinakidhi mahitaji, viwango na ubora wa mita za LUKU na mlitupa taarifa kuwa  mna uwezo wa kuzalisha takriban mita Laki Tano kwa mwaka huku mahitaji ya TANESCO ikiwa ni takriban mita Laki Tatu kwa mwaka,” alisema Dkt Kalemani.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini una faida mbalimbali ikiwemo kupungua kwa gharama za usafirishaji, mita kupatikana kwa haraka na kwa gharama nafuu.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe ikiwa ni uzinduzi wa kiwanda cha kuzalisha mita cha Baobab Energy Systems. Wengine katika picha ni Watendaji wa Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Awali, alipotembelea kiwanda hicho mwezi Machi, mwaka huu, Dkt Kalemani alisema kuwa  ununuaji wa mita zinazozalishwa nchini  utapunguza gharama “ Mfano gharama ya  mita moja ya njia moja ya umeme (single phase) kutoka nje ya nchi ni shilingi 150,000 na njia Tatu za umeme (three phase)  ni mpaka shilingi Laki Saba lakini mita zinazozalishwa nchini unazipata si kwa zaidi ya shilingi 120,000 kwa mita za njia moja ya umeme na haizidi shilingi  Laki Nne na Nusu kwa mita za njia Tatu za umeme,” alisema.

Aidha, Waziri aliipongeza TANESCO kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana wakati wote nchini na kusema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto kutokana na ukubwa wa nchi, TANESCO imejitahidi kupeleka umeme katika kona zote nne za Nchi.