Tarehe 30 Mei, 2018 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alifanya ziara katika vituo vya kupoza umeme vya Kurasini, Kigamboni  na kiwanda cha kutengeneza mita za LUKU cha Ihemeter  Tanzania Limited. Lengo la ziara yake katika vituo vya kupoza umeme lilikuwa ni kuangalia maendeleo ya ukamilishwaji wa vituo husika. Akiwa katika vituo vya Kurasini na Kigamboni Waziri Kalemani alielekeza kuhakikisha ujenzi wake unakamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu. Aidha, alielekeza ujenzi wa majengo ya kituo kipya cha Kigamboni kilichopo Dege jijini Dar es Salaam kukamilika mwezi Julai mwaka huu na kusisitiza mradi mzima kukamilika mapema Desemba mwaka huu.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani pamoja na watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) akiendelea na ziara katika eneo la kituo kipya cha kupoza Umeme cha Kigamboni lililopo Dege jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani akizungumza na wananchi wa Mbutu wilayani Kigamboni alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linawaunganishia wananchi huduma ya umeme mara moja ili kuondokana na changamoto ya ukosefu wa umeme.

Wakati huohuo, Waziri Kalemani akiwa katika kiwandacha kutengeneza mita za LUKU cha Ihemeter Tanzania Limited, alipongeza uzalishaji wa kiwanda hicho ambao umefikia hadi mita milioni moja kwa mwaka na kulitaka Shirika la TANESCO pamoja na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa miundombinu ya umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutumia mita hizo baada ya kujiridhisha na ubora wake. Aliitaka kampuni ya Ihemeter Tanzania Limited kuongeza uzalishaji wa mita zenye ubora na kupunguza gharama ili waweze kusambaza mita nyingi zaidi. Aidha aliitaka kampuni ya Inhemeter kuanza kuzalisha bidhaa za aina nyingine kama nyaya ili vifaa vya umeme viweze kununuliwa nchini pekee na kuepuka gharama kubwa ya kuagiza nje ya nchi.