Posts by energy

Ujenzi mradi wa umeme Rufiji kuanza mwezi Juni mwaka huu

Imeelezwa kuwa ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji utakaozalisha  megawati 2115 unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15 mwezi Juni mwaka huu.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (wa pili kushoto) wakiwa katika eneo kunapojengwa nyumba zitakazotumiwa na mkandarasi atakayejenga mradi wa umeme wa Rufiji zilizopo katika eneo hilo la mradi.

Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani katika eneo utakapotekelezwa mradi huo wilayani Rufiji mkoani Pwani mara baada ya kukagua  kazi za ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi huo ikiwemo barabara, umeme, maji na reli.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati aliambatana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu na Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa.

Viongozi wengine walioshiriki ziara hiyo ni makatibu wakuu kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Mifugo na uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Dkt. Kalemani alisema kuwa,  mkandarasi  ambaye ni Arab contractors amepewa miezi 36 ya ujenzi wa mradi huo na miezi sita ya maandalizi hivyo inatarajiwa kuwa mradi utakamilika mwezi Aprili  mwaka 2022.

Kuhusu ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi, Dkt Kalemani alisema kuwa kazi za ujenzi wa miundombinu hiyo iliyoanza miezi tisa iliyopita imekamilika kwa zaidi ya asilimia 80 .

Aliongeza kuwa, ili kutekeleza mradi huo, jumla ya megawati 30 zitahitajika katika eneo hilo ambapo mpaka sasa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeshafikisha megawati 10 huku  mahitaji ya umeme kwa sasa yakiwa ni megawati 7.

Hivyo,  aliiagiza  TANESCO kuendelea kuratibu kazi hiyo ili nishati hiyo isiwe kikwazo cha kuchelewesha utekelezaji wa mradi.

Aidha pamoja na kuzipongeza  taasisi zote zinazohusika na mradi huo,  alitoa wito wa kuendelea kushirikiana ili kukamilisha kazi ndani ya wakati na kwa ufanisi kwani mradi huo ni wa Serikali.

Miundombinu ya reli katika Kituo cha Fuga wilayani Rufiji mkoani Pwani ambayo inaboreshwa ili kuweza kutumika kushusha mizigo wakati wa utekelezaji wa mradi wa umeme wa Rufiji.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwapongeza TANESCO kwa kutekeleza kazi zao kwa ufanisi katika eneo hilo la mradi na  viongozi wa wizara ya nishati kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.

Alisema kuwa,  Wizara hiyo ilipewa kazi mbalimbali ikiwemo kupima eneo lote la mradi na kueleza kuwa wameshamaliza kupima maeneo mawili ya mradi huo ambapo eneo la kwanza ni litakalojengwa mitambo ya umeme lenye hekta 1402 ambalo mchoro wake umekamilika.

Pia, Wizara hiyo  imepima eneo lenye hekta 4711 litakalojengwa nyumba za kudumu za wafanyakazi na kwamba wameshaweka alama katika maeneo hayo ambapo alimkabidhi Waziri wa Nishati michoro ya maeneo hayo ili taratibu nyingine za umiliki ziendelee.

kwa upande wake,  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  alisema kuwa,  Wizara yake inaendelea majukumu mbalimbali yatakayowezesha kuanza kwa mradi huo ikiwemo usafishaji wa sehemu itakayokuwa ni bwawa la kuhifadhia maji ya kuzalishia umeme.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tano kushoto) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (wa pili kulia) wakiangalia kazi ya urekebishaji wa miundombinu ya barabara katika eneo kutakapojengwa mradi wa umeme wa Rufiji. Wengine katika picha ni viongozi kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo.

Aliongeza kuwa,  kazi hiyo wameigawa katika  blocks 30 na kwamba blocks 27 zimeshapata watu wa kufanya kazi hiyo na baadhi ya waombaji tayari wanaendelea na kazi husika.

Kuhusu ulinzi alisema kuwa, wanatoa ulinzi katika eneo hilo na kwa watu wote wanaofanya kazi za mradi na kwamba awali kulikuwa  na askari 115 lakini wameongeza askari wengine 115 ili kukidhi mahitaji na kueleza kuwa idadi hiyo itaongezeka kadri kazi zinavyoongezeka.

Viongozi waliohudhuria ziara hiyo kutoka Wizara ya Nishati, ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna Msaidizi anayeshughulikia maendeleo ya nishati, Mhandisi Juma Mkobya na Kaimu Mkurugenzi Msadizi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Lusajo Mwakaliku.

Na Teresia Mhagama, Pwani.

Read more

Dkt. Kalemani aridhishwa na kasi ya uboreshaji wa kituo cha umeme cha Zuzu

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na kasi ya kampuni ya KEC ya nchini India ambayo imepewa kazi ya kujenga miundombinu ya umeme katika Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, Dodoma ambacho kinaongezewa uwezo wa  megawati 400 mbali ya megawati 48 za sasa.

Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani kuhusu mitambo ya umeme katika kituo cha kupoza cha Mjini Dodoma.

Dkt. Kalemani ameyasema hayo leo jijini Dodoma baada ya kufanya ziara ya kukagua vituo mbalimbali vya kupoza umeme ikiwemo cha Msalato, Mnadani na Zuzu ambapo aliambatana na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati.

Hata hivyo, Dkt Kalemani ameeleza kuwa, mkandarasi huyo anapaswa kukamilisha kazi hiyo mwezi januari mwakani ili kuweza kuboresha zaidi hali ya upatikanaji umeme jijini Dodoma ambapo kazi ya uunganishaji umeme kwa wananchi inaendelea na hivyo kuongeza matumizi ya nishati hiyo muhimu.

Dkt. Kalemani amesema kuwa,  mkandarasi huyo anafanya kazi tatu ambazo ni kushusha umeme kwa kV 400 katika kituo hicho, kujenga kituo cha kupoza umeme cha uwezo wa megawati 400 na kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.

Ameongeza kuwa, mkandarasi huyo alianza kazi hiyo mwezi Machi mwaka 2018 ambapo gharama ya mradi huo ni Dola za Marekani milioni 53 ambazo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Baadhi ya mitambo ya umeme katika kituo cha kupoza umeme cha Zuzu jijini Dodoma.

Aidha, baada ya kukagua vituo hivyo vya kupoza umeme, Dkt Kalemani amewaagiza TANESCO kuhakikisha kuwa kila kituo kinakuwa na fundi sanifu atakayekuwa kituoni kwa masaa 24 ili inapotokea hitilafu ya umeme, iweze kutatuliwa kwa haraka.

Vilevile, Dkt Kalemani ameagiza kuwa, kila kituo kiwe na vifaa vya ziada vya umeme badala ya kusubiri kuagiza vifaa hivyo mara linapotokea tatizo hali inayopelekea wananchi kukosa umeme na kueleza kuwa ifikapo mwezi Machi mwaka huu atakagua utekelezaji wa agizo hilo na Meneja ambaye hatatekeleza, atachukuliwa hatua.

Aidha ametoa agizo kwa TANESCO kuweka walinzi katika miundombinu ya umeme kwani kumekuwa na matukio ya baadhi ya wananchi kuhujumu miundombinu hiyo kwa namna mbalimbali ikiwemo kukata nguzo za umeme na pia ametoa wito kwa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiusika.

Katika ziara hiyo pia Waziri wa Nishati alizungumza na wafanyakazi wa TANESCO katika kituo cha kupoza umeme kilichopo mjini Dodoma ambapo pamoja na kuwapongeza kwa kazi wanazofanya, alionya kuwa, katika mwaka 2019, mfanyakazi atakayeonekana amefanya uzembe utakaopeleka kukosekana kwa umeme, atachukuliwa hatua.

Na Teresia Mhagama

9/1/2019

Read more

Tanesco yapewa siku Tatu kuunganishia umeme Wizara 10 jijini Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka umeme katika Wizara kumi ambazo bado hazijalipia gharama ya kuunganishiwa umeme katika maeneo yao ya ujenzi kwenye Mji wa Serikali uliopo Ihumwa jijini Dodoma.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu) akizungumza na wafanyakazi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaofanya kazi ya kusambaza umeme katika Mji wa Serikali, Ihumwa jijini Dodoma.

Ameyasema hayo leo jijini Dodoma baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme na ujenzi wa majengo ya Serikali katika eneo hilo la Ihumwa ambapo aliambatana Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua.

Baadhi ya viongozi wengine alioambatana nao ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga.

Dkt. Kalemani amesema kuwa, Serikali imetoa transfoma kwa ajili ya kufungwa katika maeneo ya wizara zote 22 kwenye Mji wa Serikali ili kazi za ujenzi zifanyike usiku na mchana na hivyo kuwezesha ujenzi wa majengo kukamilika mwisho wa mwezi huu kama ilivyopangwa.

“ Tumeshatoa transfoma, na tunatarajia zifanye kazi, hivyo nimewaelekeza wataalam wangu kuwa pamoja na kwamba hizo Wizara hazijalipia gharama, transfoma zifungwe katika maeneo yao ndani ya siku Tatu na Wizara hizo zianze  kutumia umeme huo ndani ya Siku Tano kwani malipo ni 921,000 tu,” amesema Dkt Kalemani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (katikati), Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo (wa kwanza kulia), wakikagua kazi ya usambazaji umeme katika Mji wa Serikali, Ihumwa jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa,  jumla ya Wizara kumi ambazo tayari zimeshalipia umeme, Tanesco wanafanya kazi ya kuunganisha  nishati hiyo, ndani ya siku mbili.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati,  amemuagiza mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuongeza kasi ya ujenzi ili jengo hilo liwe limekamilika ifikapo tarehe 30 mwezi huu.

Aidha, ameeleza  kuwa, atakuwa akikagua kazi ya ujenzi wa jengo kila baada ya siku Tano ili kuona kama linaenda kwa kasi na ubora  kwa kuwa  mkandarasi huyo amekwilipwa fedha.

Na Teresia Mhagama

7/1/2019

Read more

Waziri wa Nishati ataka GGM watumie umeme wa gridi walipe kodi stahiki

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa mtambo wa kupoza umeme unaotarajiwa kujengwa Geita, kutawezesha serikali kupeleka umeme wa gridi ya taifa katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mine – GGM) na kuondoa sababu ya wao kutokulipa kodi stahiki kwa serikali kwa kigezo cha kutumia mafuta katika uzalishaji.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu-mbele), akikagua eneo kutakapojengwa mtambo wa kupoza umeme wa megawati 100 nje kidogo ya mji wa Geita, Desemba 31, 2018. Pamoja naye ni maafisa mbalimbali wa wizara, TANESCO, REA na mkandarasi CAMC Engineering kutoka China, atakayetekeleza mradi husika.

Akikagua eneo utakapojengwa mtambo huo, nje kidogo ya mji wa Geita, Desemba 31 mwaka huu, Waziri Kalemani alisema mtambo huo utafua umeme wa megawati 100 hivyo pamoja na kuwanufaisha wananchi wa Geita na maeneo jirani; utatosheleza pia mahitaji ya mgodi husika ambayo ni takribani megawati 25.

“Ni matumaini yangu, kufikia Desemba 2019, GGM watakuwa wameanza kutumia umeme wa gridi ya taifa ili waanze kulipa kodi stahiki kwa serikali. Waache kupata msamaha wa kodi wanaopata sasa kutokana na kuingiza mafuta wanayotumia kuendeshea shughuli zao mgodini,” alisema Waziri.

Waziri Kalemani aliongeza kwamba, kuwaunganisha GGM na umeme wa gridi, kutakamilisha azma ya serikali kuwaunganishia umeme wachimbaji wa madini wakubwa wote nchini kwani kwa sasa ni mgodi huo pekee uliobaki.

Alimtaka Meneja wa TANESCO Mkoa wa Geita, Mhandisi Joackim Ruweta kuwapa taarifa uongozi wa mgodi huo ili waanze kufanya maandalizi ya kuupokea umeme kwenye miundombinu yao.

Akizungumzia kuhusu mradi wenyewe, Waziri Kalemani alieleza kuwa serikali imetoa takribani shilingi bilioni 23 kwa ajili ya kuujenga ili kuboresha hali ya upatikanaji umeme kwa wananchi wa Geita na maeneo jirani. Alisema mradi unahusisha kusafirisha umeme mkubwa kutoka Bulyanhulu, umbali wa kilomita 55 hadi Geita.

Aidha, alisema kuwa taratibu zote za maandalizi zimekamilika hivyo akamtaka mkandarasi atakayetekeleza mradi huo, ambayo ni kampuni ya CAMC Engineering kutoka China kuanza mara moja shughuli za ujenzi, ambao kwa mujibu wa mkataba utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 17.

“Pamoja na kuwa mkataba unabainisha muda wa kukamilisha ujenzi ni miezi 17 lakini tumekubaliana na mkandarasi ajitahidi kukamilisha ndani ya miezi 12,” alifafanua Waziri.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mapinduzi, Buseresere mkoani Geita, kabla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo, Desemba 31, 2018 akiwa katika ziara ya kazi.

Akizungumzia majukumu ya mkandarasi kwa mujibu wa mkataba, Waziri Kalemani alisema yanajumuisha ujenzi wa mtambo wenyewe wa kupoza umeme katika eneo la Mpomvu, nje kidogo ya mji wa Geita, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bulyanhulu hadi eneo la mtambo, umbali wa kilomita 55 pamoja na kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji 11 vinavyopitiwa na mradi vikiwemo vya Nyantororo na Buyagu.

Waziri aliagiza mambo kadhaa yafanyike katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo ambayo ni pamoja na kujenga uzio kuzungushia eneo husika kwa sababu za kiusalama pamoja na kuepusha watu kuvamia eneo husika na kujenga makazi.

Pia, aliagiza kuanza mara moja kwa kazi za kusafisha eneo husika pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ambako mradi unapita ili wajue namna ya kujiandaa kuupokea mradi husika.

Waziri Kalemani alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ambapo mbali na kukagua eneo utakapojengwa mtambo huo, aliwasha umeme Katoro na Buseresere katika vijiji kadhaa pamoja na kuzungumza na wananchi.

Na Veronica Simba – Geita.

Read more

Waziri Kalemani awataka Wakandarasi miradi ya umeme kueleza mipango kazi yao kwa Viongozi

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote, kuwasilisha mipango-kazi yao kwa viongozi na wawakilishi wa wananchi wa maeneo wanakofanyia kazi ili waweze kuielewa hivyo kusimamia utekelezaji wake.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akimweleza dhamira ya ziara yake, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Colonel Magembe (kushoto) pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, alipowasili wilayani humo Desemba 30, mwaka huu, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Alitoa maagizo hayo jana, Desemba 30, 2018 wilayani Ukerewe akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.

Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, Colonel Magembe, Waziri Kalemani alifafanua kwamba viongozi na wawakilishi wa wananchi ndiyo wanawajibika kuisemea serikali, hivyo wanapaswa kuifahamu kwa kina miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao, waweze kuwaeleza wananchi.

“Hili ni agizo kwa wakandarasi wote wa miradi hii nchi nzima, wapatieni viongozi wa maeneo mnayofanya kazi mipango-kazi yenu, wajue nini mnatekeleza, kwa namna gani na kwa kipindi gani ili nao wasaidie kuwaelimisha wananchi wao,” alisisitiza Waziri.

Aidha, alitaja umuhimu mwingine wa viongozi kuelewa mipango-kazi ya wakandarasi kuwa itawawezesha kusimamia ipasavyo utekelezaji wake ikiwemo kuhoji pale ambapo watabaini mkandarasi anasuasua.

Akikagua utekelezaji wa miradi husika katika vijiji vya Chabilungo, Namasabo na Muluseni, ambako pia aliwasha umeme rasmi, Waziri Kalemani aliwasisitiza wananchi kulipia gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu ili wapate huduma hiyo na kuutumia umeme katika shughuli za kimaendeleo zitakazoboresha maisha yao.

Alisema, baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kulalamika kuwa serikali haiwapelekei umeme lakini ufuatiliaji unapofanyika inabainika kuwa wengi wao wanakuwa hawajalipia gharama husika.

“Ndugu zangu, lipieni ili muunganishiwe umeme, msibaki kulalamika tu,” alisisitiza.

Waziri pia aliwataka viongozi wa wananchi katika maeneo mbalimbali kusaidia kutoa elimu kwa wananchi wao ili wafahamu utaratibu wote wanaopaswa kuufuata katika suala la kuunganishiwa nishati ya umeme, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kujitokeza kwa wingi na kulipia gharama husika.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chabilungo wilayani Ukerewe, Desemba 30, 2018 kabla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Awali, akitoa taarifa ya hali ya umeme katika eneo lake, Mkuu wa Wilaya, Colenel Magembe alimweleza Waziri kuwa kati ya vijiji 76 vya Wilaya hiyo, 40 vimekwishaunganishiwa umeme.

Alimwomba Waziri kuwa, wananchi ambao hawajafikiwa na umeme wapelekewe pia ili waende sambamba na wenzao waliokwishaunganishiwa kwa kuutumia umeme katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Waziri aliahidi kutekeleza hilo huku akiwataka wananchi kuwa na subirá kwani mpango wa serikali ni kuwapatia wananchi wote umeme, zoezi linalotekelezwa hatua kwa hatua.

Waziri Kalemani anaendelea na ziara yake ya kazi aliyoianza Desemba 20, mwaka huu kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme katika mikoa mbalimbali ambapo anatarajia kuhitimisha Januari 2, mwakani.

Na Veronica Simba – Ukerewe.

Read more

Mji wa Serikali Ihumwa kupendezeshwa kwa njia ya Umeme inayopita chini ya ardhi

Imeelezwa kuwa eneo la Ihumwa, kunakojengwa ofisi za wizara na taasisi za serikali, litatandazwa mfumo wa njia ya umeme chini ya ardhi badala ya uliozoeleka wenye nguzo zilizosimikwa juu ya ardhi, ili kulipendezesha.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili-kushoto), akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Tumaini Nyale (kulia), wakati wa ziara aliyoifanya Desemba 28, 2018 kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya wizara na shughuli za upelekaji miundombinu ya umeme katika mji wa Serikali Ihumwa.

Hayo yalibainika jana, (Desemba 28, 2018) wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alipotembelea eneo hilo na kukagua shughuli za ujenzi wa ofisi ya wizara ya nishati pamoja na maeneo kunakopita miundombinu ya umeme.

Akitoa maelezo kuhusu mpango wa upelekaji umeme katika eneo hilo, Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga, alimweleza Waziri Kalemani ambaye alifuatana na Katibu Mkuu Dkt Hamisi Mwinyimvua, kuwa mbali na kuupendezesha mji huo wa serikali, pia mfumo wa umeme unaopita chini ya ardhi utasaidia upatikanaji wa nishati hiyo muhimu kwa uhakika.

“Unapokuwa na mfumo wa umeme unaopita chini ya ardhi, unakuwa na umeme wa uhakika na pia matengenezo mbalimbali kama vile kurekebisha nyaya zilizokatika yanapungua sana maana hauathiriwi sana kwa kuwa umefunikwa,” alifafanua.

Pia, Kamishna Luoga aliongeza kuwa, mfumo huo utaondoa kwa kiasi kikubwa tatizo la ukatikaji umeme.

Hata hivyo, alibainisha kuwa, mpango wa kutandaza mfumo huo ni wa muda mrefu ambao utaanza kutekelezwa siku za usoni na kwamba kwa sasa unatekelezwa mpango wa muda mfupi, unaohusisha kusambaza umeme eneo hilo kwa njia ya kawaida inayotumia nguzo zinazosimikwa juu ya ardhi.

Akieleza zaidi, Luoga alisema lengo la kuanza na mpango huo wa muda mfupi ni ili kusaidia kufanya kazi za awali, ambapo kufikia mwishoni mwa Januari mwakani, ofisi zote mahali hapo ziwe na umeme.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Tumaini Nyale, alimweleza Waziri na Katibu Mkuu kuwa, ofisi yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha eneo hilo linasambaziwa umeme kwa kasi. “Vifaa vyote vipo na kila mteja atakayelipia ataunganishiwa umeme mara moja.”

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye suti ya bluu) akijadiliana jambo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Josephat Kakunda (kushoto); walipokutana Ihumwa, wakati wakikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za wizara zao, Desemba 28, 2018. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua.

Waziri Kalemani, alitumia fursa hiyo kuwahamasisha viongozi wa wizara na taasisi zote zinazojenga ofisi zao Ihumwa, kulipia gharama za kuunganishiwa umeme, ili wapatiwe huduma hiyo muhimu na hivyo kuendelea na utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa ufanisi.

Alizipongeza wizara ambazo zimekwisha kuchukua fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, ambazo alizitaja kuwa ni Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Elimu na Nishati yenyewe.

Awali, akizungumza na mkandarasi anayejenga ofisi za wizara ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Waziri Kalemani alimtaka kuongeza kasi na kuhakikisha analeta vitendea kazi vyote eneo hilo, pamoja na kuongeza idadi ya vibarua ili akamalishe jengo hilo na kulikabidhi kwa wizara mwishoni mwa Januari mwakani kama yalivyo makubaliano.

Katika ziara hiyo, Kamati ya Wizara inayosimamia shughuli za ujenzi wa ofisi husika, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Raphael Nombo, ilishiriki pia.

Na Veronica Simba – Dodoma.

Read more

Waziri Kalemani aibua shangwe Iparamasa

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewasha umeme katika Kijiji cha Iparamasa, Wilaya ya Chato mkoani Geita, tukio lililoibua shangwe na nderemo kwa wananchi wa eneo hilo.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Iparamasa, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, akiwa katika ziara ya kazi Desemba 21, mwaka huu ambapo pia aliwasha rasmi umeme kijijini hapo.

Tukio hilo lilifanyika jana, Desemba 21, 2018 kijijini hapo, wakati Waziri akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuzungumza na wananchi.

Akizungumza na wananchi, Waziri Kalemani aliwataka wautumie umeme huo katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuendeshea viwanda vidogovidogo vya kusaga na kukoboa nafaka, kuchomelea vyuma na vingine vya aina hiyo.

“Umeme huu siyo kwa ajili ya kuwasha taa tu. Ni umeme unaotosha kwa matumizi ya viwanda, hivyo basi utumieni ipasavyo ili kuboresha maisha yenu,” alisisitiza Waziri.

Aidha, aliwahamasisha wananchi ambao hawajalipia, waendelee kulipia ili waunganishiwe huduma hiyo muhimu.

Halikadhalika, aliwashauri wananchi wenye matumizi madogo ya umeme, kutumia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ili kuondokana na gharama za kufunga nyaya katika nyumba zao.

Sambamba na hilo, alitoa vifaa vya UMETA 50 bure kwa ajili ya wazee na wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za kufunga nyaya za umeme.

“Mbali ya vifaa 250 vya UMETA ambavyo hutolewa bure kila eneo tunapowasha umeme kwa ajili ya wananchi watakaojitokeza mwanzo kulipia na kuunganishiwa umeme, mimi nikiwa kama Mbunge wenu, nawaongezea vifaa vingine 50 bure ili vifungwe kwa wazee na wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za kufunga nyaya za umeme,” alisema.

Kwa upande wa wachimbaji wadogo wa madini wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo, Waziri Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa Chato, aliwaambia kuwa alikwishaagiza mashine umba (transfoma) kubwa saba ambazo zitafungwa ili kuwawezesha kuendesha mitambo yao bila shida.

Mzee Yohana Masanyiwa akisoma risala kwa niaba ya wazee wa kijiji cha Iparamasa, Wilaya ya Chato; kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati wa hafla ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo, Desemba 21, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Geita, Mhandisi Joachim Ruweta, mpaka sasa jumla ya wateja 331 wamekwishaunganishiwa huduma ya umeme kwa Wilaya ya Chato, ambapo 16 kati yao ni kutoka kijiji hicho cha Iparamasa.

“Jumla ya waliolipia huduma ya kuunganishiwa umeme katika kijiji cha Iparamasa ni 36 lakini tumeshawaunganishia 16. Zoezi la kuunganisha wateja wengine linaendelea,” alifafanua Mhandisi Ruweta.

Waziri Kalemani yuko katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Kanda ya Ziwa hadi Januari 2, mwakani.

Na Veronica Simba – Chato.

Read more

Hali ya hewa isiwe kisingizio cha kuchelewesha miradi ya umeme vijijini- Mgalu

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaosambaza umeme  vijijini kutochelewesha utekelezaji wa miradi hiyo kwa kisingizo cha mabadiliko ya hali ya hewa kama vile uwepo wa mvua.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akikata utepe ikiwa ni ishara ya wananchi katika Kijiji cha Bulongwa wilayani Makete kuanza kupata huduma ya umeme. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Makete, Veronica Kessy.

Aliyasema hayo wilayani Makete mkoani Njombe  wakati alipokuwa akikagua kazi ya usambazaji umeme vijijini inayotekelezwa kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) mzunguko wa kwanza.

“ Kabla ya Serikali kuwakabidhi kazi hii ya usambazaji umeme vijijini, mlishafanya upembuzi wa maeneo mnayoenda kufanyia kazi na mnayafahamu vizuri, hivyo basi, iwe Jua au mvua, tunataka kuona kazi hii inaendelea kutekelezwa ili wananchi wengi wapate huduma ya umeme,” alisema Mgalu

Aliongeza kuwa, wakandarasi hao wanapaswa kuwa na mipango mbalimbali  ya utekelezaji wa kazi kulingana na hali ya hewa ya maeneo wanayofanyia kazi ili kuweza kusambaza umeme katika vijiji vyote walivyopangiwa na Serikali ifikapo Juni 2019.

Awali, Mkuu Wilaya ya Makete, Veronica Kessy, alimweleza Naibu Waziri kuwa, jumla ya vijiji 29 vimepangwa kuunganishiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ya usambazaji umeme vijijini, ingawa uongozi wa Wilaya hiyo umekuwa na wasiwasi na kasi yake katika usambazaji umeme.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme, alisema kuwa Wilaya  hiyo inapata umeme kutokea mkoani Mbeya lakini laini hiyo ni ndefu na inapelekea changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara hivyo aliomba Wilaya hiyo ipate laini nyingine ya umeme kutokea mkoani Njombe.

Kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alisema kuwa, Serikali ilishaona changamoto hiyo ya umeme wilayani Makete na kueleza kuwa Wilaya hiyo ipo katika mpango wa kupelekewa umeme  kupitia mradi wa Makambako- Songea ambao umekamilika.

Baadhi ya nguzo za umeme zilizosimamishwa katika Kijiji cha Usungilo wilayani Makete mkoani Njombe ambapo kijiji hicho kitapata umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza.

Akiwa wilayani humo, NaibuWaziri aliwasha umeme katika kijiji cha Bulongwa na kukagua miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Usagatikwa na Usungilo ambapo alimsisittiza mkandarasi kuongeza kasi ya  kusambaza umeme.

Wilaya ya Makete ina Vijiji 96 ambapo vijiji 29 tayari vimeshasambaziwa umeme, vijiji 29 vinasambaziwa umeme kupitia REA III mzunguko wa kwanza na Vijiji 38 vinavyosalia vitasambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu unaotarajiwa kuanza Julai mwakani.

Na Teresia Mhagama, Njombe.

Read more

Naibu Waziri wa Nishati aendelea kuwasha umeme vijijini mkoani Ruvuma

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ameendelea na ziara  ya ukaguzi wa miradi ya umeme mkoani Ruvuma ambapo leo amewasha umeme Kijiji cha Palangu na Mang’ua pamoja mtaa wa Luhila Seko katika Wilaya ya Songea ambavyo vimepata umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) mzunguko wa kwanza na mradi wa Makambako – Songea.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kulia) akikagua mitambo ya umeme katika kituo cha kupoza umeme cha Songea ambacho kimejengwa kupitia mradi wa umeme wa Makambako-Songea na kimeanza kusambaza umeme wa gridi kuanzia mwezi wa Tisa mwaka huu.

Huo ni muendelezo wa kazi ya ukaguzi na uzinduzi wa miradi ya umeme vijijini mkoani Ruvuma aliyoianza tarehe17 Disemba, 2018 kwa kuwasha umeme katika Vijiji Saba vilivyopo katika Wilaya ya Tunduru na Namtumbo ambapo wateja zaidi ya 200 wameunganishwa na huduma ya umeme.

Aidha, kuunganishwa kwa umeme katika Vijiji Palangu, Mang’ua pamoja na Mtaa wa Luhila Seko, wilayani Songea kumewezesha wateja zaidi ya 230 kuunganishwa na huduma hiyo huku wengine wakitumia umeme huo kwa shughuli za kiuchumi kama kusaga na kukoboa nafaka.

Pamoja na kuwasha umeme katika Vijiji hivyo, Naibu Waziri alikagua kazi ya usambazaji umeme katika Vijiji vya Liula, Mpangula na Litapwasi na kumsisitiza mkandarasi, kampuni ya Namis kufanya kazi kwa kasi na umakini ili kuondoa malalamiko ya wananchi ya kucheleweshewa huduma ya umeme.

Kuhusu Mkandarasi huyo, Naibu Waziri alisema kuwa, Serikali inaangalia kasi yake katika utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini mkoani Ruvuma na endapo atasua sua hadi kufikia mwezi ujao, atanyang’anywa kazi hiyo.

“ Serikali inatoa vipaumbele kwa wakandarasi wazawa kufanya kazi hizi za usambazaji umeme vijijini, lakini na sisi tunataka mfanye kazi kwa kasi na umakini ili kutorudisha nyuma juhudi za Serikali za kuwapelekea umeme wananchi,” alisema Mgalu.

Akiwa wilayani Songea, Naibu Waziri pia alifanya mazungumzo na  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ambapo walijadiliana  masuala mbalimbali kuhusu nishati ya umeme mkoani Ruvuma na baadaye alikagua  kituo cha kupoza umeme cha Songea kilichojengwa kupitia mradi wa Makambako-Songea na kinasambaza umeme wa gridi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.

Moja ya nyumba zilizounganishiwa umeme katika Kijiji cha Palangu wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) mzunguko wa kwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,  alimshukuru Naibu Waziri kwa kazi anazofanya ikiwemo ukaguzi wa miradi ya umeme katika sehemu za pembezoni mwa nchi na kueleza kuwa Mkoa wa Ruvuma sasa unapata nishati ya umeme ya kutosha na uhakika mara baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa Makambako- Songea.

Alisema kuwa Mkoa huo unapata umeme wa kiasi cha megawati 139, hata hivyo nyakati za mchana kiasi cha umeme kinachotumika ni megawati 11 na usiku umeme unaotumika ni megawati 3 hivyo alitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kuutumia umeme huo usiku na mchana kwa shughuli mbalimbali ikiwemo za maendeleo kwani umeme upo wa kutosha.

Kuhusu kiwango  hicho cha matumizi  ya umeme mkoani Ruvuma, Naibu Waziri alisema kuwa, kiwango hicho kitaendelea kuongezeka kwani  kazi ya uunganishaji  umeme kwa wananchi  inaendelea na wataitumia nishati hiyo kwa shughuli za maendeleo ambapo pia alitoa wito kwa wawekezaji  mbalimbali kuendelea kuwekeza mkoani humo.

Na Teresia Mhagama, Ruvuma.

Read more

Wilaya zenye majimbo mawili ziangaliwe kwa umakini katika miradi ya umeme vijijini – Mgalu

Naibu Waziri wa Nishati, Subira  Mgalu, amewataka wataalam katika Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa makini katika kazi ya upangaji wa vijiji vinavyopaswa kupelekewa umeme kwenye wilaya zenye majimbo mawili ya uchaguzi ili kuepusha malalamiko ya kupendelea upande mmoja wa Wilaya.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi, (hawapo pichani) kabla ya kuzindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Hanga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Namtumbo, Eng. Edwin Ngonyani na kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Sophia Mfaume.

Aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akikagua miradi ya usambazaji umeme vijijini katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ambapo Wilaya hiyo ina Jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo baada ya kupata malalamiko kuwa, Vijiji vingi vya Tunduru Kaskazini ndivyo vimesambaziwa umeme huku Tunduru Kusini ikiwa na Vijiji vichache.

Aidha, Naibu Waziri aliagiza kuwa, kazi ya upangaji wa Vijiji vinavyotarajiwa kupelekewa umeme kupitia miradi mbalimbali ishirikishe viongozi wa ngazi mbalimbali katika maeneo ili kuondoa malalamiko katika miradi hiyo.

Vilevile alisema kuwa, wataalam hao wahakikishe kuwa hawaruki Vijiji na badala yake kila kijiji kinachopitiwa na mradi kisambaziwe nishati ya umeme.

Kuhusu kazi ya uunganishaji Wilaya ya Tunduru  kwenye umeme wa gridi,  Naibu Waziri alisema kuwa, wilaya hiyo itaanza kupata  umeme huo kuanzia mwezi Machi mwakani baada ya kuvuta umeme kutokea wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

Akiwa wilayani Tunduru, Naibu Waziri, aliwasha umeme katika Kijiji cha Namiungo, Mchuluka, Kangomba na Daraja Mbili ambapo kaya zaidi ya 100 zimeunganishwa na huduma hiyo ikiwemo vituo vya afya na shule.

Naibu Waziri pia alifanya ziara katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambapo pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini, aliwasha umeme katika Kijiji cha Migelegele, Mtakanini na Hanga.

Baada ya umeme kufika  katika vijiji hivyo, jumla ya kaya 105 zimesambaziwa umeme huo zikiwemo Taasisi za umma na sehemu za ibada huku kazi hiyo ya uunganishaji umeme inaendelea.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika Kijiji cha Mtakanini, wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.

Wananchi mbalimbali katika vijiji vilivyosambaziwa umeme waliishukuru Serikali kwa kuwasambazia umeme huo ambao umewawezesha kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kupata huduma za matibabu hata nyakati za usiku tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Na Teresia Mhagama, Ruvuma.

Read more