Imeelezwa kuwa Bandari ya Mtwara itapokea mafuta tani za ujazo 8000 (lita milioni 9.6) ifikapo mwezi Septemba mwaka huu ikiwa ni mara ya Pili kupokea shehena hiyo ya mafuta kutoka yaliposhushwa kwa mara ya kwanza mwezi Juni mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 29 Agosti, 2018 na Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mjiolojia Erasto Simon, alipokuwa akiwasilisha ripoti ya Wizara ya Nishati kuhusu uanzishwaji wa gati la kupokelea mafuta katika bandari ya Mtwara kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini  jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hamisi Mwinyimvua waliwaongoza Watendaji mbalimbali wa Wizara na Taasisi zake katika utoaji wa taarifa na ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyojitokeza.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa kwanza kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (wa Pili kushoto) wakiongoza Ujumbe wa Wizara pamoja na Taaisisi zake katika kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

“ Kiasi cha tani za ujazo 8,000 kinatarajiwa kushushwa katika Bandari ya Mtwara ifikapo mwezi Septemba ambapo tani 5,000 kati ya hizo zitakuwa ni mafuta ya dizeli na tani 3,000 zitakuwa ni petroli,” alisema Simon.

Ameongeza kuwa, Serikali iliamua kutumia rasmi Bandari ya Mtwara kupokea mafuta ili kupunguza msongamano wa magari ya kusafirisha mafuta kwenda mikoa ya Kusini na nchi jirani.

Amebainisha kuwa, kwa mara ya kwanza mafuta yalipokelewa katika bandari ya Mtwara tarehe 28 Juni, 2018 ambapo kiasi cha tani 8,339 kilishushwa bandarini hapo na kupokelewa kwenye maghala ya kuhifadhi mafuta yanayomilikiwa na kampuni za GM & Company /Oryx na Oilcom Tanzania.

Amesema kuwa,  kiasi hicho cha mafuta kilichoshushwa mwezi Juni, tani 5,139 zilikuwa ni mafuta ya dizeli na mafuta ya petroli yalikuwa na ujazo wa tani 3,200.

Akizungumzia manufaa yatakayopatikana kupitia kufunguliwa kwa gati hilo la Mtwara, Simon alisema kuwa ni kupokea mafuta yote yanayokwenda nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji na hivyo kupunguza msongamano wa meli zinazoshusha mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na ujumbe kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake ukiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hamisi Mwinyimvua wakiwa katika kikao kilichojadili taarifa mbili za utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC) jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa, manufaa mengine ni kuchangia katika kukuza uchumi wa mikoa ya Kusini pamoja na kupunguza bei ya mafuta katika mikoa hiyo kutokana na bei hizo kupangwa kuanzia Mtwara tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kulikuwa na ongezeko la gharama za usafirishaji  mafuta kutoka Dar es Salaam hadi kufika mikoa ya Kusini.

“Mathalan, kwa mafuta yaliyoshushwa mwishoni mwa mwezi Juni 2018 bei elekezi iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilikuwa ni shilingi 2,329 kwa lita ya dizeli mkoani Mtwara wakati Dar es Salaam ilikuwa ni shilingi 2,360 kwa lita,” alisema Simon.

Na Nuru Mwasampeta