Serikali imebainisha kuwa jumla ya shilingi bilioni 499 zimeidhinishwa na Bunge kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme nchini kote katika mwaka huu wa fedha unaoendelea.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Chisichili Kata ya Mkonze mkoani Dodoma wakati wa ziara yake kujionea hali ya upatikanaji wa umeme.

Hayo yalisemwa jana, Januari 24 na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwa katika ziara katika maeneo mbalimbali ya Dodoma Mjini kwa ajili ya kujionea hali ya upatikanaji wa nishati hiyo muhimu pamoja na kuzungumza na wananchi.

Naibu Waziri Mgalu, ambaye aliambatana na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde aliwaambia wananchi wa maeneo aliyotembelea kuwa, kiasi hicho cha fedha ni kikubwa na kitawezesha utekelezaji wa miradi hiyo ya umeme katika vijiji vyote 7873 vilivyosalia nchi nzima.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais John Magufuli pamoja na Bunge la Jamhuri kutuidhinishia kiasi hicho cha fedha. Kazi yetu sisi wasaidizi wake katika Wizara ya Nishati ni kuhakikisha tunatekeleza jukumu alilotutuma la kuwapelekea wananchi kote nchini nishati ya umeme wa uhakika. Tunaahidi hilo litafanyika kwa ukamilifu.”

Akizungumzia umuhimu wa nishati ya umeme, Naibu Waziri alisema kuwa, sekta zote zinategemea umeme ili zifanye kazi kwa ubora. Alitoa mfano wa sekta ya afya ambayo pasipo umeme wa uhakika haiwezi kutoa huduma bora. “Vivyo hivyo kwa sekta ya elimu, kilimo, viwanda na nyinginezo,” alisisitiza.

Aidha, Naibu Waziri Mgalu alitoa maagizo kwa uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo wanatoa kipaumbele kwa taasisi za kijamii kama vile shule, vituo vya afya, nyumba za ibada, miradi ya maji na nyinginezo. Hata hivyo alisema Wakandarasi lazima wahakikishe hakuna mtu au eneo linalorukwa wakati wa kutekeleza mradi huo.

Vilevile aliwataka wananchi kufanya maandalizi ya kuunganishiwa umeme katika makazi yao na katika miradi na taasisi mbalimbali. “Tunataka zoezi la kupitisha umeme katika maeneo yenu likikamilika tu nanyi bila kuchelewa mnaunganishiwa katika nyumba zenu, hivyo anzeni kufanya maandalizi sasa.”

Awali, akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, alisema kuwa wananchi wa Dodoma ni wakulima wazuri wa zabibu na mazao mengine mbalimbali, hivyo wanahitaji huduma ya umeme wa uhakika ili kuboresha kazi zao za kilimo kwa kuanzisha viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani.

Wananchi wakiuliza maswali na kutoa maoni mbele ya Naibu Waziri Subira Mgalu (hayupo pichani) wakati wa ziara yake kujionea hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Dodoma Mjini.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zakayo Temu alisema zoezi la kufanya tathmini ya awali kwa ajili ya kutekeleza Mradi huo katika maeneo yaliyosalia litaanza mapema mwezi Februari mwaka huu.

Ziara ya Naibu Waziri Mgalu ilihusisha Kata za Mpunguzi, Matumbulu, Mkonze, Nala na Ipagala zilizopo Dodoma Mjini.

Na Veronica Simba – Dodoma