Archives for Latest Updates

Maandalizi ya ujenzi mradi wa umeme wa Rufiji yafikia zaidi ya asilimia 40

Imeelezwa kuwa, kazi mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji ( MW 2115) zinazofanywa na Mkandarasi kampuni ya ubia ya Arab Contractors na Elsewedy Electric  zimefikia zaidi ya asilimia 4O.

Moja ya nyumba inayojengwa na mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme wa Rufiji ambapo katika eneo hilo kunajengwa  kambi ya muda ya Wafanyakazi wa mradi huo.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambao walitembelea eneo la mradi lililopo wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, pamoja na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa nne kutoka mbele) wakiwa  katika eneo ambalo litatumika kutekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufanya  ziara katika eneo la mradi huo.

Kamati hiyo ya Bunge pia ilikagua miundombinu wezeshi iliyotekelezwa na Serikali ikiwemo  Barabara, umeme, nyumba za Wafanyakazi na sehemu maalum ya kushushia mizigo katika Stesheni ya Tazara katika Kituo cha Fuga.

Dkt. Kalemani, alisema kuwa,  Mkandarasi huyo ameanza kazi za maandalizi mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo la mradi mwezi wa Pili mwaka huu. 

Alisema kuwa, miongoni mwa kazi ambazo Mkandarasi  anaendelea kutekeleza kwa sasa ni ujenzi wa kambi ya muda ya Wafanyakazi, uletaji wa vifaa na mitambo itakayotumika wakati wa ujenzi pamoja na kazi za kuchukua sampuli za udongo na maji kwa ajili ya utafiti.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, (katikati), akizungumza na Wataalam wanaosimamia na wanaotekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufika katika eneo la mradi huo akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kukamilisha kazi hizo za maandalizi Mkandarasi huyo anatakiwa kumaliza kazi ya ujenzi ndani ya miezi 36.

Alieleza kuwa, pamoja na kuridhishwa na hatua hiyo ya maandalizi, bado Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea kumsimania mkandarasi ili amalize kazi ndani ya muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula,  baada ya kukagua miundombinu iliyotekelezwa na Serikali pamoja na kazi za maandalizi zinazofanywa na Mkandarasi, aliipongeza Serikali kwa kuamua kuutekeleza mradi huo na kuusimamia kikamilifu.

Alisema kuwa, Kamati hiyo pia inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini ambapo pia alitoa wito kwa Wizara kutorudi nyuma katika usimamizi wa mradi.

Pia, alitoa wito kwa wafanyabiashara hapa nchini kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mradi kwani Serikali itatumia takribani shilingi Trilioni 6.5 kutekeleza mradi huo hivyo ni muhimu watanzania wafaidike na fedha hizo.

Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali waliambatana na Kamati hiyo akiwemo Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka pamoja na wataalam kutoka kampuni inayotekeleza mradi huo.

Na Teresia Mhagama

14/3/2019

Read more

Kamati ya Bunge ya Bajeti yafanya ziara katika kiwanda cha Transfoma na kupongeza uzalishaji

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, George Simbachawene wametembelea kiwanda cha kuzalisha transfoma cha TANELEC kilichoko jijini Arusha ili kukagua masuala mbalimbali ikiwemo uwezo wake katika uzalishaji wa transfoma lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na vifaa vya umeme vya kutosha.

Katika ziara hiyo waliambatana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Baada ya kukagua shughuli za uzalishaji wa transfoma katika Kiwanda hicho, Wajumbe hao kwa nyakati tofauti waliwapongeza watendaji wa Kiwanda hicho kwa kuzalisha transfoma nyingi ambazo ni 14,000  kwa mwaka huku mahitaji ya transfoma nchini kwa mwaka yakiwa ni 10,000.

Aidha Wajumbe hao walipongeza uamuzi wa Serikali wa mwaka 2017 ambao ulielekeza kuwa miradi yote ya umeme nchini itumie vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini hali inayopelekea miradi hiyo kutekelezwa kwa kasi.

Wajumbe hao pia walimtaka Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo kuongeza uzalishaji na kuwa mbunifu kwa kuangalia pia masoko mengine ya transfoma na si kulenga miradi ya umeme ya ndani ya nchi pekee.

Awali, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alisema kuwa, Serikali ilichukua uamuzi wa kusitisha kuagiza nje vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme.

Alitoa mfano kuwa upatikanaji wa transfoma nje ya nchi unaweza kuchukua hadi miezi 12  hali wakati transfoma zinazozalishwa ndani ya nchi zinachukua muda mfupi kufika katika eneo zinapohitajika.

Aidha Waziri wa Nishati alisema kuwa, uagizaji wa transfoma nje ya nchi ni gharama kubwa kwani transfoma moja kutoka nje ya nchi inauzwa kwa takriban shilingi milioni Tisa wakati zinazozalishwa nchini ni takriban shilingi milioni 6.5.

Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TANELEC, Zahir Saleh alisema kuwa kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1981 kwa sasa kinazalisha transfoma kiasi cha 14,000 kwa mwaka.

Alisema kuwa,  kiwanda kinazalisha transfoma za uwezo wa kvA 50 hadi kVA 5000 na kufanya matengenezo ya transfoma kutoka nchi mbalimbali za Afrika kama Rwanda, Burundi na Kenya.

Aliongeza kuwa, uamuzi wa Serikali kuzuia kuagiza vifaa nje ya nchi umekinufaisha kiwanda hicho kwani kabla ya uamuzi walikuwa wakizalisha transfoma 7000 kwa mwaka lakini sasa wanazalisha transfoma 14,000.

Kuhusu ajira alisema kuwa, awali waliajiri wafanyakazi 30 lakini kwa sasa wafanyakazi walioajiriwa ni 70 na kwa mwaka huu wataajiri wafanyakazi wengine 40.

Vilevile alisema kuwa, kutokana na uamuzi huo wa Serikali, Kiwanda kinafanya kazi kwa faida na wameanza kupeleka gawio serikalini la takribani shilingi milioni 500 kwa mwaka 2018 na wanategemea kuongeza kiasi cha gawio hilo kwa miaka inayokuja.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene (wa kwanza kushoto) wakiongoza Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti katika kukagua kazi zinazofanywa na kiwanda cha transfoma cha TANELEC kilichoko jijini Arusha.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika kiwanda cha kuzalisha transfoma cha TANELEC kilichopo jijini Arusha. Wa Pili kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
[metaslider id=2595 cssclass=””]
[metaslider id=2597 cssclass=””]
Read more

Nchi za Mashariki mwa Afrika zadhamiria kuimarisha Uchumi kwa kuuziana Umeme

Nchi zilizopo Mashariki mwa Afrika, zimedhamiria kwa nia moja kuimarisha uchumi wao kwa kuuziana umeme kupitia mifumo ya kusafirisha nishati hiyo, iliyounganishwa katika ukanda husika.

Hayo yalibainishwa jana, Februari 21 mwaka huu, katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na umeme kutoka nchi za ukanda huo, ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP)

Baadhi ya Mawaziri/Naibu Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza hilo la Mawaziri la EAPP, Mhandisi Irene Muloni (Uganda) na wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati (Tanzania), Subira Mgalu. Walikuwa katika Mkutano wao wa 14 uliofanyika Entebbe, Uganda, Februari 21. 2019.

Akizungumza mara baada ya Mkutano huo uliofanyika mjini Entebbe nchini Uganda, Naibu Waziri wa Nishati (Tanzania), Subira Mgalu, alieleza kuwa, nchi wanachama wa EAPP wamelenga kuhakikisha wananchi wao wanakuwa na umeme wa kutosha, uhakika na wenye gharama nafuu.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri alitoa mfano wa Ethiopia na Misri ambao alisema wanazalisha umeme mwingi, hivyo wanaweza wakauzia nchi nyingine za ukanda husika ikiwemo Tanzania kwa bei nafuu.

Awali, akifungua Mkutano husika, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja huo, Mhandisi Irene Muloni (Uganda), alibainisha kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea katika sekta ya viwanda, pasipo kuwa na umeme mwingi, wa uhakika na wenye gharama nafuu.

Aliongeza kuwa, ni kwa sababu hiyo, nchi wanachama wa EAPP, zimedhamiria kwa dhati kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kuungana na kushirikiana katika kutumia kikamilifu vyanzo vyake vyote vya uzalishaji umeme ambavyo zimejaaliwa.

“Pamoja na nchi zetu kujaaliwa vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme vikiwemo maji, upepo, jua, gesi asilia na vingine vingi, lakini bado tunakabiliwa na umaskini wa nishati hiyo adhimu,” alifafanua.

Akizungumzia mifumo mbalimbali ya umeme inayounganisha nchi hizo, ambayo ikitumika vizuri itaunufaisha ukanda husika; aliitaja kuwa ni pamoja na njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 500 kutoka Ethiopia hadi Kenya, kilovolti 400 kutoka Tanzania hadi Kenya na msongo wa kilovolti 220 kutoka Kenya hadi Uganda.

Nyingine ni njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 220 kutoka Uganda hadi Rwanda pamoja na mifumo unganishi ya umeme kati ya Rwanda, Burundi na DRC.

“Ni matumaini yangu kuwa mifumo unganishi mingi zaidi ya umeme, itaendelea kujengwa katika ukanda wetu ili itusaidie kupata matokeo chanya zaidi na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi zetu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu, akizungumzia manufaa mengine ambayo Tanzania inayapata kupitia umoja huo wa EAPP, alisema ni pamoja na kusaidiwa na Washirika wa Maendeleo ambao wanafadhili miradi mbalimbali ya umoja huo.

“Kwa mfano sasa tumeanza ujenzi wa Mradi mkubwa wa laini ya msongo wa kilovolti 400 ambayo inatoka Singida hadi Namanga pamoja na ujenzi wa laini ya msongo wa kusafirisha umeme wa kilovolti 400 ambao unatoka Iringa, Mbeya, Tunduma, Songea hadi Sumbawanga. Miradi hii inafadhiliwa na Benki ya Dunia,” alifafanua.

Suala jingine muhimu lililojadiliwa na kupitishwa na Mkutano huo, ni maboresho ya mkataba wa ushirikiano kwa nchi wanachama wa EAPP.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili-kulia), akijadiliana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima (kushoto), Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga (wa pili-kushoto) na Katibu Mtendaji wa EAPP Mhandisi Lebbi Changullah (kulia), kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Mkutano huo ulifanyika Entebbe Uganda, Februari 21, 2019.

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati Tendaji ambayo ni ngazi ya wataalamu kutoka nchi za umoja huo, uliofanyika Februari 20, 2019.

Naibu Waziri alimwakilisha Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani katika mkutano huo ambapo pia aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima pamoja na timu ya wataalamu akiwemo Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka.

Nchi wanachama wa EAPP ni Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi, Ethiopia, Libya, Sudan, Misri, Rwanda, DRC na Djibouti.

 Na Veronica Simba – Entebbe

Read more