Archives for News & Events

Maandalizi ya ujenzi mradi wa umeme wa Rufiji yafikia zaidi ya asilimia 40

Imeelezwa kuwa, kazi mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji ( MW 2115) zinazofanywa na Mkandarasi kampuni ya ubia ya Arab Contractors na Elsewedy Electric  zimefikia zaidi ya asilimia 4O.

Moja ya nyumba inayojengwa na mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme wa Rufiji ambapo katika eneo hilo kunajengwa  kambi ya muda ya Wafanyakazi wa mradi huo.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambao walitembelea eneo la mradi lililopo wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, pamoja na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa nne kutoka mbele) wakiwa  katika eneo ambalo litatumika kutekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufanya  ziara katika eneo la mradi huo.

Kamati hiyo ya Bunge pia ilikagua miundombinu wezeshi iliyotekelezwa na Serikali ikiwemo  Barabara, umeme, nyumba za Wafanyakazi na sehemu maalum ya kushushia mizigo katika Stesheni ya Tazara katika Kituo cha Fuga.

Dkt. Kalemani, alisema kuwa,  Mkandarasi huyo ameanza kazi za maandalizi mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo la mradi mwezi wa Pili mwaka huu. 

Alisema kuwa, miongoni mwa kazi ambazo Mkandarasi  anaendelea kutekeleza kwa sasa ni ujenzi wa kambi ya muda ya Wafanyakazi, uletaji wa vifaa na mitambo itakayotumika wakati wa ujenzi pamoja na kazi za kuchukua sampuli za udongo na maji kwa ajili ya utafiti.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, (katikati), akizungumza na Wataalam wanaosimamia na wanaotekeleza mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115) mara baada ya kufika katika eneo la mradi huo akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kukamilisha kazi hizo za maandalizi Mkandarasi huyo anatakiwa kumaliza kazi ya ujenzi ndani ya miezi 36.

Alieleza kuwa, pamoja na kuridhishwa na hatua hiyo ya maandalizi, bado Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea kumsimania mkandarasi ili amalize kazi ndani ya muda uliopangwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula,  baada ya kukagua miundombinu iliyotekelezwa na Serikali pamoja na kazi za maandalizi zinazofanywa na Mkandarasi, aliipongeza Serikali kwa kuamua kuutekeleza mradi huo na kuusimamia kikamilifu.

Alisema kuwa, Kamati hiyo pia inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini ambapo pia alitoa wito kwa Wizara kutorudi nyuma katika usimamizi wa mradi.

Pia, alitoa wito kwa wafanyabiashara hapa nchini kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mradi kwani Serikali itatumia takribani shilingi Trilioni 6.5 kutekeleza mradi huo hivyo ni muhimu watanzania wafaidike na fedha hizo.

Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali waliambatana na Kamati hiyo akiwemo Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka pamoja na wataalam kutoka kampuni inayotekeleza mradi huo.

Na Teresia Mhagama

14/3/2019

Read more

Kamati ya Bunge ya Bajeti yafanya ziara katika kiwanda cha Transfoma na kupongeza uzalishaji

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, George Simbachawene wametembelea kiwanda cha kuzalisha transfoma cha TANELEC kilichoko jijini Arusha ili kukagua masuala mbalimbali ikiwemo uwezo wake katika uzalishaji wa transfoma lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na vifaa vya umeme vya kutosha.

Katika ziara hiyo waliambatana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Baada ya kukagua shughuli za uzalishaji wa transfoma katika Kiwanda hicho, Wajumbe hao kwa nyakati tofauti waliwapongeza watendaji wa Kiwanda hicho kwa kuzalisha transfoma nyingi ambazo ni 14,000  kwa mwaka huku mahitaji ya transfoma nchini kwa mwaka yakiwa ni 10,000.

Aidha Wajumbe hao walipongeza uamuzi wa Serikali wa mwaka 2017 ambao ulielekeza kuwa miradi yote ya umeme nchini itumie vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini hali inayopelekea miradi hiyo kutekelezwa kwa kasi.

Wajumbe hao pia walimtaka Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo kuongeza uzalishaji na kuwa mbunifu kwa kuangalia pia masoko mengine ya transfoma na si kulenga miradi ya umeme ya ndani ya nchi pekee.

Awali, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alisema kuwa, Serikali ilichukua uamuzi wa kusitisha kuagiza nje vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme.

Alitoa mfano kuwa upatikanaji wa transfoma nje ya nchi unaweza kuchukua hadi miezi 12  hali wakati transfoma zinazozalishwa ndani ya nchi zinachukua muda mfupi kufika katika eneo zinapohitajika.

Aidha Waziri wa Nishati alisema kuwa, uagizaji wa transfoma nje ya nchi ni gharama kubwa kwani transfoma moja kutoka nje ya nchi inauzwa kwa takriban shilingi milioni Tisa wakati zinazozalishwa nchini ni takriban shilingi milioni 6.5.

Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TANELEC, Zahir Saleh alisema kuwa kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1981 kwa sasa kinazalisha transfoma kiasi cha 14,000 kwa mwaka.

Alisema kuwa,  kiwanda kinazalisha transfoma za uwezo wa kvA 50 hadi kVA 5000 na kufanya matengenezo ya transfoma kutoka nchi mbalimbali za Afrika kama Rwanda, Burundi na Kenya.

Aliongeza kuwa, uamuzi wa Serikali kuzuia kuagiza vifaa nje ya nchi umekinufaisha kiwanda hicho kwani kabla ya uamuzi walikuwa wakizalisha transfoma 7000 kwa mwaka lakini sasa wanazalisha transfoma 14,000.

Kuhusu ajira alisema kuwa, awali waliajiri wafanyakazi 30 lakini kwa sasa wafanyakazi walioajiriwa ni 70 na kwa mwaka huu wataajiri wafanyakazi wengine 40.

Vilevile alisema kuwa, kutokana na uamuzi huo wa Serikali, Kiwanda kinafanya kazi kwa faida na wameanza kupeleka gawio serikalini la takribani shilingi milioni 500 kwa mwaka 2018 na wanategemea kuongeza kiasi cha gawio hilo kwa miaka inayokuja.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene (wa kwanza kushoto) wakiongoza Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti katika kukagua kazi zinazofanywa na kiwanda cha transfoma cha TANELEC kilichoko jijini Arusha.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika kiwanda cha kuzalisha transfoma cha TANELEC kilichopo jijini Arusha. Wa Pili kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
[metaslider id=2595 cssclass=””]
[metaslider id=2597 cssclass=””]
Read more

Nchi za Mashariki mwa Afrika zadhamiria kuimarisha Uchumi kwa kuuziana Umeme

Nchi zilizopo Mashariki mwa Afrika, zimedhamiria kwa nia moja kuimarisha uchumi wao kwa kuuziana umeme kupitia mifumo ya kusafirisha nishati hiyo, iliyounganishwa katika ukanda husika.

Hayo yalibainishwa jana, Februari 21 mwaka huu, katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na umeme kutoka nchi za ukanda huo, ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP)

Baadhi ya Mawaziri/Naibu Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza hilo la Mawaziri la EAPP, Mhandisi Irene Muloni (Uganda) na wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati (Tanzania), Subira Mgalu. Walikuwa katika Mkutano wao wa 14 uliofanyika Entebbe, Uganda, Februari 21. 2019.

Akizungumza mara baada ya Mkutano huo uliofanyika mjini Entebbe nchini Uganda, Naibu Waziri wa Nishati (Tanzania), Subira Mgalu, alieleza kuwa, nchi wanachama wa EAPP wamelenga kuhakikisha wananchi wao wanakuwa na umeme wa kutosha, uhakika na wenye gharama nafuu.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri alitoa mfano wa Ethiopia na Misri ambao alisema wanazalisha umeme mwingi, hivyo wanaweza wakauzia nchi nyingine za ukanda husika ikiwemo Tanzania kwa bei nafuu.

Awali, akifungua Mkutano husika, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja huo, Mhandisi Irene Muloni (Uganda), alibainisha kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea katika sekta ya viwanda, pasipo kuwa na umeme mwingi, wa uhakika na wenye gharama nafuu.

Aliongeza kuwa, ni kwa sababu hiyo, nchi wanachama wa EAPP, zimedhamiria kwa dhati kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kuungana na kushirikiana katika kutumia kikamilifu vyanzo vyake vyote vya uzalishaji umeme ambavyo zimejaaliwa.

“Pamoja na nchi zetu kujaaliwa vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme vikiwemo maji, upepo, jua, gesi asilia na vingine vingi, lakini bado tunakabiliwa na umaskini wa nishati hiyo adhimu,” alifafanua.

Akizungumzia mifumo mbalimbali ya umeme inayounganisha nchi hizo, ambayo ikitumika vizuri itaunufaisha ukanda husika; aliitaja kuwa ni pamoja na njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 500 kutoka Ethiopia hadi Kenya, kilovolti 400 kutoka Tanzania hadi Kenya na msongo wa kilovolti 220 kutoka Kenya hadi Uganda.

Nyingine ni njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 220 kutoka Uganda hadi Rwanda pamoja na mifumo unganishi ya umeme kati ya Rwanda, Burundi na DRC.

“Ni matumaini yangu kuwa mifumo unganishi mingi zaidi ya umeme, itaendelea kujengwa katika ukanda wetu ili itusaidie kupata matokeo chanya zaidi na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi zetu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu, akizungumzia manufaa mengine ambayo Tanzania inayapata kupitia umoja huo wa EAPP, alisema ni pamoja na kusaidiwa na Washirika wa Maendeleo ambao wanafadhili miradi mbalimbali ya umoja huo.

“Kwa mfano sasa tumeanza ujenzi wa Mradi mkubwa wa laini ya msongo wa kilovolti 400 ambayo inatoka Singida hadi Namanga pamoja na ujenzi wa laini ya msongo wa kusafirisha umeme wa kilovolti 400 ambao unatoka Iringa, Mbeya, Tunduma, Songea hadi Sumbawanga. Miradi hii inafadhiliwa na Benki ya Dunia,” alifafanua.

Suala jingine muhimu lililojadiliwa na kupitishwa na Mkutano huo, ni maboresho ya mkataba wa ushirikiano kwa nchi wanachama wa EAPP.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili-kulia), akijadiliana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima (kushoto), Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga (wa pili-kushoto) na Katibu Mtendaji wa EAPP Mhandisi Lebbi Changullah (kulia), kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Mkutano huo ulifanyika Entebbe Uganda, Februari 21, 2019.

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati Tendaji ambayo ni ngazi ya wataalamu kutoka nchi za umoja huo, uliofanyika Februari 20, 2019.

Naibu Waziri alimwakilisha Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani katika mkutano huo ambapo pia aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima pamoja na timu ya wataalamu akiwemo Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka.

Nchi wanachama wa EAPP ni Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi, Ethiopia, Libya, Sudan, Misri, Rwanda, DRC na Djibouti.

 Na Veronica Simba – Entebbe

Read more

Wachimbaji wadogo wilayani Mbogwe wafurahia ahadi ya kupata umeme ndani ya Siku Kumi

Wachimbaji wadogo katika machimbo ya Nyakafuru yaliyo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe wameonesha kufurahishwa na ahadi ya Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ya kufikisha umeme katika machimbo hayo ndani ya siku kumi.

Ahadi hiyo aliitoa jana mara baada ya kufanya ziara ya kikazi wilayani Mbogwe mkoani Geita ambapo akiwa katika machimbo hayo, wachimbaji hao walilalamika kuhusu gharama kubwa wanazotumia katika kununua mafuta ya kuendesha mitambo mbalimbali ikiwemo ya kuchenjulia ya madini.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa umeme katika Kijiji cha Kasosobe, Kitongoji cha Mkolani wilayani Mbogwe. Wa Tatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga.

Kwa nyakati tofauti walieleza kuwa, mchimbaji mmoja anaweza kutumia zaidi ya shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea mitambo suala ambalo linawafanya kutopata faida inayostahiki katika shughuli zao.

Kutokana na hilo, Dkt Kalemani alisema kuwa, “kutoka umeme unapoishia hadi hapa ni kilometa 1.5 tu, na hapa kuna wachimbaji wadogo zaidi ya Elfu Nne na mashine za kuchenjulia madini zaidi ya 200, hivyo nakuagiza Meneja wa TANESCO kuleta umeme hapa ndani ya siku Kumi na pia muwafungie transfoma itakayohudumia eneo hili,”.

Waziri wa Nishati pia alitembelea mitambo ya kisasa ya kuchenjulia madini tani 10 kwa saa ambayo ipo katika Kijiji cha Shenda wilayani Mbogwe ambayo nayo uendeshaji wake unatumia mafuta  badala ya umeme.

Baada ya kukagua mitambo hiyo, Dkt. Kalemani alimwagiza Meneja wa TANESCO wilayani Mbogwe kuhakikisha kuwa, ifikapo tarehe 25 mwezi huu awe ameshafikisha  umeme katika eneo hilo.

Akiwa wilayani Mbogwe, Dkt Kalemani pia alikagua kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Bulugala na kukuta nguzo zimesimikwa huku nyaya zikiwa bado hazijavutwa hivyo alimuagiza mkandarasi wa umeme (kampuni ya Whitecity Guangdong JV) kuwasha umeme katika Kijiji hicho kabla ya tarehe 5 mwezi ujao.

Katika ziara yake wilayani Mbogwe pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Kasosobe, Kitongoji cha Mkolani ambapo awali alielezwa kuwa umeme huo bado haujafika katika maeneo muhimu ya kijamii kama Shule na Nyumba za ibada pamoja na vitongoji vingine vya Kijiji hicho.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto) akikagua mitambo ya kisasa ya kuchenjulia madini tani 10 kwa saa ambayo ipo katika Kijiji cha Shenda wilayani Mbogwe na kuahidi kupeleka umeme hivi karibuni.

Dkt Kalemani alimuagiza mkandarasi wa umeme kufikisha umeme katika vitongoji vyote vya Kijiji hicho ikiwemo ikiwemo Shule, na Nyumba za Ibada ndani ya siku 14.

Vilevile Dkt.Kalemani alifanya ziara katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo aliwasha rasmi umeme katika Kijiji cha Ryobaika, kilicho katika Kata ya Uyovu na kutoa wasaa kwa wananchi kulipia huduma ya umeme mapema na wataalam wa TANESCO pamoja na mkandarasi kutokataa malipo ya wananchi kwa kisingizio chochote kile.

Read more

Kazi ya uwashaji umeme vijijini inazidi kushika kasi- Dkt Kalemani

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ameeleza kuwa kasi ya usambazaji umeme vijijini inaendelea kuongezeka ili kuweza kufikia lengo la Serikali la kusambazia umeme vijiji vyote ifikapo mwaka 2021.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, (katikati) akiwasha umeme katika Kijiji cha Lwezera wilayani Geita ambacho kimepata umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III).Kushoto kwake ni Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo jana akiwa katika ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme katika Wilaya ya Geita mkoani Geita ambapo aliambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga, Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyau, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Amos Maganga.

“Kasi ya usambazaji umeme vijijini kupitia mradi wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza inaongezeka, kwa mfano leo, tunawasha umeme katika Vijiji 61 nchi nzima, na katika ziara yangu ya Siku Tatu mkoani Geita nitawasha umeme katika Vijiji 12,” alisema Dkt Kalemani.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake, Dkt Kalemani alikagua miradi ya umeme wilayani Geita na kuwasha umeme katika Kijiji cha Lwezera, Luhuha na mtaa wa Ibanda ulio katika Kata ya Kanyala. Pia amewasha umeme katika Gereza la Butundwa ambalo linajishughulisha Kilimo na Ufugaji.

Awali, Dkt Kalemani alifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel ambaye alimueleza Waziri kuhusu mahitaji ya umeme katika Mkoa huo na kueleza kuwa Mkoa  umeshatenga eneo kwa ajili shughuli za Mnada wa madini na kuna wawekezaji walioonesha nia ya kujenga mitambo ya kuchenjulia madini mkoani humo hivyo ili kufanikisha suala hilo wanahitaji umeme wa uhakika.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ( wa Tano kushoto) akikagua miundombinu ya umeme katika Kata ya Kanyala wilayani Geita ambayo imepata umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza (REA III).Wa Tatu kulia ni Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyau na Wa Tano kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga.

Kuhusu suala hilo, Dkt Kalemani, alieleza kuwa, Wizara inatambua lengo  la Serikali la kuwa na viwanda vya kutosha ili kuingia katika uchumi wa viwanda, hivyo Mkoa huo unachotakiwa kufanya ni kuwasilisha mahitaji yake ya nishati ili yaweze kufanyiwa kazi.

Kwa upande wao, Mbunge wa Geita Mjini na Geita Vijijini, kwa nyakati tofauti walieleza kuhusu masuala mbalimbali yanayopaswa kufanyiwa kazi ikiwemo TANESCO kusogeza huduma karibu na wananchi na kasi ya mkandarasi kuendelea kuongezeka, masuala ambayo Waziri wa Nishati aliyaafiki na kutoa maelekezo kwa TANESCO na mkandarasi kampuni ya Whitecity Guangdong JV.

Read more

Waziri wa Nishati, azindua Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kutoa maelekezo

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, leo amezindua Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), na kutoa maelekezo mbalimbali kwa Bodi hiyo yatakayopelekea kazi ya usambazaji umeme vijijini kufanyika kwa kasi na ufanisi.

Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo imezinduliwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.

Kikao cha Waziri na Bodi hiyo kimefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga na watendaji wengine kutoka Wizara na REA.

Akizungumza na Bodi hiyo, Dkt Kalemani alieleza sababu mbalimbali za  kuvunjwa kwa Bodi iliyopita tarehe 12 Novemba, 2018 kuwa ni kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kushindwa kusimamia vizuri Wakala wa Nishati Vijijini.

“Leo tunawakabidhi majukumu yenu lakini suala la msingi ni kuwatumikia wananchi kwani tunawajibika kwao hivyo yaliyotokea kwenye Bodi iliyopita, yasitokee kwenye Bodi yenu”. Alisema Dkt Kalemani

Alitaja majukumu ya Bodi hiyo kuwa ni kusimamia Wakala wa Nishati Vijijini ili utekeleze majukumu yake kwa ufanisi na weledi na kusimamia shughuli za Wakala  ili zifanyike kwa malengo na Dira ya Serikali ya kusambaza umeme katika Vijiji vyote nchini.

Aliongeza kuwa, majukumu mengine ya Bodi hiyo ni kusimamia Fedha za Mfuko wa Nishati Vijijini ili tija yake ionekane na kuitaka Bodi hiyo kutokuwa chanzo cha migogoro inayoweza kuchelewesha au kukwamisha kazi za Wakala.

Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Raphael Nombo (katikati) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati akizungumza na Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini.

Aidha, ameiagiza Bodi hiyo kuharakisha utekelezaji wa kusambaza umeme katika Vijiji, vitongoji na miradi mbalimbali ya kijamii na kuwasimamia ipasavyo wakandarasi wa umeme vijijini ili kazi zao ziende kwa haraka kwani wengi wao hawafanyi kazi zao inavyotakiwa.

Dkt. Kalemani amezindua Bodi hiyo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kumteua Bw. Michael Nyagoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo tarehe 14 Februari 2019.

Wajumbe wa Bodi hiyo ni Oswald Urassa, Mhandisi Styden Rwebangila, Francis Songela, Louis Accaro, Dailin Leonard, Henry Mwimbe na Dkt. Andrew Komba.

Read more

Yaliyojiri wakati wa hafla ya kukabidhi eneo la ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Rufiji (Megawati 2115) kwa Mkandarasi (Jv Arab Contractors na Elsewedy Electric)

Aliyoyasema Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani

Nampongeza Rais, Dkt John Pombe Magufuli kwa kuchukua hatua madhubuti na za ujasiri katika kutekeleza mradi huu ambao ni wa muda mrefu lakini  kwa sasa Serikali imeamua kuutekeleza.

Mradi ulianza kufanyiwa usanifu miaka ya 1970 lakini gharama za utekelezaji zilikuwa kubwa na kwa kipindi hicho umeme uliokuwa ukihitajika ni megawati 100 tu,,, ila kwa leo mahitaji ya umeme ni makubwa, tunahitaji kutekeleza mradi huu sasa na si baadaye.

Mkandarasi wa mradi huu ana majukumu makubwa manne ambayo ni kujenga bwawa kuu lenye uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo bilioni 35, kujenga kituo cha kufua umeme kitakachokuwa na mashine Tisa za kuzalisha umeme wa megawati 235 kila moja hivyo kwa ujumla zitazalisha megawati 2115.

Kazi nyingine za mkandarasi ni kujenga kituo cha kupoza na kukuza umeme cha kV 400 na kujenga njia za kusafirisha umeme utakaoingia katika gridi ya Taifa kwa kutumia njia kuu mbili ambazo ni kutoka eneo la mradi kwenda Chalinze ili kuunganishwa na njia ya kutoka Chalinze kwenda Dodoma na Dar es Salaam.

Njia nyingine ya Umeme ya kV 400 itajengwa kutoka Rufiji kuelekea Kibiti ambapo takribani Vijiji 21 vitafaidika na umeme huo.

Mradi wa umeme wa Rufiji una manufaa mbalimbali ikiwemo, kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya Taifa, kuvutia shughuli za utalii ambazo zitaingiza kipato kwa nchi, maji ya bwawa yataweza kutumika kwa shughuli za umwagiliaji na hivyo kuchochea kilimo cha kisasa, pia Vijiji 37 na vitongoji 142 vinavyopitiwa na mradi vitasambaziwa umeme.

Utekelezaji wa mradi utapelekea kupungua kwa gharama za nishati kwani nchi ambazo zinatumia umeme wa maji kwa wingi gharama zake za umeme zipo chini kuliko zinazotumia vyanzo vingine vya nishati, mfano sisi leo gharama ya umeme ni Dola senti 11 kwa uniti huku Ethiopia ambako wanatumia sana umeme wa maji gharama ni Dola senti 2.4.

Wito wangu kwa wakandarasi ni kutekeleza mradi huu, kwa weledi na ufanisi mkubwa ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa na wasiondoke eneo la kazi kwani miundombinu yote wezeshi kama nyumba, maji, umeme na Reli imeshakamilika.

Nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati pamoja na wataalam wote waliofanya kazi za maandalizi ya mradi pamoja majadiliano mbalimbali ambayo yamepelekea mradi huu kuanza kutekelezeka.

Aliyoyasema Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu

Ninawaahidi watanzania kuwa, mimi na watendaji wenzangu ndani ya Wizara ya Nishati tutasimamia kikamilifu mradi huu ili uweze kutekelezaka kwa wakati.

Aliyoyasema Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Dkt.Ashatu Kijaji

Wizara ya Fedha imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa mradi huu wa kihistoria  ndani ya Taifa letu unatekelezeka.

 Dira ya Taifa inaelekeza kuwa mpaka mwaka 2025  tuwe na Tanzania ya kipato cha kati na hili halitawezekana bila kuwa na Tanzania ya Viwanda ambavyo navyo uwepo wake unategemea uwepo wa umeme wa bei nafuu, hivyo mradi huu ni muhimu katika kuhakikisha kuwa Dira hii inatekelezeka.

Aliyoyasema Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu

Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa majukumu mawili makubwa ambayo ni kutoa ulinzi kwa wakandarasi na watu wote wanaofanya kazi katika eneo hili na kusafisha beseni litakalotumika kuhifadhi maji yatakayotumika katika mradi huu.

Kwa ujumla tunaendelea kutekeleza vizuri majukumu haya tuliyokabidhiwa na tunaahidi kuwa kwa yote yatakayojitokeza huko mbele tutaendelea kuyatekeleza bila wasiwasi.

Aliyoyasema Makamu wa Rais, Elsewedy Electric, Eng. Wael Hamdy.

Kwa niaba ya Serikali ya Misri, napenda niwahakikishie kuwa tutatekeleza mradi huu kwa ufanisi mkubwa bila kujali changamoto zozote.

Huu si mradi mwepesi kutekeleza lakini kwa sisi kama wahandisi hii ni kazi yetu hivyo tutaitekeleza ipasavyo na huu si mradi wa kwanza kwetu kuutekeleza.

Tunawaahidi kuwa hatutaawangusha, tutakabidhi mradi kama kama yalivyo matarajio yenu na ndani ya wakati uliopangwa.

Na Teresia Mhagama

Read more

PBPA yatakiwa kuhakikisha kuwa Bandari zote zinatumika kupokea\kushusha mafuta.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameitaka Bodi ya Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuhakikisha kuwa bandari zote nchini zinatumika katika shughuli za kupokea na kushusha mafuta ili kuongeza wigo wa upatikanaji  mafuta katika sehemu mbalimbali nchini.

Aliyasema  hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao chake na Wajumbe wa Bodi ya Wakala huo  ambapo kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya na watendaji wengine wa Wizara.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo baada ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, kumueleza kuwa, mpaka sasa mafuta yanapokelewa katika Bandari Tatu tu ambazo ni Dar es Salaam, Mtwara na Tanga.

“Tunataka kila Bandari ifanye kazi ya kupitisha mafuta mfano ni  Bandari ya Bukoba ambapo mafuta yakipokelewa pale yanaweza pia kusafirishwa kwenda nchini jirani badala ya kusafirishwa kwa njia ya barabara kutoka jijini Dar es Salaam,” alisema Dkt Kalemani.

Aidha, Dkt Kalemani aliagiza kuwa, Bandari zote zinazotumika sasa zipokee pia mafuta ya taa kwani wananchi bado wanatumia mafuta hayo kwa shughuli mbalimbali kwa kuwa usambazaji wa nishati ya umeme bado haujafikia asilimia 100.

Pia, Dkt Kalemani aliiagiza Bodi ya PBPA kuhakikisha kuwa ushiriki wa wazawa katika shughuli za uingizaji mafuta nchini  unaongezeka kwa kuwajengea uwezo wa aina mbalimbali ikiwemo kuwapa elimu kuhusu shughuli hizo.

Kwa ujumla, Dkt Kalemani aliitaka Bodi hiyo kuwa na mikakati mbalimbali itakayopelekea kampuni nyingi zaidi kushiriki katika kazi ya uingizaji wa mafuta nchini tofauti na ilivyo sasa ambapo kati ya kampuni 25 zilizosajiliwa, kampuni zisizozidi Saba ndizo zinashiriki katika uletaji wa mafuta nchini.

Vilevile aliiagiza Bodi hiyo kuhakikisha kuwa, inasimamia masuala mbalimbali ikiwemo  suala la nchi kupata mafuta kwa wakati huku yakiwa salama, kutokuwepo migogoro katika shughuli za uingizaji mafuta nchini, kutokuwepo kwa upotevu wa mafuta, mafuta kushushwa ndani ya muda mfupi  mara yanapowasili na kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na  mafuta ya ziada katika muda wote.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alitoa angalizo kwa Bodi hiyo kuhakikisha kuwa, kampuni zinazopewa kazi za uingizaji mafuta nchini zinakuwa na uzalendo na hivyo kuepusha hujuma zozote zinazoweza kutokea na kusababisha nchi kuwa na upungufu wa nishati hiyo au kupata mafuta yasiyo salama.

Na Teresia Mhagama

Read more

Waziri Kalemani ahimiza TPDC kujiendesha kibiashara

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kuipa changamoto kuhakikisha shirika hilo linajiendesha kibiashara.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Profesa Sufian Bukurura (kushoto), akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili-kulia) na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo (hawapo pichani), kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Shirika hilo jijini Dar es Salaam, jana Februari 10, 2019. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) na Katibu Mkuu Dkt. Hamisi Mwinyimvua (wa pili-kushoto).

Alitoa changamoto hiyo jana Februari 10, 2019 jijini Dar es Salaam, ambapo aliwaelekeza wajumbe wa Bodi husika kuandaa andiko mahsusi likieleza namna shirika hilo linavyoweza kujiendesha kibiashara na kuleta tija zaidi kwa Taifa na wananchi pasipo kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Kikao hicho pia kiliwashirikisha Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Dkt. Hamisi Mwinyimvua na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Raphael Nombo; ambapo mambo mbalimbali yahusuyo utendaji wa shirika yalijadiliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba (kushoto), akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo (hawapo pichani), kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Shirika hilo jijini Dar es Salaam, jana Februari 10, 2019.

Na Veronica Simba – Dar es Salaam.

Read more

Wafanyabiashara wa Mafuta kujiunga katika umoja wa kisekta ni hiari siyo lazima – Kalemani

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kamwe Serikali haiwezi kumlazimisha mdau yeyote wa sekta ya mafuta nchini kujiunga na Chama, Jumuiya au Umoja wowote wa kisekta kwani hilo ni suala la hiyari kwa kila mmoja.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza na wadau wa sekta ya mafuta nchini (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika Februari 10, 2019 jijini Dar es Salaam. Wengine pichani, kutoka kulia ni Mwenyekiti TAOMAC, Sophonie Babo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya na Kaimu Mkurugenzi wa PBPA, Erasto Simon.

Badala yake, Waziri Kalemani, ameushauri uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mafuta Tanzania (Tanzania Association Of Oil Marketing Companie – TAOMAC) na Jumuiya nyingine za aina hiyo, kuziimarisha zaidi kwa kuweka mazingira ambayo yatawashawishi wadau wengi kujiunga nazo.

Aliyasema hayo jana, Februari 10, 2019 jijini Dar es Salaam katika mkutano baina yake na wadau wa sekta ya mafuta nchini, wakiwemo waagizaji, wauzaji na wafanyabiashara wa mafuta.

Waziri Kalemani alikuwa akijibu ombi maalumu lililowasilishwa kwake na Mwenyekiti wa TAOMAC, Sophonie Babo na kuungwa mkono na wanachama kadhaa wa Umoja huo; kuwa Serikali iweke sheria na kanuni zitakazomlazimu mtu yeyote atakayeomba leseni ya kufanya kazi katika sekta husika kuwa kwanza mwanachama wa TAOMAC.

Akifafanua, Waziri Kalemani alisema kuwa, Serikali itaendelea na utaratibu wake wa kawaida katika kutoa leseni za biashara ya mafuta kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa ambayo hayahusishi mwombaji kuwa mwananchama wa Umoja au Jumiya yoyote ya kisekta.

“Chama ni hiari ya mtu, huwezi kumlazimisha. Kama mmeweka utaratibu mzuri, watu watajiunga tu. Hakuna sababu ya kuweka kanuni au sheria. Ukisema kuwalazimisha watu kujiunga na Chama fulani, utakuwa unaingilia uhuru wao kinyume na utaratibu wa sheria.”

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alisema malengo ya serikali ni kuhakikisha inaendelea kuisimamia sekta ya mafuta vizuri ili iweze kuwa na tija kwa pande zote mbili yaani Serikali kwa niaba ya wananchi na wafanyabishara kwa upande mwingine.

Alisema, lengo la serikali kuhakikisha sekta husika inaleta manufaa kwa wananchi wake ni la msingi na litaendelea kusimamiwa lakini pia serikali itahakikisha wafanyabiashara nao kwa upande wao wanapata faida, ilimradi walipe kodi zote stahiki.

Aidha, alisema, mifumo, será na kanuni zote zilizowekwa na serikali katika kusimamia sekta ya mafuta hazina lengo la kuathiri biashara ya mtu yeoyote bali ni kwa lengo la kusimamia maslahi ya wananchi na upande mwingine wafanyabiashara husika.

Wadau wa sekta ya mafuta, wataalamu kutoka wizarani na sekta mbalimbali za serikali, wakifuatilia kikao baina yao na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), kilichofanyika Februari 10, 2019 jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Manunuzi ya Petroli kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency  – PBPA), Erasto Simon pamoja na wadau mbalimbali kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali zinazojihusisha na masuala ya mafuta.

Waziri Kalemani alielekeza kuwa kikao kama hicho kifanyike mara moja kila mwaka ili kutoa fursa kwa serikali na wadau wa sekta husika kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa sekta hiyo.

Na Veronica Simba – Dar es Salaam.

Read more