• Afanya ziara wilayani Handeni, Lushoto na kuwasha umeme katika Vijiji Vitano

Katika kuhakikisha kuwa  adhma ya Serikali ya kusambaza umeme katika vijiji vyote  nchini ifikapo mwaka 2021 inatekelezwa, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amefanya ziara  katika Wilaya ya Handeni na Lushoto mkoani Tanga ili kukagua kazi za usambazaji umeme vijijini na kuwasha umeme katika baadhi ya vijiji.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto) akimkabidhi kifaa cha UMETA, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Waziri wa Nishati alitoa vifaa vya Umeta 30 kwa Mbunge huyo ili kuwawezesha wananchi kuunganishwa na huduma ya umeme bila kutandaza nyaya ndani ya nyumba.

Akiwa wilayani Handeni, Waziri wa Nishati aliwasha umeme katika Kijiji cha Madebe, Nyasa  na Kwamnele na wilayani Lushoto aliwasha umeme katika Kijiji cha Mabugai na Nkelei.

Aidha alifanya ziara katika kata na Vijiji mbalimbali ambavyo bado havijasambaziwa umeme ikiwemo Kijiji cha Mahezangulu kilicho katika Jimbo la Bumbuli, wilayani Lushoto ambapo aliagiza kuwa, kiwashiwe umeme ifikapo tarehe 12 mwezi huu.

Katika ziara yake wilayani Handeni, Viongozi wa Wilaya hiyo walimweleza kuwa, kuna vijiji 10 ambavyo vimepitiwa na miundombinu ya umeme lakini havina nishati hiyo, hivyo kuleta malalamiko miongoni mwa wananchi kuwa walitoa maeneo yao kupisha miundombinu hiyo lakini hawapati umeme.

Kuhusu suala hilo, Dkt Kalemani aliagiza kuwa, kuanzia Jumatatu ya tarehe 8 Oktoba, 2018 wataalam wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) waanze utaratibu wa kupeleka umeme katika Vijiji hivyo kwani kinachohitajika ni kusambaza tu umeme kwa wananchi hao kwa kuwa miundombinu ipo.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizidua rasmi huduma ya upatikanaji wa umeme katika Kijiji cha Mabugai wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga.

Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani alitoa onyo kuwa, Meneja yeyote wa TANESCO atakayeonekana anatetea wakandarasi wanaochelewesha kazi kwa kisingizio cha kutokuwa na vifaa atakuwa amejihesabia kuwa kashindwa kazi.

“ Hawa wakandarasi tayari wameshalipwa fedha za kuwawezesha kuanza kazi ya usambazaji umeme vijijini, hivyo wanatakiwa kuwa na vifaa vyote vinavyohitajika katika kazi hii,” alisema Dkt Kalemani.

Vilevile aliwataka watumishi kuwa na lugha ya staha pale wanapohudumia wananchi na kueleza kuwa atakayeshindwa kufanya hivyo ataondolewa katika nafasi yake.

Ziara ya Dkt Kalemani wilayani Handeni na Lushoto ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya hizo, Wabunge, Madiwani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.

Na Teresia Mhagama