• Atoa wiki moja kwa mkandarasi kukamilisha usambazaji umeme

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  leo  tarehe 13 Februari, 2018 amefanya ziara katika wilaya ya Chato mkoani Geita lengo likiwa ni kukagua miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na  Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa mkandarasi, wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kalembela kilichopo wilayani Chato mkoani Geita.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika vijiji vya Iparamasa na Kalembela vilivyopo wilayani Chato mkoani Geita, Dkt. Kalemani ameitaka kampuni iliyopewa kazi ya kujenga miundombinu ya umeme katika vijiji husika, ya White City JV Guandong kukamilisha kazi iliyopewa ndani ya wiki moja  katika kijiji cha Iparamasa na  siku tatu katika kijiji cha Ilembela ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika.

“ Wananchi hawa wamechoka na adha ya kukosa  huduma ya umeme kwa muda mrefu, ninatoa wiki moja kwa mkandarasi kuhakikisa kijiji cha  Iparamasa kinapata umeme wa uhakika na siku tatu kwa kijiji cha Kalembela wanapatiwa huduma ya umeme kwa kuwa tayari nguzo zimefika katika vijiji husika,” alisema Dkt. Kalemani

Waziri Kalemani aliendelea kusema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imepanga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia ya 75 ya watanzania wanapata huduma ya umeme ambao ni wa uhakika na kuchangia nchi kutoka kwenye orodha ya nchi masikini na kuingia kwenye orodha ya nchi za kipato cha kati

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kalembela kilichopo wilayani Chato mkoani Geita, wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)

Alisisitiza kuwa, kwa kutambua mchango wa nishati kwa ukuaji wa uchumi wa viwanda, Wizara ya Nishati imepanga mikakati ya kuhakikisha miradi ya REA inatekelezwa kwa wakati kwa kutenga fedha za kutosha, na usimamizi  makini ili wananchi wote wanufaike na huduma ya umeme.

Aidha, katika hatua nyingine Dkt. Kalemani aliwataka wananchi wa vijiji husika kujiandaa na huduma ya umeme kwa kutandaza nyaya kwenye nyumba zao (wiring) au kuweka Kifaa Maalum cha Umeme Tayari (UMETA) ili waunganishwe na huduma ya umeme mapema.

Pia Waziri Kalemani aliwataka wananchi kuchangamkia fursa zitakazojitokeza mara baada ya upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika kama vile uanzishwaji wa viwanda vya kusindika nafaka, mashine za kuchomea vyuma na kuondokana na umaskini.

Na Greyson Mwase, Chato