• Dkt. kalemani aiagiza TANESCO kuunda kikosi maalum kukagua miundombinu ya umeme

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameliagiza Shirika la umeme nchini (TANESCO) kuunda kikosi maalum kitakachokagua miundombinu yote ya umeme kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kuondoa iliyochakaa, kwa lengo la kumaliza tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria kuwasha umeme katika kijiji cha Kajionee Mwenyewe wilayani Urambo, mkoani Tabora ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa REA III katika Wilaya hiyo.

Alisema kuwa, changamoto ya miundombinu chakavu ndiyo sababu kuu ya umeme kukatika mara kwa mara, licha ya kuwepo kwa mitambo inayozalisha umeme mwingi, wakutosha na wa ziada kila siku, hivi sasa.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA III mkoani humo pamoja na kuwasha umeme katika Kijiji cha Kajionee Mwenyewe kilichopo katika Wilaya ya Urambo mkoani humo, tarehe17 Aprili, 2018.

Kijiji cha Kajionee mwenyewe ni cha kwanza kuwashiwa huduma ya umeme ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa REA III katika Mkoa wa Tabora.

Akizungumzia suala la kukatika kwa umeme katika maeneo mengi nchini, Dkt.Kalemani aliwaagiza TANESCO kufanya ukarabati na kubadilisha miundombinu ya nguzo pamoja na nyaya zilizochakaa ambazo husababisha hitilafu za mara kwa mara tatizo la kukatika umeme unaosababisha kero kwa wananchi.

Sambamba na hilo, aliaagiza kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu, miundombinu ya nguzo zilizochakaa ama kuanguka zibadilishwe kwa kutumia nguzo za zege ambazo zitadumu kwa muda mrefu zaidi badala ya kusubiri mwezi Septemba kama ilivyokuwa imeelekezwa hapo awali.

Aidha, katika hatua nyingine aliwaagiza TANESCO kuweka vidhibiti Radi katika nguzo za umeme na kubadilisha vile vilivyochakaa ili kuepusha athari za nguzo hizo kuunguzwa au kupigwa na Radi na kusababisha umeme kukatika hasa katika kipindi cha mvua.

Akizungumza uimarishaji wa huduma za umeme kwa wananchi, Dkt. Kalemani aliwaeleza wananchi wa Mkoa wa Tabora na  maeneo yanayowazunguka mkoa huo kuwa, mwezi Julai mwaka huu serikali inatarajia kujenga vituo viwili vya kupooza na kusambaza umeme ili kuondoa tatizo la kukatika umeme linalosababishwa na urefu wa njia ya kusafirisha umeme katika Mkoa huo.

Tayari serikali imetenga fedha za kujenga vituo hivyo, ambapo kituo cha kwanza kitajengwa katika kijiji cha Uhuru Kata Vulimilia kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Urambo na Kaliua.

Wananchi wawili wametoa maeneo yao bure pasipo kudai chochote yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 9 na kumkabidhi Waziri wa Nishati kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu na kukamilika ndani ya miezi mitatu tangu ujenzi huo kuanza.

Kituo kingine kitajengwa katikati ya Wilaya ya Kaliua na Uvinza mkoani Kigoma.

Maadili Ahmed Said (kushoto) aliyetoa hekta 3 na Kasim Haruna (kulia) aliyetoa hekta 6 wakimuonyesha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani maeneo yao walioyatoa bure kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupooza na kusambaza umeme kitakachojengwa katika kijiji cha Uhuru kata ya Vulimialia kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Urambo na Kaliuwa.

Wananchi waliotoa maeneo hao walisema kuwa wanatambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kasi ya kuwaletea wananchi maendeleo na kusisitiza uzalendo kwanza, hivyo waliona kuwa wakati huu ni muafaka kwa wao kuunga mkono shughuli za maendeleo zinazofanywa na serikali chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake, Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta na Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya waliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa juhudi zake za kuunganisha vijiji vyote na huduma ya umeme kwa kuwatoza wananchi gharama nafuu.

Pia, wamewataka wananchi hao kulinda miundombinu ya umeme kwa kuwa serikali imetumia gharama kubwa kuijenga, ili iweze kuwasaidia, kuwaletea maendeleo na kuhakikisha kuwa inadumu kwa muda mrefu.

Na Zuena Msuya, Tabora