Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, ametembelea  eneo la kina kifupi cha Bahari  katika fukwe za Chongoleani jijini Tanga ambapo kisima cha 20 kinachorongwa  ikiwa ni moja ya kazi za awali zilizopangwa kufanyika  kabla ya kuanza kwa ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi litakalojengwa kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Baada ya kutembelea eneo hilo, tarehe 27 Machi, 2018, Dkt Kalemani alisema kuwa  visima 20 vimechorongwa  baharini  ili kupata sampuli za udongo  ambazo zinapelekwa maabara  kwa ajili ya uchanganuzi  wa takwimu za kihandisi zitakazowawezesha wataalam kufanya mapitio ya usanifu wa miundombinu  ya bomba hilo.

Rig inayochoronga kisima katika kina kifupi cha bahari mkoani Tanga ili kupata sampuli za udongo ambazo zinapelekwa maabara kwa ajili ya uchanganuzi wa takwimu za kihandisi zitakazowawezesha wataalam kufanya mapitio ya usanifu wa miundombinu ya bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga-Tanzania.

Alisema kuwa, visima 13 vimechorongwa katika kina kirefu cha Bahari na visima Sita vimechorongwa  katika kina kifupi hivyo kinachofanyika sasa ni kuchoronga  kisima cha mwisho katika kina kifupi cha Bahari ambapo kazi hiyo itakamilika tarehe 29 Machi, 2018.

Sambamba na hilo alieleza kuwa, kazi ya kuandaa eneo kutakapofungwa matenki matano ya kuhifadhia mafuta imekamilika na kinachofuata ni ujenzi wa miundombinu ambapo matenki hayo yatafungwa.  Kila tenki litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita Laki Tano za mafuta.

Alisema kuwa, kwa sasa Timu ya Majadiliano ya Serikali inafanya majadiliano na mkandarasi mjenzi wa mradi huo ili kuangalia manufaa ya mradi kwa kila upande kabla ya ujenzi kuanza ambapo kazi hiyo itakamilika katikati ya mwezi Aprili mwaka huu.

Aliongeza kuwa, kazi nyingine inayokamilishwa sasa ni upembuzi yakinifu wa masuala ya fidia ambapo vipo vikosi vitatu vinafanya kazi hiyo ambavyo vipo Tanga, Isaka-Shinyanga, na Bukoba mkoani Kagera ambapo kazi hiyo itakamilika mwishoni mwa mwezi huu.

“Sisi kama Serikali kazi yetu ni kusukuma kwa kasi kubwa, kusimamia kwa bidii kubwa na weledi ili kuhakikisha kuwa kazi inakamilika kwa wakati, tunawaahidi Watanzania kuwa tutasimamia kikamilifu mradi huu ambao una faida kubwa kwa nchi yetu,” alisema Dkt Kalemani.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kushoto) akiangalia ramani inayoonyesha maeneo mbalimbali ambayo shughuli za awali za ujenzi wa bomba la mafuta ghafi zinafanyika katika kina cha Bahari mkoani Tanga.

Alieleza kuwa, kwa ujumla taratibu mbalimbali za kuanza kutekeleza mradi  huo zinaendelea vizuri hivyo matarajio ni kuanza shughuli za ujenzi mwezi Mei mwaka huu.

Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Hoima – Tanga wenye urefu wa kilometa 1,443 zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania, utagharimu dola za Marekani bilioni 3.5.

Na Teresia Mhagama,Tanga