• Awasha umeme Magumbani na Mbuluni

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika wilaya ya Mkinga mkoani Tanga ambapo pia amezindua upatikanaji wa huduma ya umeme katika vitongoji viwili wilayani humo.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akizindua upatikanaji wa huduma ya umeme katika Kitongoji cha Mbuluni na Magumbani wilayani Mkinga. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mkinga, Yona Mark na wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbuluni Selemani Omar.

Ziara hiyo ameifanya tarehe 26 Machi, 2018 ambapo aliambatana na Mkuu wa wilaya ya Mkinga, Yona Mark, watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wizara ya Nishati.

Katika ziara hiyo, Dkt Kalemani alizindua huduma ya upatikanaji wa umeme katika Kitongoji cha Magumbani na Mbuluni, hivyo kuwawezesha wananchi wa vitongoji hivyo kuanza kupata huduma ya umeme kwa mara ya kwanza.

Kabla ya kuzindua umeme katika vitongoji hivyo, Dkt Kalemani aliwaagiza wakandarasi wa umeme vijijini kuhakikisha kuwa hawaruki vitongoji wakati wa usambazaji wa umeme na kwamba kila mwananchi anayelipia huduma ya umeme, apewe huduma hiyo bila kurukwa kwa kisingizio cha ubora wa nyumba.

Pamoja na kuwapongeza watendaji wa TANESCO na wakandarasi wanaosambaza umeme wilayani humo kwa kazi ya usambazaji umeme vijijini, aliwaagiza kuendelea kukamilisha kazi walizopangiwa ndani ya muda uliopangwa ili ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote nchini view vimesambaziwa umeme.

Kuhusu upatikanaji wa umeme mkoani Tanga, alieleza kuwa, mkoa huo una mashine zenye uwezo wa kufua umeme wa kiasi cha megawati 92,  huku mahitaji yakiwa ni megawati 59, hivyo hali ya umeme si mbaya katika mkoa huo.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia) akizungumza na mkazi wa Kijiji cha Magumbani, Kitongoji cha Mbuluni wilayani Mkinga ambaye nyumba yake (inayoonekana) imeunganishwa na umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu.

Aidha, kuhusu usambazaji wa umeme vijijini alisema kuwa, mkoa wa Tanga una vijiji 920 ambapo vijiji 446 tayari vimeshasambaziwa umeme na vilivyobaki vinaendelea kusambaziwa umeme kupitia REA III.

Awali, Mkuu wa wilaya ya Mkinga, Yona Mark pamoja na kupongeza juhudi za Serikali katika usambazaji umeme kupitia mradi wa REA III ambao Dkt. Kalemani aliuzindua mwaka 2017, alitoa ombi la kuwepo kwa Ofisi za Tanesco katika wilaya hiyo ili kuwasogezea huduma wananchi.

Aidha, aliomba umeme ufike katika miundombinu ya maji iliyopo wilayani humo ili kuweza kusukuma maji kwenda kwa wananchi.

Kabla ya kufanya ziara hiyo, Dkt Kalemani alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela na viongozi wengine mkoani hapo ambapo walizungumzia suala la upatikanaji wa umeme pamoja ujenzi wa mradi wa Bomba la Mafuta unaotarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka huu.