• Wajadili faida na umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji yanayoingia katika Bonde la Mto Rufiji

Waziri wa Nishati,  Dkt.Medard Kalemani amewataka Viongozi wa Serikali za Mitaa,Vijiji na wadau mbalimbali kuwaelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa kutunza na kulinda vyanzo vya maji nchini ili yatumike kuzalisha umeme mwingi na pia katika matumizi bora ya kilimo cha umwagiliaji.

Dkt.Kalemani alisema hayo tarehe 5 Machi, 2018 wakati wa Warsha ya Wadau wa Mradi wa kuzalisha umeme Rufiji wa megawati 2100 iliyofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mkoani Iringa.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto), Naibu Waziri wa Nishati (katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (kulia) wakiwa nje ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Warsha hiyo ilishirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji ili kupata elimu kuhusu faida na umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji yanayoingia katika Bonde la Mto Rufiji patakapojengwa Mradi wa kuzalisha Umeme wa megawati 2,100 kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto huo.

Katika warsha hiyo, Dkt.Kalemani alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa mradi huo ni vyema Wananchi wakaelimishwa umuhimu wa kutunza maji kwa ajili ya Nishati ya umeme pamoja na matumizi mengine ikiwemo Kilimo ili shughuli hizo zitekelezwe kwa pamoja pasipo kutokea athari yoyote.

Aliweka wazi kuwa, mbali na Mradi huo wa kuzalisha umeme, eneo hilo litakuwa kivutio kikubwa cha Utalii kwa kuwa lipo katika Hifadhi ya Taifa ya Selou ambayo nayo itafaidika kutokana na uwepo wa umeme huo.

Vilevile alisema kuwa, Wizara zote zitashirikiana kutekeleza Mradi huo kwakuwa utekelezaji wake unahusisha Wizara mbalimbali zikiwemo Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Alieleza kuwa hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu Mkandarasi atayetekeleza Mradi huo atakuwa amekwishapatikana na kuanza ujenzi wa mradi huo utakaokamilika kwa kipindi cha miaka 3.

Aliongeza kuwa kinachofanyika sasa katika eneo la mradi huo ni ukamikishaji wa miundombinu ya Barabara, Reli, Maji pamoja na Umeme vitakavyotumiwa na mkandarasi wakati wa kutekeleza Mradi huo.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alieleza kuwa Mradi utatoa  fursa kubwa ya ajira za muda mfupi na zile za muda mrefu kwa watanzania wenye taaluma husika na wale walio na uwezo na ujuzi.Aliwataka watanzania hasa Vijana kuchangamkia fursa hiyo katika kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza aliahidi kutoa elimu kwa Wananchi wa Mkoa wa Iringa ambao sehemu kubwa ya mito yake hutiririsha maji katika Bonde la Mto Rufiji.

Aidha alisema kuwa ataendelea kuwaelimisha Wakazi wa Iringa kuweka njia Bora za kilimo cha umwagiliaji zitakazotumika katika kilimo badala ya ile iliyozoeleka ya kulima Vinyungu katika vyanzo vya maji na Maeneo Oevu.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua wakiteta jambo wakati wa Warsha ya Wadau wa Mradi wa kuzalisha umeme Rufiji wa megawati 2,100 iliyofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mkoani Iringa.

Kwa upande wao Wabunge wa Mkoa huo akiwepo Mbunge wa Mafinga mjini, Cosato Chumi na mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto walisema kuwa watahakikisha Mradi huo unatekelezwa na hakutakuwa na changamoto zitakazoweza kuukwamisha kuanzia hatua za awali hadi mwisho.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Viongozi pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake akiwemo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), Mhandisi Amos Maganga.

Na Zuena Msuya, Iringa.