• Atoa maagizo kwa Wakandarasi

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amewasha umeme katika Kijiji cha Mbuyuni Kata ya Oljoro wilaya ya Arumeru mkoani Arusha ikiwa ni  matokeo ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu (REA III) unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Hafla ya kuwasha umeme huo ilifanyika tarehe 17 Machi, 2018 kijijini hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali mkoani humo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Mbuyuni mkoani Arusha (hawapo pichani) kuhusu kifaa cha UMETA (Umeme Tayari) kinavyofanya kazi bila kuhitaji kutandaza nyaya ndani ya nyumba. Alitoa elimu hiyo katika hafla ya kuzindua upatikanaji wa huduma ya umeme katika kijiji cha Mbuyuni mkoani Arusha. Anayeshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Kabla ya kuwasha umeme katika kijiji hicho Dkt. Kalemani alitoa maagizo mbalimbali kwa wakandarasi wa umeme vijijini, watendaji wa REA na TANESCO.

Dkt. Kalemani aliagiza kuwa, umeme usambazwe katika vijiji na vitongoji vyote bila kurukwa, aidha nyumba za udongo pia ziwekewe umeme.

Agizo jingine, ni kila mwananchi anapolipia huduma ya umeme, anapaswa kuunganishiwa huduma hiyo ndani ya siku ya Saba.

Aidha aliagiza kuwa, Mameneja wa TANESCO waanzishe vikosi kazi katika maeneo yao kwa ajili ya kukagua miundombinu ya umeme ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaokosa umeme kutokana na miundombinu hiyo kupata hitilafu.

Pia aliziagiza Halmashauri zote nchini kutenga fedha za kuunganisha umeme katika Taasisi za umma na zinazotoa huduma za kijamii kama vile Shule, Vituo vya Afya na visima vya Maji ili mkandarasi wa umeme anapofika katika eneo husika aingize umeme. Alisema kuwa ataanza kufuatilia utekelezaji wa agizo hili mwezi Juni mwaka huu.

Vilevile aliagiza kuwa, ifikapo mwezi Aprili mwaka huu, kila mkandarasi awe ameshaanza kuwasha umeme katika eneo lake la kazi.

Kuhusu maeneo ambayo tayari yamepitiwa na miundombinu ya umeme, Dkt Kalemani aliagiza kuwa, kila mkandarasi asambaze umeme kuanzia vijiji vitatu na kuendelea ndani ya siku Saba kwani katika maeneo hayo kinachohitajika ni kushusha umeme tu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alieleza kuwa Kata hiyo ya Oljoro ilikuwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme hivyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri wa Nishati kwa juhudi wanazofanya ambazo zimepeleka Kata hiyo kuanza kupata umeme.

Kuhusu suala la watu wanaojifanya kuwa ni maafisa wa TANESCO  (vishoka) na kuomba rushwa kwa wananchi ili wawaunganishie umeme, alisema kuwa umeme huo unatolewa na Serikali na kuwataka wananchi kutotoa fedha zaidi ya iliyowekwa na Serikali ambayo ni shilingi 27,000.

Baadhi ya Wananchi katika kijiji cha Mbuyuni mkoani Arusha wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati wa hafla ya kuzindua upatikanaji wa huduma ya umeme katika kijiji hicho.

Meneja wa TANESCO katika mkoa wa Arusha, Mhandisi Gasper Msigwa alieleza kuwa katika mradi huo wa REA III, (mzunguko wa kwanza) vijiji 58 vitasambaziwa umeme mkoani humo ambapo wateja 6,409 wataunganishiwa umeme.

Alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, tayari upembuzi yakinifu umefanyika kwa asilimia 100 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 90.34 na gharama za mradi ni shilingi bilioni 9.3.

Katika ziara hiyo Waziri Kalemani pia alitembelea kata ya Terati wilayani Arumeru na kuahidi kuwa vijiji 7 katika kata hiyo vitasambaziwa umeme kuanzia mwezi Aprili mwaka huu.

Teresia Mhagama na Zuena Msuya, Arusha