Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameendelea kuzindua upatikanaji wa huduma ya umeme katika vijiji mbalimbali nchini ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu  (REA III) unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (aliyeshika kipaza sauti), akimkabidhi Kifaa cha Umeme Tayari (UMETA), Mbunge wa Kuteuliwa, Anne Kilango Malecela kwa ajili ya kukigawa kwa wananchi katika kijiji cha Ndungu wilayani Same.

Akiwa mkoani Kilimanjaro, tarehe 9 Mei, 2018, alizindua huduma hiyo katika Kijiji cha Maguzo Mawili wilayani Same na Kijiji cha Kijiweni wilayani Siha pamoja na kukagua kazi ya usambazaji umeme inayoendelea katika vijiji mbalimbali mkoani Kilimanjaro.

Akiwa katika Kijiji cha Ndungu wilayani Same, alimwagiza Mkandarasi anayesambaza umeme kijijini hapo kuhakikisha kuwa anawasha umeme katika kijiji hicho ndani ya Siku Saba na kuhakikisha kuwa umeme huo unasambazwa katika vitongoji vyote vya Kijiji cha Ndungu.

Aidha, akiwa katika kijiji cha Ngarenairobi wilayani Siha na Kisiwani wilayani Same, Dkt Kalemani aliwaagiza watendaji wa TANESCO kuhakikisha wanafungua vituo vya kutoa huduma kwa wananchi ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

“Serikali ina magari, Pikipiki na vitendea kazi  ambavyo vitawawezesha kuwafikia hawa wananchi na kuwapa huduma, hivyo tuwaondolee adha ya wao kusafiri kufuata huduma pale tulipo bali sisi tuwafuate wao,” alisema Dkt Kalemani.

Vilevile, Dkt Kalemani aliwapongeza watendaji wa TANESCO mkoani Kilimanjaro kwa kufungua zaidi ya vituo 35 vya kuhudumia wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani humo suala linalopeleka wananchi hao kupata huduma kwa haraka.

Kuhusu mradi wa REA III, mzunguko wa kwanza ambao utakamilika Juni, 2019, Dkt Kalemani alisema kuwa mradi huo unahusisha zaidi ya vijiji 3559 nchini na katika mkoa wa Kilimanjaro, takriban vijiji 83 vitafaidika ikiwa ni pamoja na vitongoji vyake.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Staki, Mbunge wa Jimbo la Siha, Godwin Mollel na Mbunge wa Kuteuliwa, Anne Kilango Malecela.

Mbunge wa Jimbo la Siha, Godwin Mollel akizungumza na wananchi katika kijiji cha Ndungu wilayani Same mara baada ya kufika kijijini akiwa ameambatana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) ili kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini.

Pamoja na kupongeza kazi ya usambazaji umeme vijijini, Viongozi hao, waliishauri Serikali kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini ili vijiji vingi vifikiwe na huduma hiyo ndani ya muda uliopangwa.

Na Teresia Mhagama, Kilimanjaro