Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, tarehe 4 Oktoba, 2018, alifanya ziara katika eneo la mradi wa umeme wa Rufiji (2100) ambapo pia alikagua ujenzi wa kituo cha reli ya Tazara kitakachotumika kushusha mizigo wakati wa utekelezaji wa mradi huo wa umeme.

MASUALA MUHIMU ALIYOYASEMA MHE. KASSIM MAJALIWA

#Kila mmoja aliyepewa jukumu la kusimamia mradi ahakikishe anawajibika kikamilifu ili mradi huo ufanikiwe, na endapo wataalam zaidi watahitajika taarifa zitolewe kwa mamlaka husika ili kutochelewesha utekelezaji.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Kassim Majaliwa akitazama eneo litakalotumika kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya Mto Rufiji wakati alipotembelea eneo hilo Oktoba 4, 2018. Kushoto kwake ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.

# Wakuu wa Mikoa na Wilaya zinazozunguka eneo la mradi wahakikishe kuwa ulinzi unaimarishwa wakati wote  ikiwa ni pamoja na ulinzi wa watu na vifaa vinavyotumika katika mradi huo.  Wananchi pia wana jukumu la kulinda eneo hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

#Kazi za ujenzi wa mradi wa umeme zitakapoanza, matangazo yatolewe na usaili ufanyike katika mikoa inayozunguka mradi ili vijana wafaidike.

# Wananchi wameanza kuona faida za mradi wa umeme wa Rufiji kwani Vijiji vinavyopitiwa na  miundombinu inayopeleka umeme katika eneo la mradi  tayari vimeshaunganishwa na huduma ya hiyo.

# Mradi  utajengwa katika muda uliokusudiwa na kwa sasa Wizara inaendelea na majadilano na mkandarasi anayetarajiwa kutekeleza mradi husika.

# Mradi wa umeme wa Rufiji una malengo malengo manne, kuu likiwa ni kupata umeme na mengine ni kudhibiti mafuriko yanayojitokeza mara kwa mara kwa wakazi wa Wilaya ya Rufiji, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuimarisha sekta ya utalii.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka wa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) kuhusu ujenzi wa tawi la reli litakalounganisha Stesheni ya Fuga katika reli ya TAZARA na eneo utakapojengwa Mradi wa Umeme wa Maporomoko ya Mto Rufiji wakati alipotembelea eno hilo Oktoba 4, 2018.

# Selou ni eneo lililohifadhiwa kisheria lakini kumekuwa na tabia ya uharibifu wa mazingira kukata miti na utowekaji wa wanyama kutokana na uwindaji haramu  hivyo njia nzuri ya kudhibiti hilo ni uwepo wa umeme ambao utatumika kwa matumizi mbalimbali kama kupikia na kuona.

# Serikali inajikita katika kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kama maji na gesi ili nchi iwe na umeme mwingi, wa uhakika na gharama nafuu lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa mwananchi hadi wa kipato cha chini anaweza kumudu gharama za nishati.

# Ajira kwa vijana zimeshaanza kutolewa katika miradi wezeshi inayotekelezwa sasa ikiwemo ujenzi wa barabara na miundombinu ya   umeme.

# Vijana watakaopata ajira katika mradi huo wahakikishe kuwa wanafanya kazi kwa nguvu  zote na uaminifu.

# Kila mmoja ajikite katika fursa za biashara ikiwemo uuzaji wa chakula na huduma nyingine ili kuweza kufaidika  na mradi huo.

# Amepongeza Wizara ya Nishati kwa utekelezaji wa mradi wa umeme wa Rufiji ambapo imekuwa ikiratibu kazi mbalimbali zinazohusu mradi kwa kushirikisha Wizara nyingine.

MASUALA MUHIMU ALIYOYASEMA WAZIRI WA NISHATI, DKT.MEDARD KALEMANI

#Eneo la mradi lilianza kufanyiwa usanifu mwaka 1976 kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Norway kupitia Shirika la nchini Ureno la Norplan ambapo tafiti zilionyesha kuwa eneo hilo linaweza kuzalisha umeme wa megawati 2100.

#Mradi utatekelezwa katika hifadhi ya Selou ambayo ina jumla ya kilometa za mraba 50,000 lakini eneo litakalotumika kwa ajili ya mradi ni  kilometa za mraba 914 ambalo ni sawa na asilimia 2 tu ya eneo lote.

# Mgodi wa kuzalisha umeme utakuwa na uwezo wa kuzalisha kiasi cha umeme cha megawati 2100 hadi megawati 2, 263 ( kwa mujibu wa utafiti wa sasa).

#Kutakuwa na mitambo tisa ya kuzalisha umeme ambapo kila mtambo mmoja utazalisha megawati 235.

#Mradi uko kwenye hifadhi ya Selou ambapo shughuli mbalimbali zitafanyika lakini suala la kuhifadhi mazingira limepewa kipaumbele kwani  katika miti takriban bilioni 86,  miti itakayokatwa ni 16,000 tu ambayo ni sawa na asilimia 0.09.

# Kazi ya ujenzi itakapoanza. Mkandarasi  atatekeleza kazi hiyo ndani ya miezi 36  na kinachofanyika sasa ni utekelezaji  wa miradi wezeshi kama ujenzi wa barabara na umeme itakayomwezesha mkandarasi huyo kufanya kazi kwa ufanisi.

# Fedha kiasi cha shilingi bilioni 700 zimetolewa na Serikali kutekeleza miundombinu hiyo wezeshi.

#Ujenzi wa barabara na ukarabati wa madaraja kufika eneo la mradi ( barabara ya kutoka Kibiti hadi na eneo la mradi na barabara ya kutoka Ubena Zomozi hadi eneo la mradi) umefikia asilimia 88.

# Kazi ya kupeleka umeme katika eneo la mradi ( kV 33) kutoka Msamvu Morogoro kwa umbali wa kilometa 69. 2 imekamilika na kinachofanyika sasa ni kutandaza nguzo katika eneo la mradi.

# Kazi ya kujenga miundombinu ya maji kwa ajili ya wafanyakazi watakaokuwa katika eneo la mradi imekamilika kwa asilimia 100.

#Kazi ya kujenga na kupanua reli katika eneo la Fuga inatarajiwa kukamilika mwezi huu.

# Kazi ya kukuza mawasiliano katika eneo la hifadhi inaendelea.

Matarajio ni kuwa shughuli zote zitakamilika ifikapo tarehe 10 mwezi huu.

Na Teresia Mhagama