Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Medard Kalemani amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kukamilisha sehemu ya kwanza ya kazi ya upanuzi wa kituo cha umeme cha Zuzu ambayo imepelekea mkoa wa Dodoma kuwa na umeme wa kiasi cha megawati 248 badala ya megawati 48 zilizokuwa zikipatikana awali kutoka kwenye kituo husika.

Waziri Kalemani ametoa pongezi hizo tarehe 23 Desemba, 2020 mara baada ya kukagua kazi ya upanuzi wa kituo hicho  ambapo sehemu ya kwanza ya upanuzi inahusisha ujenzi wa kituo hicho cha umeme cha kV 220 na sehemu ya pili ya upanuzi inahusisha ujenzi wa kituo cha kV 400.

Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza na watendaji wa TANESCO na Wizara ya Nishati mara baada ya kukagua sehemu ya kwanza ya kazi ya upanuzi wa kituo cha umeme cha Zuzu mkoani Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Mradi wa Zambia-Tanzania-Kenya, Interconnector, Mhandisi Peter Kigadye.

Dkt.Kalemani ameeleza kuwa, alitoa agizo kuwa mradi huo ukamilike ifikapo mwezi Desemba mwaka huu na TANESCO wamefanikiwa kukamilisha kazi husika wiki iliyopita na  kukifanya kituo hicho kuwa na uwezo wa megawati 248 tofauti na hapo awali ambapo kilikuwa na uwezo wa megawati 48.

Kuhusu kazi ya ujenzi wa kituo cha umeme cha kV 400 amesema kuwa, kazi nyingi zimeshafanyika hivyo alitoa agizo kuwa, kikamilike mwanzoni mwa mwezi Machi, mwaka 2021.

“Kukamilika kwa kituo hiki kunamaanisha kuwa, Dodoma sasa hivi tuna uwezo wa megawati 248 na matumizi ni megawati 48 tu kwa sasa, hivyo tuna ziada ya megawati 200.” Amesema Dkt.Kalemani

Amesema kuwa, kuwepo kwa megawati 248 kunaifanya Dodoma kuwa na umeme mwingi hivyo amewakaribisha wawekezaji wa  ndani na nje ya nchi kuwekeza Dodoma kwani umeme upo wa kutosha.

Dkt. Kalemani ameongeza kuwa, kwa mkoa wa Dodoma, lengo ni kuwa na megawati 648, ambapo lengo hilo litatimia mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha umeme cha kV 400 ambacho kitakamilika mwanzoni mwa mwezi Machi mwakani.

Kutokana na uwepo wa umeme huo wa kutosha, Dkt.Kalemani ametoa agizo kwa TANESCO kutokukata umeme hasa katika msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, amesema agizo hilo la kutokata umeme ni kwa nchi nzima.

Aidha, kuhusu changamoto ya wapimaji wa maeneo yanayotakiwa kuunganishiwa umeme (surveyors) kuchelewa kutoa huduma kwa wananchi, ametoa agizo kwa TANESCO kuwanunulia pikipiki ili kuweza kutoa huduma kwa haraka.

Vilevile, kuhusu suala la ukataji wa umeme kwa wadaiwa mbalimbali zikiwemo Taasisi za Umma na Binafsi ameeleza kuwa,wateja wote wanapaswa kulipa madeni yao kwa wakati, la sivyo watakatiwa umeme.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Zambia-Tanzania-Kenya, Interconnector, Mhandisi Peter Kigadye, ameeleza kuwa, agizo la Waziri wa Nishati, la kukamilisha ujenzi wa kituo cha kV 400, mwanzoni mwa mwezi Machi, 2021, litakamilika ndani ya muda ulioagizwa.