Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato wamefanya ziara  kwenye ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) kwa ajili ya kujionea utekelezaji wa mradi huo ambao utazalisha umeme wa kiasi cha megawati 2115.

Ziara hiyo ilifanyika, tarehe 14 Desemba, 2020  na kuwahusisha Naibu Katiku Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard  Masanja, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Edward Ishengoma, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi, Mkuru mbalimbali kutoka katika Wizara ya Nishati na Taasisi zake.

Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato na Naibu Katiku Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja wakiwa pamoja na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa (mwenye shati nyekundu) pamoja na wataalam mbalimbali wakikagua maeneo mbalimbali ya mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP), Desemba 14, 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada kumaliza kukagua mradi huo, Waziri Kalemani amesema kuwa , Serikali imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo, ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi katika mradi huo.

“Tunataka mradi ukamilike  kwa wakati na kwa kiwango cha juu, sio mradi unakamilika baada ya miezi miwili unaanza kuhitaji tena ukarabati kwa gharama nyingine, kwa hili hatutakubali, kwa hiyo nitoe wito kwa mkandarasi kufanya kazi kwa weledi na kiwango cha juu.” Alisema Dkt. Kalemani

Dkt. Kalemani pia ametoa agizo kuwa, amesitisha likizo za sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya kwa mkandarasi pamoja na msimamizi wa mradi huo,ili watumie muda huo kufanya kazi kwa kasi ili mradi ukamilike kwa wakati.

Pia, amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha kuwa  wataalam wote ambao wanahitajika kwenye mradi huo wafike mara moja kwenye mradi huo ili kazi zifanyike kwa haraka.

Vilevile, amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anajiri waatalam  wote ambao wanahitajika katika ujenzi wa mradi huo na ifikapo mwisho wa mwezi huo wawe tayari wamefika nchini kwa ajili ya ujenzi huo.

Dkt. Kalemani ameongeza kuwa, mradi wa Julius Nyerere utapeleka umeme kwenye gridi ya Taifa pamoja na kwenye miundombinu yenye uhitaji wa umeme kwa gharama nafuu.

Mafundi wakiendelea na shughuli za ujenzi wa katika mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere(JNHPP), Desemba 14, 2020.

Pia umeme huo utapelekwa kwenye vijiji 12,268 nchi nzima pamoja na kwenye Vitongoji vyake ambavyo vinafikia 64,889.

Aidha, Dkt. kalemani ameeleza kuwa, kutokana na umeme wa maji kuzalishwa kwa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine, inatarajiwa kuwa, kukamilika kwa mradi kutasaidia kushusha bei ya umeme kwa watumiaji.

Akitoa tathmini ya jumla ya utekelezaji wa mradi, Waziri Kalemani amesema kiujumla mradi unaendelea vizuri ambapo eneo la uchepushaji maji limekamilika kwa asilimia 100, wakati eneo la ujenzi ambapo bwawa linahitajika kujengwa umbali wa mita 1,045 pamoja na kimo cha mita 131 unaendelea vizuri.

Kwa upande wake Naibu Waziri Nishati, Mhe. Stephen Byabato, ameelezea kufarijika na kasi ya ujenzi wa mradi huo na kuahidi kusimamia maagizo ya Waziri ili kuona yote yaliyoagizwa yanatekelezwa kwa wakati, ubunifu mkubwa na kwa usahihi.

Naye, Naibu Katiku Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard  Masanja, amesema kwamba kila mmoja katika taasisi zote zilizopo chini ya Serikali ambaye kwa njia moja au nyingine anahusika katika utekelezaji wa mradi huo analojukumu la kutekeleza wajibu wake ili mradi uende kwa kasi inayotakiwa na uweze kukamilika kwa wakati.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani pia alitembelea kijiji cha Mtemle kilichopo karibu na mradi huo na kuwaahidi wananchi wa kijiji hicho kuwa Serikali itakikisha inasimamia zoezi la upatikanaji wa ajira kwa usawa, kwa wananchi wote wanoishi katika wilaya zinazopakana na mradi huo.