Halmashauri za Wilaya nchini zimeshauriwa kutenga fedha kwa ajili ya kuziunganishia Taasisi za umma huduma ya umeme katika Mradi wa kusambaza umeme vijijini wa REA Awamu ya Tatu.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto) akiteta Jambo na mbunge wa Manonga katika Kijiji cha Matinje baada ya kukagua Mradi wa REA III, katika wilaya ya Igunga mkoani Tabora.

Ushauri huo ulitolewa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi  wa REA  Awamu ya Tatu katika Kijiji cha Miguha wilayani Nzega na kijiji cha Matinje  wilayani Igunga mkoani Tabora.

Dkt. Kalemani alisema kuwa licha ya Taasisi za umma kupewa kipaumbele katika kuunganishwa na huduma za umeme lakini halmashauri nyingi zimekuwa hazitengi fedha wala kutandaza nyaya katika Taasisi hizo zilizopitiwa na Mradi wa REA III na kusababisha changamoto katika kutekeleza mradi huo pamoja kuwaletea adha wananchi.

Alisisitiza kuwa ni vyema halmashauri zikatumia fursa ya umeme wa REA katika kuziunganisha Taasisi za Umma kwa kuwa huduma ya umeme huo hupatikana kwa bei nafuu zaidi tofauti na kuunganishwa kwa gharama za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

“Mradi wa REA unapita katika kila Kijiji, Halmashauri zote zinafahamu hili cha ajabu hazitengi fedha kwa hiyo Shule, Hospitali na Taasisi zote zinazotoa huduma kwa jamii haziunganishwi na huduma ya umeme, Halmashauri tengeni fedha wananachi wapate huduma bora na za kisasa”, alisema Kalemani.

Aidha, aliwasisitiza Wananchi hasa wasio na nyumba zinazohitaji kutandaza nyaya (wiring) kuchangamkia fursa ya mradi wa Umeme Vijijini kwa kutumia kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kitakachopatikana bure kwa wateja 200 wa mwanzo watakaolipia huduma ya umeme.

Katika ziara hiyo Dkt. Kalemani alisema kuwa kuanzia mwezi Septemba mwaka huu nguzo za zege zitaanza kutumika ili kumaliza tatizo la kudondoka kwa nguzo zilizochakaa au kuchomwa Moto wakati wa kuandaa msimu wa kilimo.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akikagua Mradi wa usambazaji Umeme Vijijini REA III katika Kijiji cha Miguha wilayani Nzega mkoani Tabora.

Aliweka wazi kuwa nguzo hizo zitatengenezwa hapahapa nchini ambapo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litakuwa na kiwanda cha kutengeneza nguzo hizo pia wawekezaji wa ndani na nje wanaalikwa kuanzisha viwanda vyao nchini.

“Nguzo yoyote ya umeme itakayoanguka iwe kwa upepo, kuoza au kuchomwa moto kuanzia mwezi Septemba mwaka huu mbadala wake itasimamishwa nguzo ya zege hivyo kumaliza kabisa tatizo la nguzo kuangua mara kwa mara, nguzo hizi za zege zinadumu muda mrefu,” alisisitiza Dkt.Kalemani.

Katika hatua nyingine, DKt.Kalemani aliwaalika wawekazi wa nje na ndani kuwekeza mkoani Tabora kwa kuwa Mkoa huo una Nishati ya umeme ya kutosha na ziada ambayo wakazi wake hawawezi kuitumia yote.

Na Zuena Msuya Tabora.