Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wadau mbalimbali wanaohusika katika mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2100) wakiwemo wanaohusika na ujenzi wa  miundombinu ya umeme, maji, barabara pamoja na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na ofisi kukamilisha miundombinu hiyo kwa wakati uliopangwa au hata kabla.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto ) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Ramadhan Maneno (kulia) wakinawa maji ya moto katika ziwa Tagalala kwenye hifadhi ya mbuga ya Selou. Maji hayo yanayoashiria uwepo wa jotoardhi inayoweza kutumika kuzalisha umeme.

Aliyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miundombinu ya miradi mbalimbali ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa umeme wa Rufiji.

Naibu Waziri alikagua ujenzi wa miundombinu ya barabara, umeme, Kituo cha Reli, ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na ofisi pamoja na maji ambayo inaendelea kutekelezwa huku baadhi ikiwa imekamilika kwa asilimia kubwa.

Mgalu alisema kuwa, miundombinu hiyo ni vyema ikakamilika mapema ili mradi huo utakapoanza rasmi kusiwe na kikwazo chochote katika utekelezaji.

” Mradi huu utakapokuwa unaanza utakuwa ukienda kwa kasi kubwa kwelikweli, sasa kusiwe na kikwazo cha kutotekeleza Mradi huu, nawasihi wadau wa umeme, barabara, nyumba, maji pamoja na reli mharakishe kukamisha kazi zenu kwa wakati”, alisisitiza Mgalu.

Aidha alieleza kuwa, kazi ya  maandalizi ya mradi wa uzalishaji umeme wa Rufiji inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 700 katika utekelezaji wake..

“Umeme unaozalishwa kwa gesi hapa nchini ni asilimia 49 ambapo kwa sasa megawati zinazopatokana nchini ni zaidi ya megawati 1,500 na matarajio ni kuzalisha megawati  5,000  ifikapo 2020 na mipango inaendelea zaidi ili kupunguza tatizo la ukosefu wa umeme katika baadhi ya maeneo hapa nchini,” alisema Mgalu.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto ) akigawa taa za umeme jua katika moja ya zahanati zilizokosa huduma ya umeme katika Wilaya ya Rufiji.

Vile vile aliwataka watendaji wa Serikali za mitaa na jamii zinazoishi katika maeneo yote kunapofanyika  mradi huo kwa namna moja ama nyingine kushirikiana ili kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili mradi utekelezeke kwa ufanisi.

“Kidakia maji hakina athari ila kuna tatizo la athari za kibinadamu ikiwemo kilimo katika vyanzo vya maji na uingizaji wa mifugo na shughuli nyingine za kibinadamu wananchi wote tushirikiane pamoja kuhakikisha mazingira hayaharibiwi na watu wachache “, alisema Mgalu.

Naye mjumbe wa Kamati ya usimamizi ya utekelezaji wa mradi huo wa Rufiji,  Mhandisi Stanslaus Kizzy alisema kuwa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo  zimeanza kutolewa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuandaa utekelezaji wa  mradi huo .

Kizzy alisema kuwa, utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika awamu tatu, ambapo kazi ya kwanza ni kuchepusha mto,  pili itakuwa kujenga ukuta, tatu na mwisho ni kujenga nyumba itakayowekwa mitambo tisa ya kuzalishia umeme.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno alisema wamejionea hatua mbalimbali zinazoendelea kuhusu  mradi huo na kuipongeza Serikali ya awamu ya Tano kwa uamuzi wa kutekeleza kwa vitendo mradi huo ulioanza kuzungumzwa tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Maneno alisema kuwa, wananchi wa vijiji jirani pia watanufaika moja kwa moja kwa  kuunganishwa na huduma ya umeme wa uhakika, ubora wa barabara na huduma ya maji, pamoja na Afya.

Utafiti wa mradi huo ulianza miaka ya 80 ambapo Mwasisi wake ni Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage  Nyerere ambapo kwa wakati huo nyumba kadhaa zilijengwa ambazo kwa sasa  zinakarabatiwa.

Katika ziara hiyo pia Naibu Waziri wa Nishati,  Mgalu, alitembelea eneo lenye maji ya moto katika  Ziwa Tagalala  ndani ya Mbuga ya Selou, maji hayo ni kiashiria cha uwepo wa Nishati ya Jotoardhi, ambayo inaweza kuzalisha umeme.

Alifafanua kuwa Serikali imetenga zaidi ya Shilingi milioni 36, kuwezesha utafiti wa maeneo na kuweka mipango thabiti ya kuweza kuzalisha umeme kwa kutumia jotoardhi .

Aidha aliendelea na zoezi kugawa  taa za umeme jua katika zahanati za vijiji ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme ili taa hizo zirahisishe utoaji wa huduma kwa akina mama wajawazito ambapo alitoa katika Vijiji vya Ngorongo na Kilimani na kufanya idadi ya zahanati   zilizopatiwa taa hizo kufikia 36.

Na Zuena Msuya