Ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Mradi wa usambazaji  umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), Waziri wa Nishati,  Dkt. Medard Kalemani amewateua Wahandisi Saba (7) kutoka Wizara ya Nishati watakaosimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na Wahandisi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaosimamia mradi huo.

Dkt. Kalemani alifanya uteuzi tarehe  4 Machi, 2018 baada ya kufanya mkutano na Wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza Mradi wa REA III,  Wenye Viwanda vya kutengeneza miundombinu ya umeme kama vile Trasfoma, Mita, pamoja na nyaya za umeme, Mameneja wa TANESCO wa Kanda na Wahandisi wanaosimamia Mradi ya REA III nchi nzima.

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa wadau wa wanaotekeleza Mradi wa REA III uliofanyika katika ukumbi wa Hazina – Dodoma.

Mkutano huo ulifanyika katika Makao Makuu ya Nchi, Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine ulilenga kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu pamoja na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Mradi huo.

Dkt.Kalemani alisema kuwa, Wahandisi walioteuliwa watashirikiana na Wakandarasi wa REA III ili kufanikisha kazi ya usambazaji umeme vijijini ambapo aliwaagiza Wahandisi hao kuwa na Mpango Kazi wa kila wiki wa kila Mkandarasi katika eneo husika ili kusisimamia kwa ukaribu utekelezaji wa kazi wa Mkandarasi wa umeme.

Alisema kuwa, Wahandisi hao wa Wizara  watarahisisha mawasiliano kati ya Wizara ya Nishati na Wakandarasi wa Umeme Vijijini suala litakalopelekea Wizara kufahamu hatua mbalimbali zinazofikiwa katika utekelezaji wa mradi pamoja na  changamoto watakazokuwa wakikabiliana nazo na hivyo kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Dkt.Kalemani aliwataka wakandarasi hao kutumia busara na uzalendo katika kuwaunganisha Wananchi na huduma ya umeme ambapo alisema kuwa mbali na kuwepo kwa mikataba inayowaongoza wakandarasi hao kutekeleza majukumu yao, lakini kuna maeneo ambayo wanapaswa kuyafikia pasipo kuangalia makubaliano ya mkataba.

” Nawasihi sana Wakandarasi mtumie busara  na uzalendo katika kuunganishia Wananchi umeme,  kwa mfano utakuta Kijiji kina Shule au Zahanati,  kimepitiwa na mradi wa umeme lakini hakipo kwenye orodha ya Vijiji mlivyopewa katika mkataba, nawasihi sana kwa tumieni  busara kuwaunganishia umeme”, alisema Dkt. Kalemani

Aidha, aliwataka Wakandarasi hao kuendelea kutumia bidhaa za ndani katika kutekeleza Mradi huo pia kununua bidhaa kutoka viwanda tofauti hapa nchini ili kuweka ushindani wa kibiashara pamoja na bei.

Kwa upande wa wenye Viwanda, Dkt. Kalemani, aliwataka kuzalisha bidhaa zenye ubora na zenye viwango vinavyotakiwa ili kuendelea kukuza soko la ndani na nje pia kuuza bidhaa hizo kwa bei nafuu.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ( katikati), Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua (kulia) wakisikiliza maoni ya wadau wanaotekeleza mradi wa REA III katika ukumbi wa Hazina wakati wa mkutano wa wadau hao uliofanyika Dodoma.

Vilevile aliwaahidi wakandarasi hao kuwa kwa sasa Serikali itaharakisha ulipaji wa madeni wanayoidai tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Aliwataja Wahandisi aliowateua kusimamia Mradi wa REA III kuwa ni

Mhandisi Salum Inegeja atakayesimamia Kanda ya Ziwa, Mhandisi John Kitonga Kanda ya Nyanda za Juu, Mhandisi Juma Mkobya Kanda ya Magharibi, na Mhandisi Ahmed Chinemba Kanda ya Kati.

Wengine ni Mhandisi Samuel Mgweno Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Christopher Bitesigirwe Kanda ya Pwani pamoja na Mhandisi Styden Rwebangira Kanda ya Kusini.

Na Zuena Msuya, Dodoma.