Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ametoa maagizo kwa watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa Mkandarasi aliyepewa kazi ya kubomoa jengo la Shirika hilo lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam anakamilisha kazi kabla ya tarehe 30 Desemba 2017.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo, tarehe 22 Desemba, 2017 alipofanya ziara katika eneo hilo ili kukagua hatua zilizofikiwa katika kazi ya kubomoa jengo hilo ili kupisha ujenzi wa Daraja la ghorofa Tatu la Ubungo (Ubungo Interchange).

“Wasimamieni hawa Wakala wa Majengo (TBA) mliowapa kazi hii,  vinginevyo mtafanya wenyewe, TBA wana ujuzi hivyo wasimamieni, hakuna  cha Krismasi wala Mwaka Mpya kwenye kubomoa jengo hili, hivyo mwisho wa mwezi huu, jengo la mbele ambalo limekusudiwa kubomolewa, liwe limeanguka chini”, alisema Dkt Kalemani.

Alisema kuwa,  ifikapo tarehe 1 Januari, 2018 atafanya ziara tena katika eneo hilo ili kuona kama agizo hilo la Serikali limefanyiwa kazi kabla ya kuchukua hatua stahiki kwa watakaohusika na kutotekelezwa kwa agizo hilo.

“Wananchi wamebomoa, bado sisi hivyo nawaagiza msimamie usiku na mchana, na hakikisheni wafanyakazi wa TANESCO wanaosimamia jengo hili na wakandarasi mliowaweka hapa hawaendi sikukuu hivyo wote washirikiane kubomoa jengo hili,” alisisitiza Dkt Kalemani.

Dkt Kalemani pia alitoa agizo kwa wataalam wa TANESCO wanaohusika na huduma kwa wateja kutosafiri nje ya vituo vya kazi ili kusimamia miundombinu ya umeme wakati wa msimu wa Sikukuu na hivyo wananchi wapate umeme  wa uhakika wakati wa Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Kahitwa Bishaija alisema kuwa watahakikisha agizo hilo linatekezwa kama maagizo yalivyotolewa.

Agizo la kubomolewa kwa jengo hilo lilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 15 Novemba, 2017 wakati alipokuwa akikagua  Ujenzi wa Daraja la juu Tazara (Tazara Fly-Over) na Ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo (Ubungo Interchange).

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Ubungo, Rais Magufuli alimuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania  (TANROADS),   Mkoa wa Dar es salaam,  kuvunja sehemu ya jengo la TANESCO na jengo la Wizara ya Maji yaliyopo katika eneo la hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.

”Sheria ya hifadhi ya Barabara katika eneo hilo ni mita tisini kila upande kutoka katikati ya barabara hivyo ni lazima sheria hiyo iheshimiwe ili kuharakisha ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu katika eneo hili la Ubungo, sheria ni msumeno haina budi kuzingatiwa hata na Serikali yenyewe” alisema Dkt. Magufuli.

Na Teresia Mhagama, DSM