Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea katika siku yake ya Tatu, Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Kamati ya Nishati ya Baraza hilo imekutana leo tarehe 1 Oktoba, 2017, ambapo Kamati hiyo imepitia na kujadili masuala yote yaliyoibuliwa katika Vikao vya Timu ya Wataalam wa nchi Wanachama.

Mkutano huo ulianza na Timu za Watalaam wa Nishati kutoka nchi Wananchama tarehe 30 Oktoba, 2017 ambapo masuala kadhaa kuhusu Sekta ya Nishati ikiwemo Gesi, Mafuta, Umeme, Nishati Jadidifu na Matumizi Bora ya Nishati yalijadiliwa.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Sekta za Kijamii na Uzalishaji, Christophe Bazivamo (kulia) na Mwenyekiti wa mkutano kutoka nchini Uganda Kaimu Kamishna kutoka Idara ya Petroli, Utafiti na Uzalishaji nchini humo, Honey Malinga, (kushoto) wakifuatilia kikao hicho.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Nishati cha Baraza hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Sekta za Kijamii na Uzalishaji,  Christophe Bazivamo amesisitiza umuhimu wa nishati kwa jumuiya hiyo na kuongeza kuwa, nchi wanachama wanapaswa kuzingatia kuwa nishati hiyo ndiyo kichocheo kikuu cha ukuaji uchumi kwa jumuiya hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mkutano  huo ambayo ni nchi ya Uganda, akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Kamishna kutoka Idara ya Petroli, Utafiti na Uzalishaji nchini humo, Honey Malinga, amewataka washiriki kutoka na ripoti nzuri ambayo itawezesha utekelezaji wa programu mbalimbali katika Sekta ya Nishati  zilizopangwa kutekelezwa  na jumuiya hiyo.

Aidha, amewataka kuyachukulia kwa uzito masuala yote yanayojadiliwa katika kikao hicho kwa kuwa yanalenga kuwezesha maendeleo na ukuaji uchumi kwa jumuiya hiyo.

Mapendekezo yanayojadiliwa   katika kikao cha Kamati ya Nishati cha Baraza hilo, yanatarajiwa kuwasilishwa katika Kikao cha Makatibu Wakuu wa nchi wanachama tarehe 2 Novemba, 2017, kabla ya kuwasilishwa katika kikao cha Mawaziri wa Nishati ifikapo tarehe 3 Novemba, 2017.

Nchi wanachama zilizowakilishwa katika Mkutano huo ni Tanzania, Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi ambapo Mwenyekiti wa Mkutano ni nchi ya Uganda na Katibu wa mkutano huo ni Rwanda.

Wataalam mbalimbali kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na wakifuatilia kikao hicho.

Tanzania katika mkutano huo, inawakilishwa na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Mazingira na Nishati ya Zanzibar, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta, Zanzibar (ZURA).

Na Asteria Muhozya,Arusha