Nchi  Washiriki wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki wametakiwa kuongeza kasi ya upatikanaji Nishati miongoni mwa nchi hizo ili kuwezesha Mapinduzi ya Viwanda na kukuza uzalishaji wa ndani.

Hayo yamesemwa leo la Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Sekta za Kijamii na Uzalishaji,  Christophe Bazivamo wakati akifungua Mkutano huo  kwa upande wa Timu ya Wataalam kutoka nchi za Tanzania, Uganda, Rwanda, Uganda na Kenya.

Bazivamo ameeleza kuwa, ili nchi hizo ziweze kuendelea Kiviwanda zinahitaji kuwa na nishati  ambayo ndiyo kichocheo kikuu cha maendeleo na kwamba nishati ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele kwa Jumuiya hiyo.

Ameongeza kuwa, bado jamii kubwa ya wananchi wa Jumuiya hiyo hawajaunganishwa na nishati  ya umeme na kuongeza kuwa, ukosefu wa nishati ya umeme hauzuii tu maendeleo ya kiviwanda bali pia unadidimiza maendeleo ya watu.

Pia, ameongeza kuwa, mbali na kudidimiza maendeleo ya watu pia unaathiri sekta ya elimu kwa kuwa, kukosekana na nishati kunasababisha wanafunzi hususani waishio vijijini kutumia muda mwingi kutafuta nishati ya kuni kwa ajili ya kupikia badala ya kujikita na masomo.

Aidha, ameeleza kuwa, matumizi ya muda mrefu ya kuni kwa ajili ya kupikia pia  yanachangia kuathiri afya za kina mama wengi kutokana na moshi unaotokana na matumizi hayo.

Mkutano huo wa 12 wa Baraza la Kisekta pamoja na mambo mengine unatarajiwa kujadili maeneo mbalimbali katika Sekta ya Nishati ikiwemo umeme, Nishati Jadidifu, Gesi na Mafuta.

Mkutano huo ulioanza  leo tarehe 30 Oktoba,2017, unatanguliwa na Timu za Wataalam katika Sekta ya Nishati kutoka nchi husika . Baada ya mkutano wa Wataalam utafuatiwa na  mkutano wa Makatibu Wakuu kutoka nchi hizo na  kuhitimishwa  tarehe 3 Novemba,2017 na  Mawaziri wa Nishati wa nchi husika.

Tanzania inawakilishwa na Wataalam wa masuala ya Nishati kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) na Wataalam kutoka upande wa Zanzibar.