Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli Mhandisi Innocent Luoga amefanya ziara ya kukagua Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu unaotekelezwa katika Mkoa wa Lindi na Mtwara.

Katika ziara hiyo pia, alikagua Mradi wa Ujenzi wa Njia ya kusambaza umeme ya Msongo wa kilovolti 33 yenye urefu wa kilomita 17 ya kutoka Mahumbika hadi Ruangwa na kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ndani ya wakati.

Vilevile, alikagua ujenzi wa njia ya kusambaza umeme ya Msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 12 inayounganisha Mkuranga na Ikwiriri ili kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakamilika ifikapo tarehe 10/3/2018.

Pia, alitembelea Kituo cha umeme cha Mbagala ili kufuatilia uwezo wake wa kupeleka Umeme katika Wilaya za Ikwiriri na Kilwa.

Mbali na shughuli za kukagua mitambo, Kamishna Luoga pia alifanya ufuatiliaji wa upatikanaji wa Spare Parts za Mashine N0.8 ya Kituo cha Mtwara ili kuhakikisha zinapatikana ili mtambo huo uanze kufanya kazi.

Aidha, alikagua kazi ya ufungaji wa Mashine 2 mpya za kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia katika kituo cha Mtwara ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati.

Kamishna Luoga pia, alikagua Kituo cha kuzalisha umeme cha Somanga Fungu na kufanya kikao na Mkandarasi kampuni ya Reycon pamoja na kukagua eneo linalounganisha umeme wa SomangaFungu na Mtwara.

Kamishna Luoga alifanya ziara hiyo mwanzoni mwa wiki.