Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, amefurahishwa na maombi ya wawekezaji wa Kampuni ya CTC Power Equipment Co. Ltd, kutoka China, wenye nia ya kujenga Kiwanda cha kutengeneza vifaa maalum vinavyotumika kuzuia upotevu wa umeme vijulikanavyo kitaalam kama ‘Insulators.’

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, akiwa katika mazungumzo na Ujumbe kutoka Kampuni ya CTC Power Equipment ya China, waliwasilisha maombi ya kujenga kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kuzuia upotevu wa umeme (Insulators), Juni 18, 2018, Makao Makuu ya Wizara Dodoma. Wengine pichani ni wataalam wa Nishati wa Wizara.

Wawekezaji hao ambao wameingia ubia na Kampuni ya kizalendo iitwayo Interbest Investment Co. Ltd, waliambatana na Mkurugenzi wake, Augustine Masonga na kuwasilisha maombi hayo kwa Waziri, Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma, Juni 18, 2018.

Waziri Kalemani alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha vifaa vyote vinavyotumika kuunganisha umeme vinanunuliwa hapa nchini na tayari imekwishapiga marufuku kuagiza vifaa kama transfoma, nguzo na nyaya mbalimbali, ambavyo vinapatikana hapa nchini.

“Kwa upande wa ‘insulators’, tumeshindwa kutoa zuio hilo kwakuwa, hazipatikani nchini na hivyo tunalazimika kuziagiza kutoka nje ya nchi,” alisema Waziri na kuongeza kuwa, itakuwa ni faraja kubwa kwa Serikali endapo wawekezaji hao watafanikiwa kuanzisha Kiwanda husika ili kuepusha gharama kubwa zinazotumika kuagiza vifaa hivyo nje na pia kupunguza muda mrefu unaotumika katika kuvisafirisha.

Aliwataka wawekezaji hao kukutana na wataalam wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kujadiliana nao kuhusu suala la viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya vifaa husika. Pia, aliwataka kukutana na wataalam kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili waweze kufahamishwa viwango vinavyotakiwa nchini.

Waziri aliwapongeza wawekezaji hao kuingia ubia na mzalendo kwani ni moja ya vigezo vya kisera vinavyohitajika katika uwekezaji wa aina hiyo nchini.

Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Salum Inegeja (wa pili kutoka kulia), Sebastian Shana (wa tatu kutoka kulia) na Mhandisi Ahmed Chinemba (wa pili kutoka kushoto), wakijadiliana na Ujumbe kutoka Kampuni ya CTC Power Equipment kutoka China, baada ya kikao chao na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) ambapo waliwasilisha maombi ya kujenga kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kuzuia upotevu wa umeme (Insulators) nchini. Kikao hicho kilifanyika Juni 18, 2018 Makao Makuu ya Wizara Dodoma.

Alisema kuwa, mbali na kuwapatia ajira wananchi lakini pia itasaidia kuwapa fursa ya kujifunza teknolojia husika ili baadaye waweze wao wenyewe kuanzisha aina hiyo ya uwekezaji na kuisimamia kikamilifu.

Wawekezaji hao waliahidi kutekeleza yale yote waliyoelekezwa na Waziri na kusema kwamba wanatarajia kukamilisha kazi zote za maandalizi ndani ya kipindi cha miezi zita kutoka sasa, na hivyo Kiwanda kuanza kazi ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu au Januari mwakani.

Na Veronica Simba – Dodoma