Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imekagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Mara, ikiwa katika ziara yake ya kazi, Machi 15 mwaka huu.

Moja ya shughuli kubwa na muhimu iliyofanyika wakati wa ziara hiyo mkoani Mara ni kuwasha umeme katika kijiji cha Nyabange kilichopo Wilaya ya Butiama.

Kamishna wa Nishati Mhandisi Innocent Luoga (wa pili kutoka kulia) akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakati ilipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu. Katikati ni Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na kulia ni Mwenyekiti wa Kamati Dustan Kitandula.

Aidha, Kamati ilikagua utekelezaji wa miradi ya umeme katika vijiji vya Muryaza na Busegwe pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Mara.

Akiwasilisha taarifa husika kwa Kamati hiyo; Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania Mkoa wa Mara, Mhandisi Obay Sigala alisema kuwa, hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, Mkoa ulikuwa na jumla ya wateja 55,871 huku mahitaji ya juu ya umeme yakiwa ni megawati 31.5.

Kuhusu usambazaji wa umeme mkoani humo, Mhandisi Sigala alibainisha kuwa huduma ya upatikanaji wa umeme imeboreka kwa kiwango kikubwa baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga, Oktoba 2016.

“Wilaya zote zinapata umeme kutoka Gridi ya Taifa kupitia vituo vya Bunda, Musoma na Nyamongo, ambavyo vina uwezo wa kupokea jumla ya umeme wa kiwango cha megawati 72 (90MVA). Vituo hivi vinaendelea kupokea wateja wakubwa na wadogo katika kuendana na falsafa ya uchumi wa viwanda.”

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini awamu ya pili (REA II), Mhandisi Sigala alieleza kuwa, Mkoa huo umetekeleza mradi husika kuanzia mwaka 2013 na kukamilika Desemba 2016, ambapo Wilaya zote zimenufaika.

“Mradi huu umejumuisha ujenzi wa laini za kilovoti 33, laini ndogo ya kilovoti 0.4, ufungaji wa transfoma na uunganishaji wa wateja. Takribani wateja 12,500 kati ya wateja 14,520 waliotarajiwa, wameunganishiwa umeme ambao ni sawa na asilimia 86.1.”

Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakikagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.

Kwa upande wa utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu (REA III), Meneja Sigala alisema uzinduzi rasmi ulifanyika Machi 18, 2017 na utakamilika Mei 21mwaka huu.

Alitaja idadi ya vijiji vitakavyonufaika kuwa ni 58 na kwamba unatekelezwa na Mkandarasi Angelique International Limited kutoka India kwa gharama za Dola 3,347,620.78 na shilingi za Tanzania 1,498,345,851.96.

Na Veronica Simba – Mara