Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imewataka wananchi kuwa wazalendo na kujali maslahi ya nchi na taifa katika kutekeleza miradi ya mikubwa ya maendeleo ukiwemo mradi kuzalisha umeme wa maji wa megawati 2100 katika maporomoko ya bonde la Mto Rufiji.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ussi Pondeza, mkoani Njombe wakati wa mkutano wa Wadau wa mradi wa kuzalisha umeme wa maji katika maporomoko ya bonde la mto Rufiji.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ussi Pondeza ( katikati), Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( kushoto) na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga (kulia) wakifuatilia mada.

Pondeza alisema kuwa,  Watanzania wengi wamekuwa na tabia ya kupenda kuangalia maslahi yao binafsi kwa kutaka malipo makubwa ama fidia zinazoweza kuepukwa  pindi Serikali inapoanzisha miradi mikubwa ya maendeleo bila kujali kuwa miradi hiyo ni kwa manufaa ya Watanzania wote.

Alitoa angalizo kuwa,  tabia hiyo imekuwa ikichelewesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo  na hata wakati mwingine kukwamisha utekelezaji wake.

“Baadhi yetu sisi watanzania sijui tuna tabia gani, tunaletewa mradi kwa maendeleo yetu wenyewe lakini kwa vile ni wabinafsi tunaanza kukwamisha kwa kutaka fidia ili mradi mtu upate fedha! unasahau kuwa hizo ni juhudi za Serikali katika kutuletea maendeleo sisi wenyewe,” alisema Pondeza.

Aliongeza kuwa,  kuna baadhi ya watu wakikosa huduma fulani huilalamikia Serikali kuwa haijafanya kitu hali ya kuwa wao ndio walikuwa wakizuia utekelezaji hivyo aliwataka wabadilike.

Kwa upande wake,  Waziri wa Nishati,  Dkt. Medard Kalemani alisema katika kuelekea uchumi wa viwanda nchi inahitaji umeme mwingi, wa uhakika, gharama nafuu na unaotabirika.

Aliongeza, kuwa kwa sasa nchi ina umeme wa kutosha lakini hauwezi kutosheleza mahitaji ya miaka ijayo katika kujenga uchumi wa viwanda.

Alifafanua kuwa,  ili kutimiza adhma  ya Serikali ya uchumi wa Viwanda, sasa ni wakati muafaka wa kutekeleza miradi mikubwa ya nishati ya umeme ukiwemo wa kuzalisha umeme wa maji kwa  maporomoko ya mto Rufiji (Rufiji Hydropower Project).

Aliweka wazi kuwa,  umeme unaozalishwa kwa kutumia nguvu za maji huwa ni wa gharama nafuu na hudumu kwa miaka mingi.

Aidha, Dkt. Kalemani aliongeza kuwa,  Tanzania ina maji ambayo yanaweza kuzalisha umeme wa  zaidi ya MW 4700 ambayo bado hayajaanza kutumika.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa nne kushoto) na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ( wa Tano kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na viongozi mbalimbali kutoka mkoa wa Njombe walioshiriki mkutano huo wa wadau.

Vilevile alisema kuwa, Serikali itaendelea kuzalisha umeme kupitia vyanzo vingine ikiwemo Makaa ya Mawe, Gesi asilia, Joto ardhi, Upepo na Jua.

Kwa upande wake,  Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka alisema kuwa Wabunge watashirikiana na Serikali katika  kutoa elimu sahihi kwa wananchi ili waweze kuuelewa vyema  mradi huo kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wake.

Vile vile alitoa wito kuwa, Serikali iangalie utaratibu wa kuunda vikundi maalum vitakavyokuwa na jukumu la kulinda vyanzo maji ili kudhibiti uharibifu unaofanywa na baadhi ya watu katika vyanzo hivyo.