Tarehe 03 Aprili, 2018 Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga alifanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha mita za LUKU cha Inhemeter Tanzania Limited kilichopo jijini Dar es Salaam.

Lengo la zira hiyo lilikuwa ni kuangalia utendaji kazi wa kiwanda hicho pamoja na kutatua changamoto zilizopo katika kiwanda hicho.

Akizungumza katika ziara hiyo Mshauri Mkuu wa Kiwanda hicho, Mhadisi Dkt. Adelhelm Meru alisema  kiwanda hicho kilichoanzishwa Februari mwaka huu kina uwezo wa kuzalisha mita 500,000 kwa mwaka na kusisitiza kina uwezo kwa kuzalisha hadi mita milioni moja kulingana na mahitaji ya soko.

Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (katikati) akitoa maelekezo kwa uongozi wa kiwanda hicho. Kushoto ni Mshauri Mkuu wa Kiwanda hicho, Mhadisi Dkt. Adelhelm Meru na kulia ni Meneja Mwandamizi wa kiwanda hicho,Will Tang.

Dkt Meru aliendelea kusema kuwa, kiwanda kimeanza kuzalisha mita kidogo na kuiomba serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa miundombinu ya umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa oda za mita nyingi ili waanze kuzalisha mita nyingi za kutosha kulingana na soko.

“Mita tunazotengeneza zina ubora wa hali ya juu zenye kuendana na mazingira ya aina yoyote, tunaunga mkono juhudi za Serikali kuelekea kwenye uchumi wa viwanda kwa kusambaza vifaa kwa ajili ya wakandarasi wanaojenga miundombinu ya umeme nchini,”alisema Dkt. Meru.

Wakati huohuo Meneja Mwandamizi wa Kampuni hiyo, Will Tang aliomba Serikali kutoa kipaumbele kwa matumizi ya vifaa vya umeme vinavyotengenezwa na viwanda vya ndani ya nchi.

Naye Mhandisi Luoga aliuhakikishia uongozi wa kiwanda hicho kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaunga mkono juhudi za kiwanda hicho na kusisitiza kuwa ipo tayari kutumia bidhaa zake katika miradi ya umeme vijijini.

“Mara baada ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zenu, mnatakiwa kujiandaa kupokea oda kubwa kutoka TANESCO na REA kwa mwaka,” aliongeza Kamishna Luoga.

Alisema katika kuhamasisha Sera yake ya Uchumi wa Viwanda, Serikali ya Awamu ya Tano inatoa kipaumbele cha matumizi ya bidhaa za ndani hususan katika miradi ya umeme nchini kwa kuwa viwanda vya ndani vitaongeza mapato, ajira na hata kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa bei nafuu nchini.

Kutoka kushoto mbele Meneja Mwandamizi wa kiwanda cha kuzalisha mita za LUKU cha Inhemeter Tanzania Limited, Will Tang Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, Mshauri Mkuu wa Kiwanda hicho, Mhadisi Dkt. Adelhelm Meru na Msimamizi wa Utawala wa kiwanda hicho, Khilna Chohan wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho.

Akielezea hatua kadhaa zilizochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwenye uhamasishaji wa uwekezaji wa viwanda vya ndani, Mhandisi Luoga alieleza kuwa, Serikali imepiga marufuku uingizaji wa nguzo za umeme kutoka nje ya nchi pamoja na bidhaa nyingine zinazopatikana hapa nchini.

“Tunataka ifike mahali mita za LUKU, transfoma, nyaya na vifaa vingine vyote vya umeme vitoke ndani ya nchi tu na kukuza uchumi wa viwanda,” alisisitiza Mhandisi Luoga.

Hata hivyo Mhandisi Luoga alielekeza kampuni hiyo kukaa pamoja na Wizara, TANESCO na REA na kupanga namna ya kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme nchini.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam