Leo tarehe 10 Aprili, 2018, Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga amefanya ziara katika kampuni ya Mantrac iliyopo jijini Dar es Salaam ambapo aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Lengo la ziara yake lilikuwa ni kukagua maendeleo ya mitambo miwili ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi iliyoingizwa nchini na kampuni ya Mantrac kwa ajili ya kusimikwa kwenye kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi cha Mtwara ambapo kila mtambo una uwezo wa Megawati 2.

Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (kulia) akisalimiana na mmoja wa watendaji wa kampuni ya Mantrac, Matiko Bugumia (kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za kampuni hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam.

Akielezea  hatua iliyofikiwa ya uingizwaji wa mitambo na vifaa vyake kwa Kamishna Luoga, Meneja Miradi kutoka kampuni ya Mantrac, Ahmed Maamoun alisema kazi inayoendelea kwa sasa ni uundwaji wa mitambo pamoja na  vifaa vyake kabla ya kusafirishwa katika kituo za kuzalisha umeme cha Mtwara kwa ajili ya  usimikwaji.

Maamoun aliongeza kuwa msingi kwa ajili ya usimikaji wa mitambo husika umekamilika na kusisitiza kuwa Mantrac inafanya kazi usiku na mchana katika kuhakikisha kuwa mradi unakamilika mapema na kukabidhiwa kwa serikali

Naye Kamishna Luoga alisema kuwa, Serikali ipo tayari kushirikiana na kampuni ya Mantrac ili mradi uweze kukamilika kwa wakati na kusisitiza kuwa wananchi wa Mtwara wanahitaji umeme kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.

Alisema kuwa mahitaji ya umeme katika mkoa wa Mtwara yanazidi kuongezeka na kufafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeweka mikakati ya muda mfupi na mrefu katika kuhakikisha kuwa nishati ya uhakika na ya gharama nafuu inapatikana.

Aliendelea kusema  ununuzi wa mitambo husika ni moja ya mikakati  ya muda mfupi ya  Wizara ya Nishati katika kutatua changamoto ya upatikanaji  wa umeme wa kutosha katika mkoa wa Mtwara.

Alitaja mikakati ya muda mrefu kuwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 300 mkoani Mtwara na kituo kingine cha Somangafungu chenye uwezo wa Megawati 330 mkoani Lindi.

Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (katikati) akitoa maelekezo kwa uongozi wa Mantrac kwenye ziara hiyo.

Katika hatua nyingine Mhandisi Luoga mbali na kupongeza kampuni ya Mantrac katika utekelezaji wa mradi husika, aliitaka kampuni  kuongeza kasi  ili kuhakikisha mradi  unakamilika na kukabidhiwa kwa Serikali kabla ya mwisho wa mwezi Aprili.

“Mradi huu ni muhimu sana kwa kuwa tunahitaji wananchi wa Mtwara wapate umeme wa uhakika ndani ya kipindi cha muda mfupi, kasi inahitajika na pale mtakapokwama katika utekelezaji wa mradi msisite kuwasiliana na Serikali  ili iweze kuwasaidia,” alisisitiza Mhandisi Luoga.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam