• Waziri Kalemani asema wanakaribishwa ikiwa wana vigezo

Wawekezaji kutoka Kampuni ya Hainan Zhenrong Energy Ltd ya China wamemtembelea Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na kumweleza nia yao ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini; hususan kwenye sekta ndogo ya gesi asilia.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia), akiwa na baadhi ya wajumbe kutoka Kampuni ya Hainan Zhenrong Energy Ltd kutoka China.

Ujumbe huo kutoka China ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Li Zemng, waliwasilisha maombi husika kwa Waziri na timu yake ya wataalam kutoka wizarani na TANESCO, Aprili 11, 2018 Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Zemng alimweleza Waziri Kalemani kuwa nia yao ni kuwezesha usafirishaji wa gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini ambako bomba la gesi halifiki kwa kutumia teknolojia maalum.

“Tutatumia teknolojia maalum kuigeuza gesi asilia katika hali ya kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG), kisha tutaihifadhi katika makontena maalum na kuyasafirisha kwenda maeneo mbalimbali ambako itatumika kwa shughuli mbalimbali za maendeleo,” alifafanua Zemng.

Akijibu maombi hayo, Waziri Kalemani alisema Serikali inakaribisha wawekezaji katika sekta husika lakini akatahadharisha kuwa ni lazima wawe na vigezo stahiki.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kushoto), akizungumza na Ujumbe kutoka Kampuni ya Hainan Zhenrong Energy Ltd kutoka China. Wengine pichani ni wataalam kutoka wizarani na TANESCO.

Alitoa mwongozo kwa Kampuni hiyo kuwasilisha maombi yao rasmi kimaandishi ili yafanyiwe kazi. Aidha, aliwataka kukutana na timu ya wataalam kutoka wizarani na TANESCO ili wajadiliane kwa kina kuhusu maombi hayo ya uwekezaji ili kujiridhisha kabla ya kuwapatia jibu rasmi.

Na Veronica Simba – Dodoma