Watendaji kutoka Kampuni ya CET ya nchini China (China Electric Power Equipment and Technology) wamekutana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ili kueleza nia yao ya kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji umeme nchini.

Kikao cha Watendaji hao na Waziri wa Nishati kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam ambapo ujumbe wa kampuni hiyo uliongozwa na Makamu wa Rais, Jiang Longhua.

Longhua alieleza kuwa, kampuni hiyo imewasilisha maombi ya kujenga miundombinu ya usafirishaji umeme (kV 400) kutoka Chalinze mkoani Pwani hadi Dodoma kwa umbali wa kilometa 342 ambapo alisema kuwa kama wakikabidhiwa kazi hiyo watamaliza ujenzi ndani ya miezi 18.

Aliongeza kuwa, kampuni hiyo pia imeshawasilisha maombi kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ya kujenga miundombinu ya usafirishaji umeme (kV 400) kutoka Mbeya-Tunduma-Sumbawanga-Mpanda hadi Kigoma kwa umbali wa zaidi ya kilometa zaidi ya 500.

“Kama tukipata kazi hii, tutamaliza ndani ya muda muda wa miezi 22 tu kwani tuna uzoefu wa kujenga miundombinu hii katika nchi mbalimbali duniani na kwa Bara la Afrika tumeshajenga miundombinu hii nchini Ethiopia, ambapo tumetekeleza mradi wa urefu wa kilomita 1200 ambao tuliumaliza ndani ya miaka miwili tu,” alisema Longhua. Kwa upande wake, Waziri wa Nishati aliishukuru kampuni hiyo kwa kuonesha nia ya kuendeleza miradi ya umeme nchini na kuwasihi kuendelea kufanya hivyo kutokana na mahitaji ya umeme nchini kuendelea kuongezeka.

Aidha kuhusu maombi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya umeme ambayo kampuni hiyo imewasilisha TANESCO, alieleza kuwa, kampuni nyingi zimejitokeza ili kupata ridhaa ya kujenga miundombinu husika lakini Serikali itatoa kazi kwa kampuni itakayokidhi vigezo vilivyowekwa.