Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua amekutana na kufanya mazungumzo na watendaji wa Kampuni ya Rift Valley Energy inayotaka kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya upepo mkoani Njombe.

Dkt.Mwinyimvua alikutana na watendaji wa Kampuni hiyo tarehe 2 Machi, 2018 katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati mjini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo watendaji wa Kampuni hiyo walieleza  kuwa mbali na kutaka kuzalisha umeme wa upepo, tayari kampuni hiyo inazalisha umeme wa Megawati 4 kwa kutumia maporomoko ya maji  katika eneo Mwenga mkoani Njombe na kuusambaza kwenye vijiji 34 vinavyozunguka eneo hilo.

Aidha watendaji hao walimweleza Katibu Mkuu kuwa kampuni hiyo pia itatekeleza miradi mingine ya umeme kwa kutumia maporomoko madogo ya katika maeneo ya Luponda mkoani Njombe na Suma mkoani Mbeya.

Kwa upande wake Katibu Mkuu alieleza kuwa, Tanzania bado ina uhitaji wa umeme hivyo ni muhimu kwa kampuni hiyo kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme ili nchi iwe na umeme wa kutosha.

Na Zuena msuya Dodoma.