Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amesema kuanzia sasa kila Mkoa utakuwa ukinunua vifaa vya umeme kulingana na mahitaji ya Mkoa husika tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo vifaa hivyo vilikuwa vikinunuliwa na Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na baadaye kuambazwa mikoani pale vinapohitajika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Wizara ya Nishati, Dunstan Kitandula (kushoto) akisikiliza uwasilishwaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Wizara ya Nishati na taasisi zake.

Dkt.Kalemani alisema hayo tarehe 27/8/2018  wakati akiwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na wizara yake kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Aliieleza kuwa hatua ya kuruhusu kila Mkoa kununua vifa vyake, itaharakisha utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme katika kila Mkoa na kuondoa usumbufu wa kusubiri vifaa kwa muda mrefu kutoka TANESCO, Dar es saalam.

Aliwekawazi kuwa, vifaa hivyo ni nguzo za umeme, nyaya, transfoma pamoja na vifaa vingine vinavyotumika katika miundombinu ya usambazaji wa umeme.

Alieleza zaidi kuwa, kuanzia sasa miradi mingi ya usambazaji wa umeme itakuwa ikikamilika kwa wakati kwa kuwa kila Mkoa utakuwa ukiagiza vifaa vyake kutokana na mahitaji husika na hivyo kuendana na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini ili ifikapo  2021 kila kijiji kiwe kimepata huduma ya umeme nchini

Katika kikao hicho taarifa mbalimbali za utekelezaji zilijadiliwa ikiwemo ya  utekelezaji wa Nguzo za zege, Hatua zilizofikiwa na Serikali katika uendelezaji wa miradi ya Umeme wa Upepo pamoja na Uendelezaji wa Umeme katika maeneo yaliyo nje ya Gridi.

Akizungumzia mradi wa utekelezaji wa nguzo za Zege, Dkt. Kalemani alisema kuwa mpaka sasa tayari kampuni nne zimejitokeza kutaka kuzalisha nguzo hizo.

Kwa mujibu wa Dkt. Kalemani, TANESCO itakuwa ikisimamia ubora wa nguzo hizo na kwamba itakuwa ikizinunua kutokana na mahitaji husika.

Dkt. Kalemani alieleza kuwa katika suala la utekelezaji wa umeme kwa kutumia nguvu ya upepo, ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wanatarajia kutangaza zabuni kwa makampuni yaliyojitokeza kutaka kufanya uwekezaji huo.

Alieleza kuwa katika zabuni hiyo washindi ni wale watakaokwenda sambamba na bei elekezi iliyowekwa ambayo itatumika kuwauzia TANESCO umeme unaozalishwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula pamoja na mambo mengine aliiagiza Wizara pamoja na taasisi zake kuetekeleza miradi iliyokusudiwa hasa ule wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia upepo kwa manufaa ya watanzania na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( aliyesimama) akiwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Wizara kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

“ Wizara na Taasisi hakikisheni huu mradi wa umeme wa upepo unatekelezwa, maana umekuwa ukizungumzwa kila wakati, sasa hivi tunataka ufike mwisho,utekelezeke na uanze kunufaisha taifa”, alisisitiza Kitandula.

Aidha aliwaagiza kusimamia ipasavyo miradi yote inayotekelezwa na wizara kwa kushirikiana na tasisi zake ikiwepo utekelezaji wa nguzo za zege  ili itekelezwe kwa ubora unaotakiwa, iweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.

Pia kushirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ili waweze kuwekeza katika miradi inayotekelezwa hapa nchini ikiwepo uzalishaji wa umeme wa kutumia upepo na ule wa uzalishaji wa nguzo za zege.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya  Nishati na Madini, zitaendela na kikao kama hichi kesho kujadili masuala mbalimbali yanayohusu upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.

Na Zuwena Msuya