Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa, ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Tipper- Kigamboni unakamilika na kituo kianze kufanya kazi ifikapo mwezi Julai mwaka huu.

Dkt. Kalemani alitoa maagizo hayo tarehe 23 Machi, 2018 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea eneo ambalo kituo hicho kinajengwa na kukuta mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi.

Alisema kuwa, eneo la Kigamboni bado linakabiliwa na changamoto ya umeme ndiyo maana Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kutatua changamoto hiyo.

Aliongeza  kuwa,  licha ya kuanza kwa  ujenzi wa kituo kipya cha umeme cha Tipper-Kigamboni, Serikali ilifanya jitihada ya kuongeza kiwango cha umeme kwenye eneo hilo kwa kufunga transfoma yenye uwezo wa MVA 15 tofauti na iliyokuwepo awali, iliyokuwa na uwezo wa MVA 5 tu.

Vilevile, alisema kuwa baada ya kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha Mbagala, baadhi ya wananchi wa Kigamboni wameanza kupata umeme kutoka kituo hicho hivyo kuwapunguzia adha ya kutopata umeme wa uhakika.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kulia), pamoja watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wilaya ya Kigamboni, wakikagua eneo likalojengwa mitambo ya kupoza umeme, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Kigamboni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile.

Alisema kuwa mashine zitakazofungwa katika kituo hicho cha Tipper- Kigamboni zitakuwa na uwezo wa kuhudumia wateja wengi zaidi ya wanaohudumiwa sasa.

Ili kukamilisha ujenzi wa kituo ndani ya muda uliopangwa, aliagiza kuwa, kikosi kazi kutoka TANESCO kinachohusika na ujenzi wa miundombinu ya vituo vya kupoza umeme nchini, kiende kufanya kazi katika eneo hilo.

Vilevile, Dkt. Kalemani alitoa agizo kuwa, wateja wote wa Kigamboni waliokwishalipia huduma ya umeme na bado hawajaunganishwa na huduma ya hiyo, wawe wameunganishiwa ndani ya mwezi mmoja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigamboni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile, alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kuendelea kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi wa Jimbo hilo  na kueleza kuwa baada ya kituo cha kupoza umeme cha Mbagala kukamilika, baadhi ya wananchi wameanza kupata umeme wa uhakika.

Kuhusu ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Tipper-Kigamboni, alishauri kuwa uende sambamba na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme ili kutochelewesha mradi huo.

Aidha alieleza kuwa, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa nguzo na nyaya katika Jimbo hilo hivyo aliomba suala hilo pia lipewe kipaumbele katika kushughulikiwa.

Na Teresia Mhagama