Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa kata za Kigamboni, Vijibweni, Tungi zinatarajiwa kupata umeme wa uhakika  kufuatia kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kigamboni kilichopo jijini Dar es Salaam.

Waziri Mgalu aliyasema hayo tarehe 27 Novemba, 2017 kwenye ziara yake katika kituo cha kupoza umeme Kigamboni na katika mikutano ya hadhara aliyoifanya katika kata za Kisiju na Mkamba zilizopo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wateja kutoka 6,000 hadi 12,000 na kuongeza kuwa Serikali kupitia  Wizara ya Nishati  itahakikisha  vituo vingine vya kuboresha  hali ya umeme ndani ya jiji la  Dar es Salaam  vinakamilika mapema Desemba 15, 2017 na kuondoa  tatizo la  kukatika kwa umeme mara kwa mara lililokuwa linajitokeza.

Mzimamizi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Kigamboni kilichopo jijini Dar es Salaam, Sylvester Sikare (kulia) akielezea maendeleo ya ukamilishaji wa kituo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) mara alipofanya ziara katika kituo hicho tarehe 27 Novemba, 2017

Aidha, alilitaka  Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) kukamilisha vituo  vingine  vilivyobaki vya Kurasini, Gongo la Mboto na Mbagala mapema ili wakazi wa jiji la Dar es Salaam waweze kuondokana na  tatizo la ukosefu wa umeme.

Katika hatua nyingine, Mgalu aliwataka wandarasi waliopewa kazi ya kujenga miundombinu ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukamilisha miradi mapema na kuongeza kuwa Serikali haitamvumilia mkandarasi atakayezembea ukamilishwaji wa mradi wake.

“ Wananchi wanahitaji umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, umeme ndio uchumi wa nchi na kama Wizara ya Nishati  tupo kwa ajili ya kuhakikisha  uchumi  wa viwanda unakua kwa kuhakikisha nishati ya umeme ya uhakika inapatikana sehemu zote hasa vijijini,” alisisitiza  Mgalu

Vilevile, Mgalu aliitaka REA kuainisha vipaumbele katika usambazaji wa umeme vijijini, kipaumbele kikiwa ni vijiji vyenye wakazi wengi na taasisi kama hospitali, makanisa na misikiti.

Akizungumzia suala la fidia kwa wakazi wanaopisha  ujenzi wa miundombiniu ya umeme unaosimamiwa na  REA, Naibu Waziri Mgalu alisema hakuna fidia kwa kuwa serikali imekwishagharamia gharama zote na kinachohitajika kwa wananchi ni kulipia gharama za Kodi (VAT) ambayo ni shilingi 27,000.

Aliwataka wakazi wa Kata za Kisiju na Mkamba wilayani Mkuranga kutandaza mifumo ya nyaya (wiring) kwenye nyumba zao au kununua kifaa maalum cha Umeme Tayari (UMETA) mapema kwa ajili ya kujiandaa na huduma ya umeme.

Akielezea mikakati ya Serikali katika kuhakikisha umeme unapatikana hususan katika wilaya ya Mkuranga yenye viwanda vingi, Naibu Waziri Mgalu alisema Serikali inatarajia kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi Somanga Fungu na kusambaza gesi nyingine kwenye viwanda vitakavyohitaji.

Aliongeza kuwa Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Stieglers Gorge utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,100 na kukamilisha miradi ya Kinyerezi II na Kinyerezi III

Alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 Megawati 5,000 zinapatikana na nchi kuingia kwenye uchumi wa viwanda utakaozalisha ajira kwa vijana hususan kwa vijana waishio vijijini.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Kigamboni, Mhandisi Richard Swai (kushoto mbele) akieleza jambo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) katika ziara hiyo.

“Tunataka mazao yasindikwe vijijini na kusafirishwa ndani na nje ya nchi yakiwa kama bidhaa, tunataka mtumie fursa ya umeme kwa ajili ya uchumi wa viwanda badala ya matumizi ya majumbani tu,” alisema Mgalu.

Naye Mbunge wa Mkuranga ambaye ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega alimshukuru Naibu Waziri Mgalu kwa ziara yake katika wilaya ya Mkuranga na kuongeza kuwa wananchi wana matumaini makubwa ya umeme wa uhakika kwani wilaya  hiyo imekuwa na changamoto ya ukosefu wa umeme kwa muda mrefu.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam