Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa kuanzia Septemba Mosi, nguzo yoyote itakayoharibika na kuanguka katika eneo lolote nchini, mbadala wake iweke nguzo ya zege na si kurudishia nguzo ya mti tena.

Dkt. Kalemani alisema hayo, June 7, 2020, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini pamoja na kuwasha umeme katika Vijiji vya Hunyali wilayani Bunda, Bukoba wilayani Musoma na Kerukerege wilayani Serengeti mkoani Mara.

Alisema kuwa nguzo za zege zinakaa zaidi ya miaka mia moja, hivyo kwa kutumia njia hiyo kutapunguza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara kwa kisingizo cha kubadilisha nguzo katika baadhi ya maeneo hasa yalioyopo katika ardhi yenye maji mengi, na pia katika maeneo yanayochomwa moto kila wakati na kusababisha nguzo kuungua.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (pili kushoto),Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Msafiri Mtemi (kushoto), kwa niaba ya mkuu wilaya Serengeti na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati( pili kulia) wakimsikiliza Diwani wa Kijiji cha Kerukerege( hayupo pichani)wilayani humo, wakati wa ziara ya Waziri huyo ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika Mkoa wa Mara Juni 7,2020.

“Sasa hivi umeme haukatiki, na hakuna sababu ya kukatika kwa kuwa umeme upo mwingi na ziada, lakini kuna baadhi ya maeneo wamekuwa wakikata umeme mara kwa mara kwa kisingizio cha kubadilisha nguzo hasa maeneo korofi, sasa tunaweka za zege hizi haziungui wala kuoza na kuanguka, hii ndiyo dawa pekee ya kuweka nguzo imara kumaliza tatizo hilo”, Alisema Dkt, Kalemani.

Kuhusu upatikanaji wa umeme katika visiwa vilivyopo katika ukanda wa ziwa Viktoria, Dkt. Kalemani alisema kuwa visima vyote vitapelekewa umeme kwa kupitisha nyaya chini ya maji( underground cable) na tayari wameshaaza kupeleka katika kisiwa cha Ukerewe, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Amewatoa hofu wakazi wa maeneo hayo kuwa hawajasaulika na serikali iko katika hatua nzuri za kuendelea na utekelezaji wa kazi hiyo katika kila kisiwa, hivyo wawe wavumilivu kwa kuwa tayari tafiti zimefanyika na kiasi cha fedha kinachohitajika kinafamika kinachosubiriwa sasa ni kuanza kwa utekelezaji wake.

“Visiwa vyote vinapelekewa umeme wa kupitia njia ya underground cable tayari tumeanza katika kisiwa cha Ukerewe, tutafika visiwa vyote vya Tanzania, tumeachana na kupitisha mawaya ambayo wakati mwingine yalikuwa yanakatwa na wavuvi na changamoto zingine, huu ni mkakati madhubuti wa kuhakikisha kuwa visiwa vyote vinatumia umeme huu tunaouzalisha nchini na inawezekana, wananchi wa maneo hayo vumilieni kidogo, kazi inafanyika”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Aliendelea kuwasisitiza wananchi wasisubiri nguzo bali waendelea kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi elfu 27,000 tu, pia wasikubali kuuziwa nguo, mita za LUKU wala nyaya, na pia watumie wakandarasi walioidhinishwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kutandaza nyaya katika nyumba zao ili kuepuka vishoka na watu wasiowaaminifu.

Alisema kuwa baada ya zoezi la kuwafikisha umeme katika kila kijiji,zoezi litakalofuata ni kufanya msako wa kukagua kaya ambazo hazijaunganishwa na umeme, na kaya itakayobainika kwa kutokuungashiwa umeme mali zake kama mbuzi,kuku, mbwa na kadhalika vitapigwa mnada ili kupatikana shilingi 27,000 ya kuunganisha umeme katika nyumba husika.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani(kulia)na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alipofika kuwasha umeme katika Kijiji cha Bukoba Wilayani Musoma Mkoani humo wakati wa ziara yake ya kukagua maeneo ya usambazaji wa umeme katika mkoa huo, Juni 7,2020.

Wakiwa Katika ziara hiyo na kuwasha umeme katika shule ya msingi Bunyunyi, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Zena Said walifanya harambee ya kuchangia mashine ya kutoa Nakala Kivuli( Photocopy)katika shule hiyo iliyopo wilayani Bunda mkoani Mara baada ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuomba msaada wa mashine hiyo kwa viongozi hao.

Viongozi hao walifanya harambee na kupata fedha za kuunua mashine kubwa ya gharama kubwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi ikilinganishwa na mashine aliyoiomba mwalimu huyo ama kutaka kutengenezewa ile iliyoharibika.

Baada ya viongozi hao kueleza nia yao ya kufanya harambee hiyo katika mkutano wa Waziri wa Nishati ili kumsaidia Mwalimu mkuu huyo ambaye pia alikuwa ni mwanamama, Dkt. Kalemani aliwaunga mkono akimama hao  kwa kuchangia kiasi cha fedha na kuchukuwa jukumu la kuongoza harambee kwa kuwabana akina Baba waliofika katika mkutano huo na wale alioambatana nao katika ziara yake.

“Akina mama ni wajanja sana jamani na wanaumoja kwelikweli,muda mchache tuu huu waliofika hapa wameshanong’onezana na wakajua hitaji la mwenzao na wanataka fedha kulimaliza, sasa na sisi(akinababa) hatubaki nyuma tunawaonyesha kuwa sisi ndiyo tuko mstari wa mbele kuwasaidia wao tunachangia fedha nyingi kuliko wao ili wapate mashine kubwa zaidi ya walioitaka, haya naanza na wewe Mbunge Getele unachangia ngapi sipokei chini ya shilingi elfu 50,000 kwa mliokaa meza kuu, mimi ni wa mwisho kuchangia!”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Zena Said( kushoto) wakichangia fedha za kununua mashine ya kutoa nakala kivuli (Photocopy) kwa ajili ya shule ya msingi Hunyanyu,katika kijiji cha Hunyali wilayani Bunda Mkoani Mara, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini na kuwasha umeme katika baadhi ya vijiji vya mkoa huo, Juni 7,2020.

Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni moja ilipatika ambayo itanunua mashine ya kutoa nakala kivuli (Photocopy) yenye thamani ya shilingi laki tisa ( 900,000).

Wanakijiji hao waliwampatia Waziri Dkt. Kalemani na Naibu Waziri Mgalu zawadi ya Kondoo,pia Katibu Mkuu Mhandisi Said alipewa zawadi ya Mbuzi.

Ziara hiyo ilishia katika kijiji cha Kerukerege, wilayani Serengeti Mkoani Mara, ambapo baada ya kuwasha umeme katika kijiji hicho pamoja na mambo mengine, wakazi wa kijiji hicho walimsimika Waziri wa Nishati Dkt. Kalemani kuwa Chifu wa eneo hilo na kumpa jina na Dkt. Chacha Remu Kalemani pamoja na kumakabidhi Ng’ombe wawili, mmoj akiwa wakwake na mwingine ampelekee Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Sambamba na hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said , alipewa jina la Rhobi Kerongwe ikiwa ni heshma ya jina la mwanamke wa kwanza katika jamii hiyo pamoja na kumkabidhi mbuzi, walifanya hivyo ikiwa ni furaha yao kwa kuwa hao ni viongozi wa kwanza kufika katika eneo hilo tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho.

Na Zuena Msuya, Mara