Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza serikali kuunganisha gesi asilia katika viwanda mbalimbali nchini jambo ambalo limesaidia kupunguza gharama za uendeshaji.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Vedastus Mathayo, ametoa pongezi hizo leo, Machi 17, 2020 baada ya Wajumbe wa Kamati kutembelea Kiwanda cha kufua vyuma cha Lodhia, kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kwa lengo la kujionea manufaa yaliyopatikana kutokana na matumizi ya gesi asilia.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa katika ziara iliyolenga kujionea matumizi ya gesi asilia katika kiwanda cha kufua vyuma cha Lodhia kilichopo Mkuranga mkoani Pwani, Machi 17 mwaka huu.

“Kama Kamati, tumefurahishwa sana na mafanikio yaliyopatikana baada ya kiwanda hiki kuunganishiwa mtandao wa gesi asilia na tunaipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Nishati,” amesema Mathayo.

Pamoja na pongezi hizo, Kamati imeishauri serikali kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme ambayo itasaidia upatikanaji wa nishati hiyo kwa wingi hivyo kuwezesha gharama yake kupungua na hivyo kuwawezesha wawekezaji katika viwanda kuzalisha kwa tija zaidi.

Akitoa maelezo ya serikali kutokana na maelekezo hayo yaliyotolewa na Kamati, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, ambaye alimwakilisha Waziri mwenye dhamana, Dkt Medard Kalemani, alisema Serikali itahakikisha inaendelea kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme ili kuwezesha upatikanaji wa umeme mwingi na wa uhakika wenye gharama nafuu.

“Tuna matumaini kwamba kukamilika kwa miradi mikubwa, ukiwemo wa Julius Nyerere (MW 2,115) kutawezesha kushuka gharama za umeme kwa kiasi kikubwa.”

Awali, akiwasilisha taarifa ya kiwanda hicho mbele ya Wajumbe wa Kamati, Meneja Rasilimaliwatu, Martin Mkange alisema kupatikana kwa gesi asilia kumewasaidia pamoja na mambo mengine kuondokana na matumizi ya mafuta mazito ambayo yalikuwa na gharama kubwa katika uendeshaji.

Sehemu ya shehena ya vyuma ambavyo vimetengenezwa na kiwanda cha Lodhia kilichopo Mkuranga mkoani Pwani. Taswira hii ilichukuliwa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani) kiwandani hapo, Machi 17 mwaka huu, kwa lengo la kujionea matumizi ya gesi asilia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa Kamati, Kiwanda cha Lodhia kinatumia gesi asilia kiasi cha wastani wa futi za ujazo milioni 0.1 hadi 0.2 kwa siku, sawa na makusanyo ya zaidi ya shilingi milioni 70 kwa mwezi.

Taarifa inaeleza zaidi kuwa kiwanda hicho kilianza kutumia gesi asilia mwezi Juni, 2019.

Miradi ya usambazaji gesi asilia nchini inaendelea kutekelezwa katika maeneo ambayo tayari kuna miundombinu wezeshi ikihusisha mikoa ya awali ya Pwani na Dar es Salaam.

Veronica Simba – Dar es Salaam