• Timu ya Wataalam yaundwa kuanza kazi za awali utekelezaji mradi

Na Zuena Msuya, Njombe.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja ameongoza timu ya Wataalam iliyoundwa kutoka Wizara ya Nishati pamoja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukagua eneo kutakapojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto Ruhudji.

Timu hiyo iliundwa mahsusi kwa ajili ya kusimamia kazi za awali kabla ya kuanza rasmi za ujenzi wa mradi huo, ambapo timu hiyo itashirikisha Taasisi na Wizara mbalimbali.

Muonekano wa sehemu moja ya eneo la Mto Ruhudji ambalo limegawanyika mara mbili katika eneo moja, utakapojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto huo. Eneo hilo lipo kati ya Kijiji cha Itipula na Lupembe, wilayani Njombe, mkoani Njombe.

Ziara hiyo ilifanyika Januari 12,2021, ikiwa na lengo la kukagua na kuona jiografia ya eneo husika lililopo kati ya Kijiji cha Itipula na Lupembe, wilayani Njombe mkoani Njombe.

Kwa mujibu wa Mhandisi Masanja, mradi huo unatarajiwa kuzalisha takribani megawati 358 ambazo zitaingizwa katika gridi ya Taifa pindi mradi huo utakapokamilika.

Katika mujibu wa mipango ya Serikali, mradi huo utaanza kujengwa mwezi Julai 2021 na utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 36.

Mhandisi Masanja, amewatoa hofu watanzania kuwa, endapo mradi huo utalazimika kuchukua baadhi ya maeneo ya wakazi wanaozunguka eneo la mradi, sheria na taratibu za nchi zitafuata ili kila mmoja apate haki yake ikiwemo kulipwa fidia.

“Mradi huu ni muhimu sana kwetu na umekuja wakati sahihi kwa kuzingatia uchumi wa viwanda, kwani utaongeza kasi ya uwekezaji katika ujenzi viwanda vipya, kuongeza na kuboresha uzalishaji wa katika viwanda vilivyopo sasa, vilevile kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuwa na umeme mwingi, wa uhakika, wa kutosha na wa gharama nafuu nchi nzima.”Alisema Mhandisi Masanja

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakati walipofanya ziara ya kukagua na kuona jiografia ya eneo litakalojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Ruhudji, lililopo kati ya Kijiji cha Itipula na Lupembe, wilayani Njombe, mkoani Njombe, Januari 12, 2021.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka alisema kuwa, Shirika hilo limeupokea mradi huo, na kwamba wako tayari kuanza utekelezaji wa ujenzi wake kulingana na taratibu na miongozo ya Serikali.

Vilevile, alisema kwa kuwa TANESCO ndiyo msimamizi mkuu wa miradi ya umeme nchini, watahakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo kuanzia hatua za awali na kuhakikisha kuwa unakamilika kwa wakati uliopangwa.

“TANESCO tunauzoefu katika kutekeleza miradi mikubwa na midogo ya kuzalisha umeme ikiwepo ya Maji, kama vile Mtera, Kidatu, Kihansi na huu mwingine mkubwa kabisa wa Julius Nyerere, niwatoe hofu watanzania kuwa mradi huu, utakamilika kwa wakati, na endapo kuna maeneo ya watu katika eneo la kuzunguka mradi sheria na kanuni za nchi zitafuata ili kila mmoja aweze kupata haki yake.” Alisisitiza Dkt. Mwinuka

Ikumbukwe kuwa Januari 8, 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya nje ya China, Wang Yi, kuhusu miradi hiyo.

Mazungumzo yao pamoja na mambo mengine, Rais Dkt. Magufuli aliomba ufadhili kutoka Serikali ya China wa ujenzi wa miradi hiyo miwili ya kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto Ruhudji na Rumakali.