Katibu Mkuu Mpya wa Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said, ametoa hamasa kwa watumishi wa Wizara husika na Taasisi zake, kuwatumia viongozi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kuwafikishia huduma wananchi.

Amesema kuwa kwa kuwatumia Wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wa Halmashauri, kutaleta matokeo chanya kwani wao hushughulika moja kwa moja na wananchi kuanzia ngazi ya chini kabisa, hivyo wanatambua namna bora zaidi ya kuwafikia.

Kutoka kulia ni Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja na Katibu Mkuu mstaafu, Dkt Hamisi Mwinyimvua, wakifurahia jambo muda mfupi kabla ya makabidhiano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika Februari 7, 2020, Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma.

Mhandisi Zena aliyasema hayo Februari 7, 2020 wakati akizungumza na Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini yake, muda mfupi baada ya kukabidhiwa rasmi Ofisi na mtangulizi wake, Dkt Hamisi Mwinyimvua.

Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said (mbele-katikati), Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Leonard Masanja (mbele-kulia) na Katibu Mkuu mstaafu, Dkt Hamisi Mwinyimvua (mbele-kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini yake, mara baada ya makabidhiano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika Februari 7, 2020 katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma.

“Tunahitaji kutumia muundo uliopo wa Serikali Kuu na zile za Mitaa ambazo watu wanalipwa lakini bado hawatumiki vizuri.  Chochote tutakachofanya kama Wizara, tukitumia Serikali za Mitaa katika kufanya kampeni za uelimishaji, itatusaidia sana,” alieleza.

Akifafanua zaidi, Katibu Mkuu aliwaeleza viongozi hao kuwa, siyo jambo la busara kufanya kazi kwa kujitenga kwani itakuwa ngumu lakini kwa kuwatumia watendaji husika itawasaidia kurahisisha kazi.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu alisisitiza umuhimu na ulazima wa watumishi wote kuzingatia kanuni, sheria na taratibu mbalimbali zilizowekwa ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na hivyo kila mmoja kwa nafasi yake kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli katika kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Aidha, alihimiza utendaji kazi jumuishi yaani kama timu moja huku akitahadharisha kuwa, mmojawao akiharibu kazi kwa kutowajibika, atakuwa ameiangusha Wizara nzima.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wafanyakazi wa wizara, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Leonard Masanja, alimpongeza na kumshukuru Katibu Mkuu mstaafu Dkt Mwinyimvua kwa utendaji kazi mahiri na kuahidi ushirikiano kwa Katibu Mkuu mpya, Mhandisi Zena.

“Dkt Mwinyimvua, tunaamini Ofisi hii umeiacha katika mikono salama ya Mhandisi Zena. Mimi binafsi pamoja na watumishi wenzangu, tunaahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.”

Awali, akizungumza kabla ya kukabidhi Ofisi, Katibu Mkuu mstaafu Dkt Mwinyimvua aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa watendaji wote wa Wizara wakati wowote watakapomuhitaji.

Mhandisi Zena Said na Mhandisi Leonard Masanja, waliteuliwa na kuapishwa na Rais John Magufuli, Februari 3, mwaka huu katika nafasi ya Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. Kabla ya uteuzi, Mhandisi Zena alikuwa ni Katibu Tawala Mkoa wa Tanga na Mhandisi Masanja alikuwa ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati.

Veronica Simba – Dodoma