Waziri wa Nishati,  Dkt Medard Kalemani amemtaka Katibu Mkuu mpya, Mhandisi Zena Said, kulipa kipaumbele suala la kukutana na watumishi wa Wizara pamoja na Taasisi zake, ili kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema, kwa kufanya hivyo itasaidia kuwajengea watumishi hao utulivu wa kisaikolojia hivyo watatekeleza majukumu yao ya kuwahudumia watanzania kwa ufanisi zaidi.

Baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati wakiwa katika kikao maalum cha kuwakaribisha viongozi wapya ambao ni Katibu Mkuu Mhandisi Zena Said na Naibu wake, Mhandisi Leonard Masanja. Kikao hicho kilifanyika Februari 7, 2020 Makao Makuu ya Wizara, Mtumba Dodoma.

Alikuwa akizungumza katika kikao maalum cha viongozi na watumishi wa Wizara, kilicholenga kumkaribisha rasmi Katibu Mkuu mpya pamoja na Naibu wake, Mhandisi Leonard Masanja, kilichofanyika Februari 7, 2020 Makao Makuu ya Wizara, Mtumba Dodoma.

“Simaanishi kwamba changamoto za watumishi zilikuwa hazishughulikiwi, la hasha, lakini kila mtu ana namna yake ya utekelezaji. Hayo ndiyo maelekezo yangu kwako,” alisema Waziri.

Akifafanua, Dkt Kalemani alisema kuwa changamoto kwa watumishi ni jambo la kawaida mahala pa kazi lakini ni muhimu kuzitatua kwa wakati, kwani zinapoachwa kwa muda mrefu husababisha utendaji mbovu unaozorotesha utoaji huduma kwa wananchi na kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Waziri alimtaka Katibu Mkuu kutumia uzoefu wake katika masuala ya manunuzi ili aisaidie Wizara katika eneo hilo na kuiepusha na migogoro ya aina hiyo ambayo hutokea katika mashirika na taasisi mbalimbali za serikali.

“Tusaidie kusimamia na kutatua mapema ili isitokee migogoro ambayo itatupotezea muda wa kuwahudumia wananchi. Unapotumia muda mwingi kushughulikia migogoro unakosa muda wa kufanya mambo ya msingi kama kupeleka umeme kwa wananchi hivyo kurudisha nyuma jitihada za Serikali.”

Vilevile, Waziri alimwelekeza Katibu Mkuu kusimamia miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Wizara kwani inalenga kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha kunakuwepo na nishati ya uhakika na yenye gharama nafuu huku akisisitiza kwamba sekta ya nishati imebeba dhamana kubwa kwa wananchi maana inagusa maisha yao moja kwa moja.

Baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati wakiwa katika kikao maalum cha kuwakaribisha viongozi wapya ambao ni Katibu Mkuu Mhandisi Zena Said na Naibu wake, Mhandisi Leonard Masanja. Kikao hicho kilifanyika Februari 7, 2020 Makao Makuu ya Wizara, Mtumba Dodoma.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Pamoja na maelekezo hayo kwa Katibu Mkuu mpya, Waziri alieleza wazi kuwa Wizara ina imani na matumaini makubwa kwake kutokana na historia yake ya utendaji kazi katika sehemu zote alikopita.

Sambamba na hilo, alimpongeza Naibu Katibu Mkuu Masanja na kumwelezea kuwa ni mfano wa kuigwa kutokana na utendaji kazi wake mahiri aliouonesha akiwa mtumishi wa Wizara husika kwa nafasi mbalimbali.

Alimtaka kushirikiana na Katibu Mkuu pamoja na viongozi wengine katika kuwaongoza watumishi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, pamoja na kuwapongeza Katibu Mkuu na Naibu wake, alitoa shukrani kwa Rais John Pombe Magufuli kwa uteuzi alioufanya ambao alisema umeipatia Wizara ya Nishati viongozi makini na wachapa kazi.

“Binafsi nafurahi zaidi kwani uteuzi umewezesha kuleta uwiano wa kijinsia (50/50) ambapo suala hili liko katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Waziri na Naibu Waziri walimpongeza Katibu Mkuu aliyestaafu, Dkt Hamisi Mwinyimvua kwa utendaji kazi mzuri ambao umeiwezesha Wizara ya Nishati kufanya vizuri katika kutekeleza miradi mbalimbali.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu mpya, alishukuru kwa mapokezi mazuri lakini akaahidi kufanya kazi kwa bidii na pia akaomba ushirikiano kutoka kwa viongozi na watumishi wote wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.

“Naamini uzoefu nilioupata katika utumishi wa umma na sehemu nyingine mbalimbali nilizofanya kazi, utanisaidia kutekeleza majukumu yangu kama Katibu Mkuu pasipo shaka yoyote.”

Alikiri kuwa Wizara ya Nishati inategemewa na wananchi kwa sababu inagusa maisha yao. Aliahidi kuendeleza pale mtangulizi wake alipoishia kwa kushughulikia malengo ya Wizara na Serikali kwa ujumla, ambayo ni pamoja na kupeleka umeme vijijini.

“Hadi sasa tumefanya vizuri lakini naamini tunaweza kufanya vizuri zaidi,” alisema.

Katibu Mkuu mpya na Naibu Katibu Mkuu, waliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli hivi karibuni na kuapishwa Februari 3, mwaka huu.

Na Veronica Simba