Serikali imeuagiza uongozi wa juu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza mara moja ujenzi wa maboresho ya kituo cha kupoza umeme kilichopo Mlandizi, wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, ili kukiongezea uwezo.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, aliyetembelea kituo hicho akiwa katika ziara ya kazi mkoani Pwani, Februari 2, 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara yake kituoni hapo, Waziri Kalemani alisema ililenga kujionea hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa maboresho husika pamoja na kujiridhisha kuhusu malalamiko ya wananchi kuwa umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara na nyakati nyingine unakuwa mdogo usio na nguvu.

“Nashukuru jitihada zimeshaanza za kuagiza vifaa na mashine nyingine zinazohusika. Nimewaagiza TANESCO ujenzi huo uanze kesho (Februari 3) na siyo wiki ijayo kama walivyokuwa wamepanga,” alisema.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhusu uboreshaji wa kituo cha kufua umeme Mlandizi ili kukiongezea uwezo, akiwa katika ziara ya kazi mkoani Pwani, Februari 2, 2020.

Akifafanua zaidi kuhusu uboreshaji kituo hicho, Dkt Kalemani alisema unahusisha kufunga mashine mpya yenye uwezo wa megawati 48 za umeme.

Alisema uwezo wa sasa wa kituo hicho ni megawati 48 za umeme, hivyo baada ya uboreshaji wake, zitaongezeka megawati nyingine 48 hivyo kitakuwa na uwezo wa megawati 96.

Waziri alisema, lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanaopata huduma ya umeme kupitia kituo hicho wanakuwa na umeme wa uhakika muda wote.

“Kwetu sisi TANESCO na Wizara, tumejipanga kila kituo cha kupoza umeme kiwe na ziada ya megawati zisizopungua 50. Kwa hivi sasa kituo hiki kina ziada ya megawati nane katika matumizi, hivyo muda wowote kinaweza kuzidiwa. Tumeona tuchukue tahadhari mapema,” alieleza Waziri.

Akizungumzia suala la kukatika umeme mara kwa mara, Waziri Kalemani aliwataka wananchi kuondoa hofu kwani tayari limeshatatuliwa kwa kurekebisha kikata umeme (circuit breaker) ambacho kiliharibika na kufunga kingine kipya.

Hata hivyo, alisema amewaagiza watendaji wa TANESCO kuhakikisha kunakuwa na hifadhi ya vifaa hivyo katika kila kituo cha kupoza umeme nchini, ili kinapoharibika, warekebishe mara moja na kuwaondolea adha wananchi kukaa muda mrefu wakisubiri kifaa kingine kiagizwe na kufungwa.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chasimba, kilichopo Kata ya Yombo, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani alipokuwa katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani humo, Februari 2, 2020.

Awali, katika ziara hiyo, Waziri Kalemani alitembelea kijiji cha Sanzale B, Kata ya Magomeni, wilayani Bagamoyo ambapo aliwasha umeme katika nyumba ya ibada (msikiti) na kuzungumza na wananchi.

Pia, alitembelea kijiji cha Chasimba, Kata ya Yombo, wilayani Bagamoyo, ambapo alilazimika kuchukua hatua kwa wasimamizi mbalimbali wa mradi wau meme wa ‘Peri-Urban’ unaoendelea katika eneo hilo kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Waziri aliagiza askari wamkamate mkandarasi anayetekeleza mradi huo, ili wakamhoji ni kwanini hatekelezi mradi ipasavyo ambapo tangu mwezi Agosti mwaka jana (2019), hajafanya kitu chochote na amebaikiwa na miezi mitatu tu anayotakiwa kukamilisha mradi.

Sambamba na agizo hilo, pia alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha mradi huo ndani ya muda aliopewa kwani serikali haitamwongezea muda.

Pia, aliwaagiza viongozi wa TANESCO kumwondoa aliyekuwa msimamizi wa mradi huo na kumweka mwingine kwani nao hawakutimiza wajibu wao ipasavyo.

Veronica Simba – Pwani