KUWA NA UMEME WA KUTOSHA HAKUMAANISHI TUSIWEKEZE ZAIDI – WAZIRI KALEMANI

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amesema kwa sasa Tanzania ina umeme mwingi kiasi cha kuwa na ziada ya takribani megawati 300 kwa siku; lakini amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika sekta husika na kuzalisha umeme mwingi zaidi.

Aliyasema hayo, Septemba 25, 2019 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Warsha na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wajiolojia Tanzania, uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa kwanza – kulia) na Ujumbe wake, akifafanua jambo kwa wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), alipokuwa akikagua mabanda ya maonesho ya taasisi mbalimbali, baada ya kufungua Warsha ya Wajiolojia nchini, iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Septemba 25, 2019.

Alisema hali ya nishati nchini inaendelea kuimarika kiuzalishaji umeme, kimiundombinu na kiusambazaji.

Akifafanua, Waziri Kalemani alisema kuna nishati ya kutosha kwa sasa kwenye gridi ya Taifa; ambayo inafikia megawati 1,600 za umeme wakati matumizi ya nchi hayajafikia megawati 1,100 kwa siku.

“Walau kila siku tuna ziada ya megawati 300 hadi 370,” amesema.

Hata hivyo, Waziri alisema kuwa, pamoja na kuwa na umeme huo unaotosheleza mahitaji ya nchi kwa sasa, haimaanishi serikali isiwekeze na kuzalisha umeme zaidi.

Alimpongeza Rais John Magufuli kwa kuamua kutekeleza mradi mkubwa wa kuzalisha umeme  wa maji wa Julius Nyerere huko Rufiji na kueleza kwamba utakapokamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu, nchi itakuwa na umeme mwingi zaidi, wa uhakika na wenye gharama nafuu.

Akizungumzia upande wa gesi asilia, Waziri alisema hadi sasa kiasi kilichogunduliwa nchini ni futi za ujazo trilioni 57.54 ambazo zinazalisha zaidi ya asilimia 55 ya umeme tulionao nchini.

Aidha, alisema gesi hiyo inatumika pia kuunganisha majumbani na kwenye viwanda, ambapo zoezi linaendelea katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Lindi na kwamba mikoa mingine pia itafikiwa.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati-waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Warsha ya Wajiolojia Tanzania, baada ya ufunguzi wake, Septemba 25, 2019 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Vilevile, alieleza kuwa, gesi husika imekwishaanza kutumika katika magari ambapo hadi sasa idadi imefikia takribani 250.

Waziri alisema mafanikio hayo katika sekta ya nishati yamechangiwa pia na Wajiolojia wazalendo ambao wamekuwa wakishiriki katika kazi mbalimbali za utafutaji wa mafuta na gesi; hivyo amewataka kuendelea kujituma zaidi katika kuitumikia nchi.

Kwa upande mwingine, alisema mafanikio hayo katika sekta ya nishati, yamesaidia kujenga mazingira wezeshi ya kiuwekezaji katika sekta ya madini, kwani pasipo nishati hakuna maendeleo.

Warsha hiyo ya Wajiolojia inafanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja huo tangu uanzishwe. Wajiolojia kutoka Wizara ya Nishati ni miongoni mwa washiriki.

Na Veronica Simba