Miundombinu ya umeme itayojengwa ili kutekeleza miradi ya kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto Ruhudji na Rumakali itawanufaisha kwanza wakazi wa vijiji vitakavyopitiwa na miundombinu hiyo.

Hayo yameleezwa na Meneja Mwandamizi Uwekezaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Costa Rubagumiya wakati wa ziara ya Timu ya Wataalam iliyoundwa kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO kwa ajili ya kusimamia kazi za awali katika kutekeleza miradi ya kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rumakali uliopo kati ya Kijiji cha Madiani na Lumage, wilayani Njombe mkoani Njombe, iliyofanyika Januari 13,2021.

Meneja Msimamizi wa Miradi ya Kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rumakali na Ruhudji, kutoka TANESCO, Toto Zedekia, akitoa maelezo kwa Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO iliyokagua eneo hilo litakalojengwa mradi wa kuzalisha umeme wa Rumakali uliopo kati ya Kijiji cha Madiani na Lumage, wilayani Makete, mkoani Njombe.

Mhandisi Rubagumiya alisema kuwa, kabla ya kuanza kutekeleza mradi huo, lazima miundombinu muhimu kama vile umeme, barabara na maji iwepo katika eneo la mradi kwa ajili ya kutekeleza mradi husika.

“Lazima tufikishe umeme katika eneo la mradi, umeme huu utatumika kufanya kazi mbalimbali wakati wa utekelezaji wa mradi huo, kama mnavyofahamu katika ujenzi wa miradi kuna kazi nyingi zinafanyika usiku na mchana, sasa bila kuwa na umeme hatuwezi kufanya kazi hizo kwa ufanisi, vilevile miundombinu ya barabara lazima iwepo ili kuwezasha wahusika kufika kwa urahisi eneo la mradi pamoja na vifaa vinayohitajika, sasa miundombinu hii itapita katika vijiji mbalimbali hadi kufika eneo la mradi, hivyo vijiji hivyo vyote vitanufaika na miundombinu hiyo.”Alisema Mhandisi Rubagumiya

Aidha, Rubagumiya aliwataka wakazi wanaoishi pembenzoni mwa miradi hiyo na hata waliopitiwa na miundombinu ya umeme hadi eneo la mradi, kuhakikisha kuwa, wanalinda miundombinu hiyo na kutoa ushirikiano kwa watakaokuwa wanatekeleza miradi hiyo kwa kuwa itawanufaisha watanzania wote.

Mradi wa kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rumakali utajengwa kati ya Kijiji cha Madiani na Lumage, wilayani Makete, mkoani Njombe na unatarajiwa kuzalisha takribani megawati 222 ambazo zitaingizwa katika Gridi ya Taifa pindi mradi huo utakapokamilika.

Aidha, mradi wa kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Ruhudji utajengwa kati ya Kijiji cha Itipula na Lupembe, wilayani Njombe, mkoani na unatarajiwa kuzalisha takribani Megawati 358 ambazo zitaingizwa katika Gridi ya Taifa pindi mradi huo utakapokamilika.

Ikumbukwe kuwa, Januari 8, 2021, Rais Dkt. John Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya nje ya China, Wang Yi, ambaye alifanya ziara hapa nchini.

Katika mazungumzo yao pamoja na mambo mengine, Rais Dkt. Magufuli aliomba ufadhili kutoka Serikali ya China wa ujenzi wa miradi miwili ya kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Ruhudji na Rumakali.

Katika utekelezaji wa mipango ya Serikali, mradi wa umeme wa Rumakali utaanza kujengwa mwezi Julai, 2021 na utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 36.