Imeelezwa kuwa, Mkandarasi wa mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115), kampuni ya JV Arab Contractors na Elsewedy Electric ameanza rasmi kazi za ujenzi wa mradi huo tarehe 15/6/2019.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani tarehe 14/6/2019 mara baada ya kukagua kazi za maandalizi ya awali ya ujenzi wa mradi huo akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na watendaji wengine kutoka kampuni ya mkandarasi, Wizara ya Nishati na  TANESCO.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kushoto) akipata maelezo kuhusu hatua za ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji kutoka kwa Meneja Mradi wa Rufiji, Mhandisi Ahmed Ouda. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo.

Mkandarasi huyo ameanza ujenzi huo baada ya kufanya matayarisho mbalimbali  ikiwemo upelekaji wa vifaa vitakavyotumika katika shughuli za ujenzi, uwepo wa kambi za wafanyakazi, Ofisi na kukamilisha kazi nyingine za awali ambapo kwa mujibu wa mkataba, alipewa miezi Sita ya kufanya kazi hizo ambayo ukomo wake ulikuwa tarehe 14/6/2019.

Dkt Kalemani alisema kuwa, kazi anazoanza nazo ni upasuaji wa miamba ili kuruhusu maji kupita  kwenda kwenye mitambo ya kufua umeme.

Aliongeza kuwa,  kazi nyingine za awali zitakazofanywa ni kujenga daraja la muda litakaloruhusu upitishaji wa vifaa kwenda kwenye eneo jingine la kazi pamoja na ujenzi wa daraja la kudumu.

Baadhi ya majengo yanayotumika kama kambi za muda za wafanyakazi katika mradi wa umeme wa Rufiji (MW 2115).

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Dkt Kalemani alieleza kuwa, Mkandarasi ameahidi kukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Juni, mwaka 2022 na mradi utatekelezwa kwa kasi hivyo  ikiwezekana, megawati zote 2115 zitapatikana kwa wakati mmoja badala ya awamu kwa awamu.

Kuhusu vifaa vitakavyotumika kwenye mradi huo, Dkt Kalemani alimwagiza mkandarasi pamoja na wasimamizi wa mradi kutoka Tanzania kuhakikisha kuwa, wanatumia vifaa vinavyopatikana nchini na kwa vifaa visivyopatikana nchini, vitanunuliwa baada ya kupata kibali maalum.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akisalimiana na Faisal Tawfik, Meneja wa Rasilimali Watu kutoka kampuni ya JV AC EE, inayojenga mradi wa umeme wa Rufiji.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Pia aliagiza Wataalam wa ndani kupewa kipaumbele katika ujenzi wa mradi huo, ili waweze kusimamia mradi mara baada ya mkandarasi kukamilisha kazi.

Aidha, aliwapongeza TANESCO na TANROADS kwa kusimamia mradi huo ipasavyo, na kuwaagiza kuendelea kuwasimamia wakandarasi usiku na mchana.

Utiaji saini mkataba wa ujenzi  wa mradi wa umeme wa Rufiji kati ya Serikali ya Tanzania na Misri ulifanyika tarehe 12/12/2018  na mkandarasi alikabidhiwa rasmi eneo la mradi, Februari 14, 2019.

Na Teresia Mhagama