Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amekerwa na taarifa za kusuasua mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika kijiji cha Nyambili, Kata ya Bungu, Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, ambapo ameagiza mkandarasi anayesimamia mradi huo, Kampuni ya T & A Business Centre, kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza kijijini hapo baada ya kupokea malalamiko ya kusuasua kwa mradi, kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kijiji hicho, Mei 16, 2020, Naibu Waziri, aliutaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambao ndiyo mfadhili wa mradi, kuwasilisha wizarani, taarifa rasmi ya utekelezaji wake, ndani ya kipindi kisichozidi wiki moja.
“Taarifa hiyo ibainishe kwanini mradi umekwama, hali iliyofikiwa na hatua za kisheria zilizochukuliwa,” amesisitiza Naibu Waziri.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akisikiliza maelezo ya Msimamizi wa miradi ya REA, Kanda ya Pwani, Mhandisi Balisidya Myula, kuhusu mradi wa umeme jua unaotekelezwa katika kijiji cha Nyambili, Kata ya Bungu, Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, Mei 16, 2020 akiwa katika ziara ya kazi.

Vilevile, Mgalu alikiri kuwa ziara yake mahali hapo ni kufuatia malalamiko hayo yaliyomfikia kupitia kwa viongozi wa eneo hilo akiwemo Mbunge, Diwani na viongozi wa Chama Tawala (CCM).

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto), akizungumza na baadhi ya viongozi na wawakilishi wa wananchi wa kijiji cha Nyambili, Kata ya Bungu, Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, alipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa mradi wa umeme jua, Mei 16, 2020.

Maagizo mengine aliyoyatoa ni kwa REA kuandaa orodha ya miradi yote ya umeme katika maeneo yasiyofikiwa na gridi ya Taifa (Off-Grid) na kuiwasilisha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa nchi nzima ili viongozi waijue.

“Viongozi wanapaswa kujua miradi hiyo iko katika hatua gani, imeunganisha wateja wangapi na matarajio/malengo yake ni nini.”

Aidha, aliutaka Wakala huo pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kukaa na Mkandarasi husika na kufanya mapitio ya bei ya umeme huo ili isitofautiane na ile ya umeme wa TANESCO kama ambavyo alielekeza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.

Vilevile, Naibu Waziri aliagiza kijiji hicho cha Nyambili, kuondolewa katika orodha ya vijiji vyenye umeme maana kiuhalisia hakina umeme kutokana na idadi ya wananchi waliounganishiwa huduma hiyo kuwa ndogo sana na kwamba hata hao waliounganishiwa hawapati huduma hiyo ipasavyo.

Alishangazwa na kusikitishwa na matumizi ya pesa iliyotumika kufadhili mradi husika yasiyowiana na utekelezaji wake ambapo amewataka wataalamu wa Serikali kujenga utamaduni wa kuwajibika kama wanavyotakiwa ili kuhakikisha miradi mbalimbali wanayoisimamia inatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri alionya kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu wahusika wote, endapo itatokea tena mahali popote nchini, viongozi wa eneo husika kutokuwa na taarifa ya miradi ya aina hiyo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Awali, akiwasilisha taarifa ya malalamiko ya kusuasua kwa mradi husika, kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo, Mtendaji wa Kijiji cha Nyambili, Elia Clement, alibainisha moja ya changamoto wanazokabiliana nazo ni umeme kupatikana kwa masaa machache kwa siku.

Aidha, alisema tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi huo mwaka 2017, wananchi hawajawahi kupewa taarifa zozote zinazouhusu na wamekuwa wakilazimika kuzitafuta wao wenyewe kwa njia mbalimbali pasipo kupewa ushirikiano.
Clement alisema hata viongozi wa ngazi mbalimbali ikiwemo kijiji, kata na wilaya, hawapewi ushirikiano wa kufahamishwa kuhusu mradi husika.

Akitoa maelezo mbele ya Naibu Waziri, Msimamizi wa miradi ya REA, Kanda ya Pwani, Mhandisi Balisidya Myula alikiri kusuasua kwa Mkandarasi katika kutekeleza mradi husika na kwamba tayari Wakala huo umechukua hatua ikiwa ni pamoja na kumwandikia barua ya kusudio la kutaka kuchukua hatua za kisheria kuhusu mradi husika.

Akieleza zaidi, amesema mkandarasi ameunganisha wateja 10 tu hadi sasa kati ya 34 aliopaswa kuwaunganisha na kwamba kwa mujibu wa mkataba, alipaswa kukamilisha mradi mwanzoni mwa mwaka 2018 lakini hadi sasa hajakamilisha.

Mradi huo umegharimu shilingi 232,170,000 za Tanzania ambazo zilitolewa na wadau wa maendeleo kupitia Wakala huo.

Na Veronica Simba – Pwani